Ticker

6/recent/ticker-posts

Vijana Nguzo Ya Utawala Bora Na Maendeleo Endelevu

 




NA AHMED ABDULLA:

Mapema asubuhi katika kituo cha bodaboda Mahonda, Salum Juma anajiandaa kuanza safari za kuwahudumia abiria wanaokwenda kwenye shughuli zao za kila siku.

Wakati akisubiri wateja na kufanya safari mbalimbali, Salum hupata muda wa kushiriki mikutano ya kijamii na shughuli za maendeleo katika shehia yake.

Anaamini kuwa vijana hawapaswi kuwa watazamaji wa masuala yanayohusu maendeleo ya jamii zao, bali wanatakiwa kuwa washiriki wa moja kwa moja katika maamuzi yanayogusa maisha yao na mustakabali wao.

Kwa mtazamo wake, ushiriki wa vijana katika utawala bora ni njia muhimu ya kuhakikisha sauti zao zinasikika na mchango wao unatumika katika kujenga jamii yenye maendeleo na uwajibikaji.

Mtazamo wa Salum unaakisi hali halisi ya vijana wengi katika visiwa vya Zanzibar ambao wanazidi kutambua umuhimu wa kushiriki katika masuala ya utawala bora na maendeleo ya jamii.

Hata hivyo, bado kunahitajika juhudi zaidi za kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika mifumo ya maamuzi kuanzia ngazi ya shehia hadi taifa.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Zanzibar ina wakazi 1,889,773, ambapo vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 ni takribani 699,216 sawa na asilimia 37 ya wakazi wote.

Takwimu hizi zinaonesha kuwa vijana ni kundi kubwa lenye mchango muhimu katika maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii.

Kutokana na idadi hiyo kubwa, ushiriki wao katika masuala ya utawala bora ni jambo muhimu kwa maendeleo endelevu ya Zanzibar.

Utawala bora unahusisha uwazi, uwajibikaji, ushirikishwaji wa wananchi, utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu.

Katika mazingira hayo, vijana wanapaswa kuwa sehemu ya michakato ya maamuzi kuanzia ngazi ya familia, shehia, wilaya hadi taifa.

Ushiriki wao husaidia kuibua mawazo mapya, kuongeza uwajibikaji na kuimarisha maendeleo endelevu.

Akizungumza na makala hii, Salum, alisema ushiriki wa vijana katika shughuli za kijamii huongeza uwazi na uwajibikaji katika jamii.

“Vijana wana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko chanya wanapopewa nafasi ya kushiriki,” alisema.

Aliongeza kuwa viongozi wanapaswa kusikiliza maoni ya vijana kwa kuwa wao ni sehemu kubwa ya jamii. Pia aliwahimiza vijana kushiriki katika mikutano ya kijamii na shughuli mbalimbali za maendeleo badala ya kubaki watazamaji, kwani ushiriki huo huwajengea uwezo wa uongozi na kujiamini.

Asha Kombo Hamadi, ni kijana mjasiriamali anayejishughulisha na saluni ya wanawake katika Shehia ya Mahonda, alisema ushiriki wa vijana katika utawala bora huwapa nafasi ya kusikika na kutoa mawazo yao kuhusu maendeleo ya jamii.

“Vijana tusiposhiriki katika maamuzi ya leo, tutakuwa tunakosa nafasi ya kujenga kesho yetu,” alisema Asha.

Alieleza kuwa elimu ya uraia na utawala bora imechangia kuongeza uelewa wa vijana kuhusu haki zao na wajibu wao katika jamii. Aidha, alisisitiza matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kama chombo cha kuibua mijadala ya maendeleo na kuhimiza uwajibikaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Jumuia ya Vijana Elimu Kaskazini Unguja (JUVIEKA), Haji Abeid, alisema vijana wamekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika masuala ya utawala bora.

“Tunawawezesha vijana kupata elimu ya uraia ili wawe sehemu ya maamuzi ya maendeleo. Utawala bora hauwezi kufanikiwa bila ushiriki wa vijana,” alisema.

Alifafanua kuwa kupitia mafunzo mbalimbali, vijana wamekuwa wakifahamu zaidi haki zao za msingi na namna ya kushiriki katika mifumo ya uongozi.

Hali hiyo imeongeza mwamko wa vijana kushiriki katika harakati za maendeleo ikiwemo elimu, siasa na uongozi.

Akielezea mchango wa mashirika ya vijana katika kuimarisha ushiriki huo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Changamoto za Vijana Zanzibar (ZAFAYCO), Abdalla Abeid, alisema mashirika ya vijana yana jukumu la kuwaunganisha vijana na viongozi ili sauti zao zisikike.

“Tunajenga uwezo wa vijana kushiriki katika majukwaa ya maamuzi. Vijana wakipewa nafasi wanaweza kuwa chachu ya maendeleo endelevu,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Viongozi wa Shehia ya Mahonda, Khadija Ali Mohammed, alisema vijana ni washirika muhimu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Mawazo ya vijana yana mchango mkubwa katika kutatua changamoto za jamii. Tunawahimiza kushiriki kikamilifu katika vikao na mipango ya maendeleo,” alisema.

Alibainisha kuwa ushirikiano kati ya viongozi na vijana umechangia mafanikio ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.

Wazazi nao wanaona umuhimu wa kuwajengea vijana mazingira rafiki ya kushiriki katika maamuzi. Naima Hamad na Faki Haji Rashid, wakazi wa Mahonda, walisema vijana wanahitaji kuaminiwa na kupewa nafasi ya kuonyesha uwezo wao.

“Tukiwaongoza vizuri leo, watakuwa viongozi bora wa kesho,” walieleza.

Akizungumza kwa niaba ya Sheha wa Mahonda, Ali Issa alisema utawala bora huanza kwa kuwashirikisha wananchi wote, hususan vijana.

“Vijana ni nguvu ya maendeleo katika shehia zetu. Ni wajibu wetu kuwahusisha katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ili kujenga jamii yenye uwazi, uwajibikaji na ushirikiano,” alisema.

Mwanasheria wa Mradi wa Uwezeshaji wa Jamii kwa Ajili ya Haki za Binadamu na Utawala Bora unaotekelezwa na Idara ya Maendeleo ya Jamii Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Peter Maswi Marwa, alisema elimu ya utawala bora ni nyenzo muhimu inayowawezesha vijana kufahamu haki zao, wajibu wao na namna ya kushiriki katika michakato ya maendeleo.

“Vijana wanapopata elimu sahihi kuhusu utawala bora, wanakuwa sehemu ya suluhisho la changamoto zinazoikabili jamii yao,” alisema.

Aliongeza kuwa misingi ya utawala bora ni ushirikishwaji, uwazi na uwajibikaji, na vijana wana nafasi kubwa ya kuimarisha misingi hiyo.

Kupitia miradi ya uwezeshaji, vijana wanaendelea kujengewa uwezo wa kuwa raia wenye maarifa na wanaoshiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii na taifa.

Kwa ujumla, ushiriki wa vijana katika masuala ya utawala bora si jambo la hiari bali ni hitaji muhimu kwa maendeleo ya jamii na taifa.

Mafanikio ya utawala bora yanategemea ushirikiano wa wananchi wote, hivyo vijana wanapaswa kujitokeza, kutoa maoni yao na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Vilevile, viongozi na jamii wanapaswa kuendelea kuwawezesha na kuwaamini vijana ili waweze kutumia uwezo wao katika kujenga taifa lenye uwajibikaji, maadili mema na maendeleo endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.


Post a Comment

0 Comments