Ticker

6/recent/ticker-posts

Safari ya Uzi Kuokoa Mazingira Kupitia Mradi wa ZanzAdapt

 


Na Ahmed Abdulla,Zanzibar

Miaka kadhaa iliyopita, pwani za Unguja zilianza kubeba alama za majeraha ya muda mrefu.

Mikoko ilikatwa hovyo kwa ajili ya kuni, maeneo muhimu ya kuzaliana samaki ikaharibiwa, na fukwe kuporomoka taratibu.

Wanawake waliotegea bahari kama chanzo cha kipato walianza kulalamika kupungua kwa kaa na kamba pamoja na viumbe vyengine vya baharini, huku wavuvi pia wakirudi nyumbani mikono mitupu, wakisema bahari “imechoka.”

Mashina ya mikoko yaliyoota kwa kustawi vyema yalibamizwa chini kwa mashoka, na maeneo yaliyokuwa makazi ya viumbe baharini yakabaki wazi kama ardhi ya jangwa.

Mikoko, ambayo ilionekana kama miti ya kawaida tu, ilitoweka kimya kimya lakini madhara yake yakavuma zaidi katika maisha ya wananchi.

Hata hivyo, kama ilivyo kawaida ya bahari kuanza safari mpya kila alfajiri, ndivyo matumaini mapya yalivyoanza kuchipua.

Kwa sasa, matumaini hayo yanaonekana wazi kabisa kupitia mradi wa ZanzAdapt ambao umeleta uhai mpya katika maeneo yaliyowahi kuteseka.

Asubuhi katika kijiji cha Uzi, upepo unapopita katika matawi ya mikoko mipya unatoa sauti ya uhai unaorudi.

Miche inayoinuka polepole kutoka kwenye matope ni kama ishara ya mustakabali mpya ishara ya ardhi inayofufuka na jamii inayopata tena nguvu ya kujitegemea.

Meneja wa Mradi wa ZanzAdapt Kanda ya Unguja, Ali Said, anaeleza kuwa mafanikio yanayoonekana leo ni ushahidi tosha kuwa jamii inapopewa mwanga na ushirikishwaji sahihi, inaweza kuandika upya historia ya mazingira yake.

“Tulishuhudia uharibifu mkubwa miaka ya nyuma. Lakini sasa jamii imeamka. Wananchi wanaielewa thamani ya mikoko, na wengi wanaiona kama ngao ya mustakabali wao,” anasema.

Anasema kuwa uelimishaji huo umegeuka kuwa injini ya mabadiliko makubwa. Wananchi sasa si mashuhuda tu wa mabadiliko, bali ni washiriki wakuu wanapanda, wanatunza, na kusimamia rasilimali hizi kwa uangalifu wa mtu anayelinda kesho yake.

Anaongeza kuwa zaidi ya uhifadhi, mradi umefungua milango mipya ya kiuchumi kupitia ufugaji wa nyuki katika maeneo ya mikoko.

Mapato yanayotokana na asali yameongeza nguvu katika uchumi wa familia bila kuathiri mazingira.

“Ufugaji wa nyuki umeleta mabadiliko ya kweli. Watu wanapata kipato bila kuharibu mazingira,” anasisitiza Ali Said.

Aidha, anasema vitalu vya miche ya mikoko vimekuwa uti wa mgongo wa safari hii ya urejeshwaji. Kitalu cha Unguja Ukuu kimezalisha takribani miche 17,000, huku cha Uzi kikijivunia zaidi ya miche 22,000, hatua ambayo imeongeza kasi ya kufufua maeneo yaliyoharibika zaidi.



Makame Simai Makame, mhamasishaji jamii kwenye masuala ya uhifadhi wa mikoko katika kisiwa cha Uzi, anasema hatua zinazoshuhudiwa leo ni matokeo ya nguvu ya elimu na ushirikishwaji wa wananchi.

“Ni jambo la kufurahisha sana kuona jamii imeanza kuelewa thamani ya mikoko,” anasema. “Leo wananchi wenyewe ndiyo walinzi wa kwanza wa maeneo haya jambo ambalo halikuwepo zamani.” Anafafanua kuwa mikoko mipya iliyopandwa inaendelea kuota vizuri, ishara ya mustakabali salama kwa kisiwa hicho. “Mikoko mipya tuliyopanda inaendelea kuota vyema. Tuna matumaini makubwa kisiwa chetu kubaki salama dhidi ya tabianchi.”

Hata hivyo, Makame anaomba watekelezaji wa mradi kuongeza vifaa vyao vya kazi ili waendelee kufanya majukumu yao kwa ufanisi zaidi katika misimu yote. “Tunahitaji makoti, buti za mvua na vifaa vya usalama. Uhifadhi ni kazi ya muda wote, na tunapaswa kulindwa,” anasema akiwa na matumaini kuwa mahitaji haya yatapewa kipaumbele.

Sauti za wanajamii wengine zinaendelea kuupa nguvu mradi huu ambapo Amina Khatib Mwamba, mmoja wa wanahifadhi wenye uzoefu, anaamini kuwa mikoko ndiyo uti wa mgongo wa maisha ya pwani.

“Tunapopanda mche mmoja, tunalinda ardhi, nyumba na riziki ya watoto wetu. Huu ni urithi unaohitaji kulindwa na kizazi chetu cha sasa,” anasema kwa msisitizo.

Naye Hadia Ali Muhammed, anasema kuwa ulinzi wa mikoko ni jukumu la jamii nzima. “Vijana lazima wajitokeze zaidi, kwa sababu mikoko ndiyo kinga yetu ya mwisho dhidi ya athari za tabianchi,” anasisitiza akisisitiza ushirikiano wa vizazi vyote.

Tafiti za kisayansi zinathibitisha umuhimu mkubwa wa mikoko katika ustawi wa mazingira na maisha ya watu.

Misitu ya mikoko hupunguza kasi ya mawimbi kwa zaidi ya asilimia 60, jambo linalosadia kupunguza athari za mafuriko na mmomonyoko wa ardhi.

Mizizi yake iliyosokotana hutoa makazi muhimu ya kuzaliana kwa samaki, kaa na kamba viumbe wanaotegemewa na wavuvi kwa ajili ya kitoeleo.

Zaidi ya hayo, mikoko ni hazina kubwa ya kaboni ambapo ekari moja ya mikoko inaweza kuhifadhi kaboni mara tatu zaidi ya msitu wa nchi kavu, hivyo kuwa chombo muhimu katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Katika kisiwa cha Uzi na baadhi ya maeneo mengine ya Unguja, mikoko inasimama kama ushuhuda hai kuwa pale jamii inapojengewa uwezo, mazingira yanaweza kufufuka, uchumi unaweza kustawi, na mustakabali unaweza kuandikwa upya kwa matumaini mapya.

Post a Comment

0 Comments