Na, Tatu Juma:
Waandishi wa habari wametakiwa kuongeza juhudi katika kuibua na kuripoti matukio ya udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana, ili kusaidia kubadili mitazamo ya jamii na kupunguza vitendo hivyo vinavyoendelea kuathiri maisha ya watu wengi.
Wito huo umetolewa na mwanachama mkongwe wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania upande wa Zanzibar (TAMWA-Zanzibar), Bi. Haura Shamte, alipokuwa akiendesha mafunzo kwa waandishi wa habari yenye lengo la kutoa uelewa wa namna bora za kuandika habari zinazohusu udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana yaliyofanyika Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema matukio ya udhalilishaji wa kijinsia yameendelea kushika kasi na kuathiri maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo kuna haja ya vyombo vya habari kuibua, kuripoti kwa weledi na kuelimisha jamii kuhusu madhara vitendo hivyo.
“Waandishi wa habari muna jukumu kubwa la kuibua na kuripoti matukio ya udhalilishaji ikiwemo mauaji, ukatili wa kingono na vitisho, ili jamii iweze kuelewa ukubwa wa tatizo na kuchukua hatua stahiki,” amesema Bi. Haura.
Bi haura amevitaja baadhi ya vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa wanawake na wasichana kuwa ni pamoja na Kushikwa maeneo ya mwili wao bila ya ridhaa,kutolewa maneno yanayoumiza kihisia pamoja na rushwa ya ngono katika baadhi ya maeneo ikiwemo madiko
Kwa upande wake, Afisa Programu kutoka TAMWA Zanzibar, Asia Hakimu, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa “Tunaweza Pamoja Kumaliza Udhalilishaji wa Kijinsia Dhidi ya Wanawake na Wasichana”, ambao unatekelezwa kwa muda wa miezi minane katika mikoa miwili ya Zanzibar ambayo ni Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba.
Ameongeza kuwa lengo la mradi huo ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari pamoja na wadau wengine ili kusaidia kupunguza na hatimaye kumaliza kabisa matukio ya udhalilishaji wa kijinsia katika jamii.
Amefafanua kuwa mradi huo utatekelezwa katika maeneo ambayo udhalilishaji hutokea kwa kiasi kikubwa, ikiwemo masokoni, maeneo ya usafirishaji, sehemu za uvuvi pamoja na biashara za mama ntilie, ambapo wanawake na wasichana hukumbana na vitendo vya udhalilishaji kwa kiwango kikubwa. Amesema elimu itakayotolewa itasaidia kupunguza na hatimaye kudhibiti vitendo hivyo kutokea.
Kwa upande wake, Afisa wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka TAMWA-ZNZ, Muhammad Khatib, amesema bado kuna changamoto ya uelewa mdogo miongoni mwa wananchi kuhusu namna ya kuripoti na kufuatilia kesi za udhalilishaji, hali inayosababisha baadhi ya matukio kubaki siri na kushindwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Amesema waandishi wa habari wana jukumu la kutumia kalamu zao kuelimisha jamii kuhusu haki zao, taratibu sahihi za kuripoti na umuhimu wa kufuatilia kesi hizo hadi mwisho ili kuhakikisha haki inapatikana.
Aidha, waandishi wa habari waliopatiwa mafunzo hayo wameahidi kuendelea kuibua na kuripoti matukio ya unyanyasaji wa kijinsia yanayofanyika katika maeneo mbalimbali ya kijamii ikiwemo masoko, madiko na usafiri wa umma, maeneo ambayo mara nyingi waathirika hukumbana na vitendo hivyo kwa kificho.
Wamesema wataendelea kutumia vyombo vya habari kuelimisha jamii na kuhimiza matumizi ya njia rasmi za kuripoti ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

0 Comments