Na Berema Nassor, Zanzibar
Katika karne ya 21, matumizi ya vidonge vya kuzuia mimba yameongezeka kwa kasi, hasa miongoni mwa wanawake vijana. Moja ya vidonge vinavyotumika sana ni Postinor 2 (P2), kidonge cha dharura kinachotumika baada ya tendo la ndoa lisilo salama.
Ingawa P2 ni msaada mkubwa kwa wanawake waliopata dharura ya ngono bila kinga, matumizi holela na ya mara kwa mara yameibua wasiwasi mkubwa wa kiafya, kisaikolojia, na kijamii.
Moja ya madhara yanayojirudia mara kwa mara ni kutokuwepo kwa mzunguko wa hedhi wa kawaida. P2 hubadilisha kiwango cha homoni mwilini, jambo linalosababisha hedhi kuchelewa, kutoka mara mbili kwa mwezi, au kutotokea kabisa kwa muda fulani.
Aidha, baadhi ya wanawake hupata maumivu ya tumbo, kichwa kuuma, kichefuchefu, au kutapika. Hali hizi huwa mbaya zaidi kwa wale wanaotumia P2 mara kwa mara, kwani mabadiliko ya homoni yanaathiri mwili.
Tafiti zinaonyesha kwamba matumizi ya mara kwa mara yanaongeza hatari ya matatizo ya uzazi.
Utafiti wa Khasiani et al. (2021) ulionyesha kwamba wanawake wanaotumia P2 mara kwa mara walipata mabadiliko ya hedhi 32% zaidi kuliko wale waliotumia kwa dharura pekee.
Aidha, ripoti ya WHO (2022) inaonyesha kwamba takriban 45% ya wanawake wanaotumia vidonge vya dharura hutumia zaidi ya mara moja kwa mwaka, jambo linaloongeza hatari ya mizunguko isiyo ya kawaida ya hedhi na matatizo ya homoni.
Dk. Nicolas Kikoti, mtaalamu wa masuala ya wanawake kutoka Hospitali ya Wilaya Ijitimai, alisema:
“Wanawake wanaotumia P2 mara kwa mara huishi kwa hofu na msongo wa mawazo, hasa kutokana na hofu ya kupata mimba au madhara ya kiafya. Hali hii inaweza kuathiri afya ya akili na mahusiano yao.”
Aliongeza kuwa kutegemea P2 mara kwa mara kunaweza kufanya baadhi ya wanawake au wapenzi wao kupuuza kondomu, jambo linaloongeza hatari ya maambukizi ya magonjwa ya zinaa (STIs) kama VVU, kisonono, na kaswende, kwani P2 haikingi dhidi ya magonjwa haya.
Asia Omar Zubeir, mkaazi wa Fuoni, alisema ni kawaida wasichana wengi kutumia P2 kwa ajili ya kujikinga na mimba isiyotarajiwa, huku pia akieleza kuwa kuna haja ya kutoa elimu kuhusu matumizi ya dharura ya vidonge hivyo.
“P2 si njia ya kudumu au mbadala wa uzazi wa mpango, bali ni suluhisho la dharura pekee.” Alisisitiza
Alisisitiza kwamba kuendelea kutumia P2 mara kwa mara kunaweza kuvuruga homoni, mzunguko wa hedhi, na afya ya uzazi kwa muda mrefu.
Aidha, elimu sahihi kwa wanawake inaweza kupunguza madhara yanayotokana na matumizi holela ya P2.
Rehema Abdalla Makame ni Muuguzi wa Afya ngazi ya jamii kutoka shehia ya Mwera alisema ni wakati wa kuwaelimisha wasichana juu ya madhara yatokanazo na matumizi holela wa vidonge hivyo.
“Wasichana wanatumia hizi dawa kiholela wakidhani wako salama lakini si salama kama wanavyodhani tuendelee kuwaelimisha” alisema
Ali Vuai Hija Mkaazi wa Mtopepo Zanzibar alisema hajawahi kushuhudia wasichana wakitumia dawa hizo licha ya taarifa kuzagaa juu yatumizi ya dawa hizo hapa Zanzibar.
“Sijawahi kuwashuhudia lakini kama linazungumzwa litakuwa linaukweli hivyo ni budi wataalamu wa afya kufanya kazi ya ziada kuondoa matumizi haya” alimaliza
Kwa msingi huo P2 ni msaada mkubwa katika kudhibiti mimba zisizotarajiwa kwa dharura.
Matumizi yake bila mpangilio wa kitabibu yanaweza kusababisha madhara makubwa kiafya, kiakili, na kijamii.
P2 si mbadala wa njia rasmi za uzazi wa mpango; inapaswa kutumika mara chache na kwa dharura tu.
Elimu zaidi kuhusu uzazi wa mpango na P2 inahitajika ili wanawake waweze kufanya maamuzi sahihi ya kiafya.
0 Comments