Ticker

6/recent/ticker-posts

Utelekezaji Wa Watoto Ndani Ya Familia Bado Ni Changamoto Inayohitaji Hatua Za Pamoja

 


Na Ahmed Abdulla:

Utelekezaji wa watoto ndani ya familia umeendelea kuwa miongoni mwa changamoto zinazozikabili familia nyingi nchini, huku ukiathiri ustawi wa watoto, wanawake na maendeleo ya jamii kwa ujumla. Licha ya kuwepo kwa sheria zinazolinda haki za watoto, bado wapo watoto wanaokosa matunzo, malezi na huduma muhimu kutokana na baadhi ya wazazi au walezi kushindwa kutekeleza wajibu wao.

Akizungumza na makala hii, Mratibu wa Mradi wa Uwezeshaji wa Jamii kwa Ajili ya Haki za Binadamu na Utawala Bora chini ya Idara ya Maendeleo ya Jamii, Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Sister Editha Asiimwe, amesema utelekezaji wa watoto bado unaathiri ustawi wa watoto wengi na familia zao, hasa pale wazazi au walezi wanaposhindwa kutekeleza wajibu wao wa msingi.

Amesema mtoto anapokosa haki zake za msingi kama chakula, elimu, huduma za afya, malazi na malezi bora, huathirika kimwili, kiakili na kisaikolojia, hali ambayo huathiri mustakabali wake na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

"Mtoto ni amana kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hivyo kila mzazi ana wajibu wa kuhakikisha anapata haki zake zote za msingi. Kutotekeleza wajibu huo ni kumnyima mtoto fursa ya kufikia ndoto zake," amesema Sister Editha.

Ameeleza kuwa kupitia Mradi wa Uwezeshaji wa Jamii kwa Ajili ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Idara ya Maendeleo ya Jamii inaendelea kutoa elimu ya sheria kwa wananchi, kujenga uwezo wa wasaidizi wa sheria, kushirikiana na viongozi wa shehia pamoja na wadau mbalimbali katika kutatua migogoro ya kifamilia inayochangia utelekezaji wa watoto.

Kwa mujibu wake, lengo la mradi huo ni kuhakikisha haki za watoto zinalindwa, wazazi wanawajibika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na jamii inakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu wajibu wa kila mmoja katika malezi ya watoto.

Kwa upande wa jamii, Asha Ali, mama wa watoto wawili kutoka Kaskazini B Unguja, amesema baada ya kuachwa na mume wake amebaki akigharamia mahitaji yote ya watoto wake, ikiwemo chakula, elimu na huduma za afya, jambo linaloongeza ugumu wa maisha.

Naye Mwanahamisi Juma, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 15, amesema migogoro ya wazazi huwaathiri watoto moja kwa moja kwa kuwanyima utulivu wa kisaikolojia na wakati mwingine kuwafanya washindwe kuendelea vizuri na masomo kutokana na kukosa mahitaji muhimu.

Mzazi Salum Hassan amesema jamii inapaswa kuendelea kuelimishwa kuhusu wajibu wa wazazi kwa watoto.

"Kila mzazi anatakiwa kutambua kuwa malezi ya mtoto ni jukumu la wazazi wote wawili bila kujali tofauti zao. Watoto hawapaswi kuathiriwa na migogoro ya wazazi," amesema.

Mratibu wa Wanawake na Watoto wa Shehia ya Kitope, Sheni Mohd Juma, amesema ofisi yao hupokea na kushughulikia migogoro ya kifamilia pamoja na kufuatilia kesi zinazohusu watoto, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa jamii katika kulinda haki za watoto.

Kwa upande wa viongozi wa dini, Sheikh Salum Gharib Salum amesema dini zinawataka wazazi kuwalea na kuwahudumia watoto wao, huku akieleza kuwa mzazi anayeshindwa kutekeleza wajibu wake anakiuka mafundisho ya dini.

Naye Mchungaji Emmanuel Malingila wa Kanisa la Tanzania Assembly of God (TAG) Kitope amesema wazazi wanapaswa kuhakikisha watoto wanapata malezi bora, elimu, mavazi, malazi na mahitaji mengine ya msingi ili waweze kufikia ndoto zao.

Aidha, Hamis Juma Omar, baba wa mtoto mmoja, amesema migogoro ya ndoa mara nyingine huonekana kuwa ni kosa la upande mmoja, ilhali wakati mwingine pande zote mbili huchangia changamoto zinazoathiri watoto. Amesisitiza wazazi kutanguliza maslahi ya mtoto hata pale wanapoamua kuachana.

Msaidizi wa Sheria wa Shehia ya Kitope, Makungu Hamad Mwinyi, amesema wananchi wengi bado hawafahamu haki za watoto na taratibu za kuzidai. Amesema wasaidizi wa sheria wameendelea kutoa elimu ya bure ili kuongeza uelewa wa jamii.

"Kumtelekeza mtoto si suala la kifamilia pekee, bali ni ukiukwaji wa haki za mtoto unaoweza kuchukuliwa hatua za kisheria," amesema.

Kwa ujumla, wadau mbalimbali wanaamini kuwa kupambana na utelekezaji wa watoto kunahitaji ushirikiano wa wazazi, viongozi wa dini, viongozi wa shehia, wasaidizi wa sheria, taasisi za serikali na mashirika ya maendeleo. Wanasema kila mtoto anastahili kuishi katika mazingira salama yenye malezi bora, ulinzi na upendo ili aweze kukua na kuchangia maendeleo ya taifa.

Post a Comment

0 Comments