Na Ahmed Abdulla
Elimu ni haki ya msingi kwa kila mwanadamu, bila
kujali hali yake ya kimwili, kiakili au kihisia.
Kwa kutambua umuhimu wa haki hiyo, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo Idara ya
Maendeleo ya Jamii ya Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar kupitia Mradi wa
Uwezeshaji wa Jamii kwa Ajili ya Haki za Binadamu na Utawala Bora unaotekelezwa
na idara hiyo, wanaendelea kuhamasisha elimu jumuishi ili kuhakikisha watoto
wenye ulemavu wanapata fursa sawa za kujifunza, na kushiriki kikamilifu katika Shughuli
za kielimu.
Kwa watu wenye ulemavu, elimu jumuishi si huduma ya
ziada bali ni haki ya msingi inayowawezesha kupata maarifa, kujitegemea na
kushiriki kikamilifu katika maisha ya kijamii na kiuchumi. Watoto na watu wenye
ulemavu wanapopewa nafasi ya kujifunza pamoja na wenzao katika mazingira salama
na rafiki, hujengewa kujiamini, huondolewa vikwazo vya ubaguzi na kupewa nafasi
ya kufikia ndoto zao.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Sheria ya
Watu Wenye Ulemavu ya Zanzibar Na. 8 ya mwaka 2022, inayotambua haki ya kupata
elimu, kushiriki katika shughuli za maendeleo na kupata huduma mbalimbali bila
ubaguzi imeendelea kuweka mazingira mazuri ya kulinda haki za watu wenye
ulemavu.
Sambamba na juhudi hizo, taasisi zisizo za kiserikali
na mashirika ya dini zimeendelea kushirikiana na serikali katika kuhamasisha
jamii kuhusu umuhimu wa kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika nyanja zote za maisha.
Aidha, sera mbalimbali za maendeleo ya jamii na elimu
zinasisitiza usawa wa fursa kwa wananchi wote ili kuhakikisha hakuna anayebaki
nyuma katika safari ya maendeleo ya Zanzibar.
"Elimu jumuishi si msaada kwa watu wenye ulemavu,
bali ni haki yao ya msingi na msingi wa kujenga jamii yenye usawa."
Akizungumza na makala hii, Katibu wa Baraza la Watu
Wenye Ulemavu Zanzibar, Ussi Khamis Debe, alisema elimu jumuishi ni
nyenzo muhimu ya kuwapa watu wenye ulemavu uwezo wa kujitegemea na kushiriki
kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Alisema ili kufanikisha azma hiyo, ni muhimu shule
zote kuwa na miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu, walimu wenye ujuzi wa
elimu maalumu pamoja na vifaa vya kufundishia vinavyokidhi mahitaji ya
wanafunzi wote.
"Jamii inapaswa kuacha tabia ya kuwaficha watoto
wenye ulemavu majumbani. Watoto hao wanapaswa kuandikishwa shule mapema kama
watoto wengine ili wapate haki yao ya msingi ya elimu na kujenga maisha yao ya
baadaye," alisema.
Aliongeza kuwa elimu ndiyo njia bora ya kupunguza
utegemezi kwa watu wenye ulemavu na kuongeza idadi ya wananchi wenye uwezo wa
kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Awena Hassan Ali, kijana
mwenye ulemavu wa kuona ambaye pia ni mwalimu wa Skuli ya Msingi Kisiwanduwi na
mkazi wa Shehia ya Kitope, alisema elimu ndiyo iliyompa ujasiri wa kujiamini,
kujitambua na kushiriki kikamilifu katika jamii.
Alisema safari yake ya kutafuta elimu haikuwa rahisi
kutokana na changamoto mbalimbali alizokutana nazo, lakini hakukata tamaa kwa
kuwa aliamini elimu ndiyo njia ya kutimiza ndoto zake.
"Nilikutana na mitazamo hasi kutoka kwa baadhi ya
watu waliodhani siwezi kufanikiwa kutokana na ulemavu wangu. Lakini leo hii
mimi ni mwalimu na ninaendelea kulitumikia taifa kama wananchi wengine,"
alisema.
Awena alitoa wito kwa vijana wenye ulemavu kutumia
kila fursa ya elimu inayopatikana, huku akizitaka taasisi za elimu kuendelea
kuboresha mazingira ili yawe rafiki kwa wanafunzi wote bila kujali hali zao.
Baadhi ya wazazi waliozungumza na makala hii, akiwemo Naima
Hamad na Omar Fakih, walisema watoto wenye ulemavu wana
uwezo sawa wa kujifunza endapo watapatiwa mazingira yanayowawezesha kuonyesha
vipaji na uwezo wao.
Walisema wazazi wana wajibu mkubwa wa kuwahamasisha
watoto wao kwenda shule na kushirikiana na walimu katika kufuatilia maendeleo
yao ya kitaaluma.
Aidha, walisisitiza kuwa kuwaficha watoto wenye
ulemavu majumbani ni kuwanyima haki yao ya elimu na nafasi ya kutimiza ndoto
zao, wakieleza kuwa ushirikiano kati ya familia, shule na jamii ndiyo msingi wa
mafanikio ya watoto hao.
Elimu jumuishi ni msingi wa kujenga jamii yenye usawa,
haki na maendeleo endelevu. Kila mtoto, bila kujali aina ya ulemavu alionao,
anastahili kupata fursa sawa ya elimu bora itakayomwezesha kutimiza ndoto zake
na kuchangia maendeleo ya taifa.
Pamoja na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kupitia Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya Zanzibar Na. 8 ya mwaka 2022, mchango
wa wadau mbalimbali unaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuimarisha elimu
jumuishi.
Miongoni mwa wadau hao ni Idara ya Maendeleo ya Jamii
ya Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, ambayo kupitia Mradi wa Uwezeshaji wa
Jamii kwa Ajili ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaendelea kuhamasisha
jamii kuhusu haki za watu wenye ulemavu, kupinga ubaguzi na kuhimiza
upatikanaji wa elimu kwa wote.
Ni wajibu wa wazazi, viongozi wa dini, walimu,
viongozi wa jamii, taasisi za umma na binafsi pamoja na wananchi kwa ujumla
kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma kwa sababu ya ulemavu. Jamii inayowapa
watu wenye ulemavu fursa sawa za kujifunza na kushiriki katika maendeleo ndiyo
jamii inayojenga utu, usawa na mustakabali bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.


0 Comments