Ticker

6/recent/ticker-posts

Kuwawezesha Watu Wenye Ulemavu Katika Sekta Ya Uchumi Ni Hatua Muhimu Katika Mafanikio Ya Ujumuishaji

Baadhi ya wanavikundi vya KIJALUBA baada ya kukamilisha mafunzo ya utengenezaji wa Achari na Pilipili yaliyofanyika Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja.

Na Ivan Mapunda:

Dunia sasa ipo kwenye harakati na mapambano ili kufanikisha ujumuishaji na ukondoeshaji wa masuala ya watu wenye ulemavu katika kila sekta.

Zanzibar kwa upande wake inajitahidi katika kuhakikisha kuwa inawafikia kimaendeleo wananchi wake wote bila kubagua jinsia au hali ya ulemavu, na hii inachangiwa na utendaji mkubwa wa Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu ambalo limekua chachu kubwa ya kukumbusha masuala ya watu wenye ulemavu pindi yanapoonekana kusahauliwa katika sekta fulani.

Katika kuwawezesha watu wenye ulemavu kiuchumi, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Shirikisho la Jumuiya za watu wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA) na Chama cha Watu wenye Ulemavu Nchini Norway (NAD) wameanzisha mradi maaalum wa vikundi vya kuweka na kukopa unaojulikana kama Kijaluba, mradi ambao umekuwa chachu katika maisha ya watu wenye ulemavu, wakionyesha jinsi gani fursa za kiuchumi zinavyoweza kubadilisha maisha yao.

Mradi wa KIJALUBA iSAVE umeleta fursa za kiuchumi kwa washiriki na wanachama wa vikundi hivyo kwani wamepata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali iiwemo uchaguzi wa biashara lakini pia utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za biashara.

Akizungumzia mafanikio aliyoyapata katika mradi wa KIJALUBA mmoja wa wanufaika wa mradi huo kutoka katika kikundi cha SUBIRA HUVUTA KHERI amesema kuwa vikundi hivyo vimekuwa nguzo muhimu katika kutoa fursa za mikopo na kutoa mwongozo katika kuanzisha miradi ya kibiashara na shughuli nyingine za kujipatia kipato.

Aliongeza kuwa washiriki katika kikundi chake wamechukua hatua za kuanzisha miradi midogo midogo inayolingana na uwezo wao ikiwemo ususi wa mikoba, utengenezaji wa achari na pilipili, kilimo, ufundi, na huduma mbalimbali iuli kuweza kujikomboa kiuchumi na kuepukana na utegemezi. 

“Kwa kweli kupitia mradi huu watu wamekomboka, nikiwemo na mimi, tunachukua mikopo ndani ya kikundi chetu bila masharti magumu na hiyo inatusaidia kuanzisha biashara zetu ndogo ndogo na kujikwamua kiuchumi”, alisema.

Alidha aliongeza kuwa vikundi vya kuweka na kukopa vimekuwa chanzo cha kuongeza kipato kwa washiriki na kuwaepusha na kuwa tegemezi. 

“Angalau sasa tunaweza kujikimu wenyew, ile tabia ya kuomba omba si nzuri, biashara tulizozianzisha zimetusaidia kuepukana na utegemezi na sasa tunasimamia familia zetu wenyewe kuanzia kulisha hadi kusomesha”, alisema. 

Mwanaidi Haji ni mwenyekiti wa kikundi cha SIKUDHANI kutoka Kusini Unguja alisema mafanikio makubwa yaliyopatikana na kujiunga na vikundi hivyo ni kujiwezesha kiuchumi na kupata mbinu mbalimbali za kufanya biashara na kujiongezea kipato.  

Nae Zaituni Zamiri ambae ni mnufaika wa mradi wa mradi wa Kijaluba amesema kuwa vikundi hivi vya kuweka na kukopa vimefungua fursa mpya za biashara kwa watu wenye ulemavu na hivyo kuwanufaisha kiuchumi. 

Khairat Haji ni afisa mradi kwa upande wa Pemba ameeleza mfanikio ya mradi mpaka sasa ambapo anasema hadi sasa  mradi huo umeshatoa mafunzo mbalimbali kwa washiriki kuhusu uchaguzi wa biashara na jinsi ya kuiendesha, stadi za biashara, ujasiriamali, na usimamizi wa fedha. 

“Mpaka sasa mradi umeshatoa mafunzo mengi, kuanzia kwenye kuufahamu mradi na utekelezaji wake hadi kwenye uanzishaji na uchaguzi wa biashara, na sasa tunaendelea na mafunzo ya biashara mbalimbali kama achari, ususi wa mikoba, kilimo cha mboga mboga na mengineyo”, alieleza

Khairat aliongeza kuwa muitikio wa watu wenye ulemavu wa kujiunga na vikundi hivyo unaonesha wazi kuwa sasa ni muda wa watu wenye ulemavu kuingia na kushiriki katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo, akiba zao wanazoziweka kwenye vikundi inatosha kuonesha muamko wao na kwamba sasa ulemavu sio kikwazo tena wala sio sababu ya umasikini.

Katika hatua nyingine mwalimu wa vikundi hivyo kwa upande wa kanda ya pwani, Mohd Ali alieleza kuwa mradi huu umeleta mabadiliko katika mitazamo ya kijamii kuhusu watu wenye ulemavu na kuthibitisha kuwa wanaweza kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya jamii na kwamba wao pia ni sehemu ya jamii.

Mradi wa KIJALUBA umekua ni fursa nzuri ya kuwakomboa kiuchumi watu wenye ulemavu, kupitia mradi huu watu wenye ulemavu wamepiga hatua muhimu katika kuepukana na utegemezi lakini pia inasaidia kuona ni kwa namna gani Zanzibar inaenda kufikia hali ya ukondoeshwaji wa masuala ya watu wenye ulemavu katika kila sekta. 


Post a Comment

0 Comments