Na Ahmed Abdulla,Zanzibar:
Kwa muda mrefu jamii nyingi za Kiafrika zimekuwa na mtazazmo kwamba uongozi ni haki ya wanaume,huku wanawake wakisukumwa pembeni na changamoto kadhaa katika kugombea nafasi mbali mbali za uongozi.
Pamoja na changamoto wanazopitia katika kutafuta nafasi za uongozi lakini wapo wanawake ambao wana uthubutu wa kujiamini katika kugombea nafasi za uongozi hasa zile nafasi za kugombea majimboni ambazo wanawake wengi wanahofia kuingia katika ulingo wa kugombea nafasi hizo kutokana na mitazamo tofauti iliyojengeka katika jamii kuwa wanawake wana nafasi zao.
Lakini hilo limethibitishwa na Muwakilishi wa jimbo la Konde Zawad Amour Nassor aliyeanza kupata nafasi ya uongozi katika jimbo hilo ambalo kwa upande wa wanawake ni kikwazo na changamoto kubwa kupata nafasi ya kuongoza majimboni.
Kutoka kijiji cha konde,Pemba hadi ndani ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar safari ya Zawadi Amour Nassor ni hadithi ya uthtbutu ujasiri na upendo kwa watu wake.
Zawadi alianza kama mwalimu wa shule ya msingi ya Konde akihamasisha watoto wa kike kuamini kwamba elimu ni silaha ya maendeleo yaliyo bora hasa kukiwa na kiongozi mwanamke ,kupitia ualimu wake alipata kuona changamoto za jamii watoto wanaoshindwa na shule, wanawake wanaokosa nafasi za maamuzi na vijana wanaopoteza matumaini.
Hapo ndipo akaamua kuingia kwenye siasa si kwa umaarufu bali ni kwa nia ya kubadilisha hali ya maisha ya wananchi wake pamoja na kuondoa dhana inayowakwaza wanawake kuwa uongozi ni kwa ajili ya wanaume pekee tu.
Safari yake ya uongozi ilianza mwaka 2019 katika kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kiongozi mwanamke katika jamii ambapo mwaka 2020 alichaguliwa kuwa mwakilishi wa jimbo la Konde ikiwa ni miongoni mwa wanawake wachache waliofanikiwa kuvuka vizingiti vya kijinsia.
“Nilipoanza kampeni wengi walinicheka lakini nilijua nikiwa na imani na wananchi
wangu hakuna lisilowezekana alieleza Zawad.”
Safari yake haikuwa nyepesi kama mwanamke aliyeingia katika anga za siasa huku akikabiliwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kiume,dharau za kijinsia na upungufu wa rasilimali fedha .
Lakini kupitia uthubutu na busara alisimama imara akithibitisha kwamba changamoto si kikwazo bali ni darasa la kujifunza na kukua ambalo litakujengea uwezo wa kujiamini katika kile unachokitafuta.
“Wanawake si wanyonge,ila wanakosa nafasi za kuonyesha uwezo wao hivyo nilipambania kwa nguvu zangu zote katika nafasi hiyo hatimae niliweza alisema Zawad.”
Zawadi Amour Nassor amekuwa kinara wa kuhimiza na kuhamasisha utekelezaji wa mikataba na sera za kimataifa zinazolenga usawa wa kijinsia ikiwemo Mkatabna wa CEDAW (1979) unaolenga kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake pamoja na Azimio la Being (1995) lililosisitiza uwezeshaji wa wanawake katika maamuzi ya kitaifa.
Pia Sera ya Jinsia ya Zanzibar inayohamasisha ushiriki sawa wa wanawake katika Nyanja zote za kijamii na kisiasa sambamba na hilo Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG 5) inayolenga usawa wa kijinsia.
Kupitia msimamo wake thabiti Zawad Amour Nassor amekuwa akikisitiza utekelezaji wa mikataba hii kwa vitendo na wala si maneno bali ni kuonesha kuwa utekelezaji wa sera hizi ni kichocheo cha maendeleo ya taifa zima.
Alisema miongoni mwa maendeleo anayojivunia ni kusambaza huduma ya nishati ya umeme maji safi na salama pamoja na kuwashajihisha wanafunzi kuweka kipaumbele sekta ya elimu na kuwasadia kwa kupelekea vifaa vya kusomea kama vitabu na computer.
Katika sekta ya afya Mwakilishi Zawad aliweza kupeleka madaktari wa magonjwa ya moyo katika hospital ya Konde pamoja na gari ya kubebea wagonjwa jambo ambalo liliweza kuleta mafanikio makubwa katika sekta hiyo.
Vile vile alisema aliwapatia mafunzo ya ujasiriamali vijana wa kike katika sekta ya ushoni ili waweze kujiajiri wenyewe jambo ambalo litasaidia kukuza uchumi wao katika familia na jamii kwa ujumla.
Hata hivyo makala hii ilizungumza na Mkuu wa wilaya ya Micheweni Khatib Juma Mja akielezea uongozi wa Mwakilishi huyo katika kushirikiana na serikali ya wilaya hiyo alisema Zawad Amour ni kiongozi ambaye anashirikiana kikamilifu na serikali ya wilaya ambapo aliweza kusaidia na kutatua changamoto mbali mbali katika jimbo lake ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama,mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana wakike pamoja na kuimarisha sekta ya afya.
“Mwakilishi Zawad Amour anashirikiana vyema na serikali ya wilaya katika harakati zake za kuwatumikia wananchi wa jimbo lake kupitia uongozi wake wananchi wamepata mafanikio makubwa kwani kiongozi mwanamke ni mwenye maono ya mbali ya mafanikio na muwajibika wa hali ya juu alieleza Mkuu wa wilaya huyo.”
Siti Hamad Memba mkaazi wa konde alisema tangu Zawad Amour achaguliwe kuwa mwakilishi wao ameona mabadiliko makubwa ya kiuchumi hasa kwa wanawake.
“Ametuhamasisha kujitegemea kuanzisha miradi ya mikopo na kujifunza elimu ya ujasiriamali ni kiongozi wa vitendo alieleza Siti Hamad”
Alisema mafanikio ya Mwakilishi huyo yameleta heshima kwa wanawake wa konde hivyo ameonyesha kuwa mwanamke anaweza kuongoza na kubadilisha mtazamo katika jamii juu ya umuhimu wa kiongozi mwanamke kwa maslahi ya jamii na taifa kwa ujumla.
Hamis Said Ali mkaazi wa Konde Sokoni alisema wanajivunia na kiongozi huyo kutokana na utekelezaji wake kuwatumikia wananchi wa rika zote bila ya ubaguzi wowote.
“Tunajivunia kuongozwa na mwanamke kwani aliweza kusajili timu 26 katika ligi ya za za mpira wa miguu kwa ngazi tofauti na kuendelea na matengenezo ya uwanja wa mpira wa Konde ni jambo la faraja kwa vijana na wapenda michezo katika jimbo hilo.
Alisema ni vyema jamii iendelee kushirikiana na viongozi wanawake kwani wanawake ni viongozi ambao hupambania maendeleo na mafanikio ya kasi zaidi hivyo mwanamke sio dhaifu bali ni kiongozi shupavu na mwenye mtazamo wa mbali kimaendeleo alieleza Hamis”
Hivyo basi safari ya Zawad Amour imedhihirisha kuwa uongozi bora haupimwi kwa jinsia bali ni dhamira uwezo na maadili.
Mwakilishi wa Jimbo la Konde ni mfano wa kiongozi mwanamke anayebeba matumaini ya mabadiliko na kupasua ukuta wa ubaguzi na kuthibitisha kwamba wanawake wanaweza kushika nafasi za juu za uongozi kwa mafanikio.
Pia ni kielelezo cha uthubutu na mfano hai kwamba mwanamke akipewa nafasi anaweza kufanya makubwa zaidi kuliko mwanaume hivyo anaendelea kuwa sauti ya wanawake vijana na jamii ya Konde akiweka historia mpya ya uongozi wa kizazi kipya cha wanawake visiwani Zanzibar.

0 Comments