Ticker

6/recent/ticker-posts

Wildlife Park Mpya Kufungua Milango Ya Ajira Na Biashara Zanzibar

 


Uhifadhi wa wanyamapori unaendelea kupewa nafasi muhimu Zanzibar huku juhudi kubwa zikielezwa katika kuunganisha uhifadhi, utalii na fursa za uwekezaji katika kukuza kiuchumi kwa wananchi na jamii kwa ujumla.

Akizungumza na mwandishi wa habari, Mhifadhi Wanyamapori Mkuu na Mkuu wa Kanda Maalum ya Kituo cha Utalii Zanzibar kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania Dkt. Gladstone Fanuel Mlay amesema ushiriki katika maonesho ya Kizimkazi Festival ni sehemu ya kuendelea kuelimisha jamii kuhusu namna uhifadhi wa wanyamapori unavyoweza kwenda sambamba na maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hasa kwa kuwashirikisha vijana na wananchi katika shuhuli mbalimbali za uhifadhi.

Amesema maonesho ya Kizimkazi Festival 2026 yanatoa nafasi kwa wananchi kufahamu kwa karibu kazi zinazofanywa na TAWA katika kulinda wanyamapori na rasilimali za asili huku yakisisitiza umuhimu wa jamii kuwa sehemu ya ulinzi wa urithi wa Zanzibar.

Pamoja na hayo katika sehemu nyengine Mhifadhi Mkuu na Mkuu wa Kanda maalum ya Utalii Zanzibar ametangaza ujio wa mradi wa Zanzibar Wildlife Park ambao unatarajiwa kuanzishwa katika eneo la Msitu wa Jambiani Muyuni Paje ambapo unaotarajia kuongeza fursa ya wananchi na watalii kujifunza kuhusu wanyamapori katika mazingira rafiki na salama ambapo mradi huo ni miongoni mwa kivutio kipya na kikubwa katika sekta ya uhifadhi na utalii Zanzibar.

Amesema Zanzibar Wildlife Park itakuwa daraja muhimu kati ya uhifadhi,elimu na utalii ambapo wageni watapata fursa ya kufahamu aina mbalimbali za wanyamapori na umuhimu wa kuzilinda huku wakipata uzoefu wa kipekee unaounganisha uhifadhi, utalii na elimu ya mazingira.

Hata hivyo, amesema kuanzishwa kwa hifadhi hiyo kunatarajiwa kufungua fursa mbalimbali kwa vijana Zanzibar zikiwemo ajira katika uhifadhi,utalii, uongozaji wa watalii, huduma kwa wageni,huduma za malazi ,usimamizi wa mazingira pamoja na shuhuli mbalimbali za kibiashara zinazoweza kuzunguka eneo hilo.

Aidha, amesema kuwa mradi huo utatoa fursa kwa wajasiriamali hususan wanawake na vijana kupitia biashara za bidhaa za utalii na huduma nyengine zitakazohitajika na wageni watakaotembelea Zanzibar Wildlife Park.

Sambamba hilo amewashauri wananchi mbalimbali waweze kuweka utaratibu wa kutembelea vivutio vya utalii vinavyosimamiwa na Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa ajili kujionea Upekee wa vivutio hivyo vya utalii na kuweza kufarahia mandhari yanayotokana na vivutio hapa nchini.

Ameongeza kuwa Zanzibar Wildlife Park inatarajia kuwa ni sehemu ya kituo muhimu cha elimu kwa watoto na wanafunzi kutoka shule za msingi hadi vyuo vikuu, ambapo kizazi kipya kitapata nafasi ya kujifunza kwa vitendo kuhusu wanyamapori,utalii na mazingira ikiwa ni sambamba na mabadiliko ya tabia nchi na umuhimu wa kulinda viumbe hai kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi, sekta binafsi, vijana na wadau wa utalii kutumia fursa zinazotokana na maonesho ya Kizimkazi Festival na ujio wa Zanzibar Wildlife Park katika kuhakikisha wanunufaika na utalii kwa ujumla.

Alifahamisha kuwa uhifadhi ukiunganishwa na elimu utalii na uwekezaji unaweza kuifanya Zanzibar kuwa na fursa mpya za kiuchumi huku ikilinda urithi wake wa asili kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.


Post a Comment

0 Comments