Ticker

6/recent/ticker-posts

Umuhimu Wa Mama Mjamzito Kuhudhuria Klinik Na Mwenza Wake


Na Ahmed Abdulla, Zanzibar

Hudhurio la klinik kwa mama mjamzito ni hatua muhimu katika kuhakikisha afya bora ya mama na mtoto lakini mara nyingi jambo hilo huonekana kama ni jukumu la mwanamke pekee yake huku baba akibaki nyuma kufanya shuhuli zake nyengine.

Ni wakati sasa jamii ielewe kuwa klinik ni safari ya pamoja inayomhusisha mwenza pia.
Mama mjamzito anapohudhuria klinik na mwenza wake anapata faraja ya kihisia na hofu zake hupungua hivyo anaona wazi kuwa hajabeba jukumu la ujauzito pekee yake bali wapo pamoja katika safari ya malezi.

Khairat Salum Abdalla ni muuguzi na mkunga katika hospitali ya Wilaya kitogani iliyopo wilaya ya mkoa wa Kusini Unguja akizungumza na Zanlight blog alisema baba anapohudhuria klinik na mwenza wake anapata elimu ya moja kwa moja kuhusu lishe,dalili hatarishi, na umuhimu wa kumuandaa vyema mwenza wake kujifungua salama .

‘’Hudhurio la klinik pamoja na mwenza hutoa nafasi ya kupima afya ya familia nzima kujua historia ya magonjwa na kupanga uzazi kwa usalama hivyo basi baba anaposhirikiana inarahisisha utekelezaji wa ushauri wa kitabibu nyumbani.’’

Alisema jambo jengine ambalo ni muhimu kwa baba kuhudhuria klinik na mwenza wake anapata elimu ya moja kwa moja kuhusu lishe, dalili hatarishi na umuhimu wa kumuaandaa vyema mama mjamzito kwa kujifungua salama hivyo ushiriki wake hupunguza mambo mengi kwa mama huyo ikiwemo msongo wa mawazo.

Pamoja na hayo makala hii ilizungumza na Asha Hussein mjamzito wa miezi mitano mkaazi wa Regeza mwendo wilaya ya Magharib ‘A’ alisema unapohudhuria klinik na mwenza wako inasaidia kujua matatizo ambayo wajawazito wanayapitia maana wanaume walio wengi hawajui chamgamoto tunazozipitia wakati wa ujauzito.

‘’Nilipofika klinik na mume wangu nilihisi fahari kubwa na aliposikia maelezo ya daktari alielewa zaidi changamoto zangu na sasa amenisaidia hata kwenye lishe.’’ alieleza biasha

Kwa upande wake Kombo Haji Faki mume wa Biasha alisema kushirikiana na mwenza wako katika safari ya klinik hutoa fursa ya wanandoa kupima afya zao ikiwemo Virusi vya ukimwi, hivyo inasaidia kupanga maisha ya familia kwa uelewa na uwazi zaidi.

‘’Awali niliona klinik ni mambo ya wanawake tu nilipoanza kuhudhuria nilijifunza umuhimu wa kupima afya yangu ma mikajua namna ya kumsaidia mke wangu kwa vitendo’’alieleza Kombo Haji.

Alieleza kuwa mara nying mama mjamzito huhimizwa kula chakula bora lakini ikiwa mume hajui umuhimu wake huweza kutozingatia lakini kupitia klinik baba hupewa mwongozo wa moja kwa moja wa namna ya kumuandalia mama lishe bora.

Pamoja na hayo aliwataka wanaume wenzake kuweka utaratibu wa kufuatana na wenza wao kwenda klinik pindi tu wanapokuwa wajawazito hii itasaidiwa kujua maendeleo ya hali yake kabla ya kujifungua na baada ya kujifungua.

Mwanajuma Othman Hamis muhudumu wa afya ngazi ya jamii shehia ya mwera alisema miongoni mwa juhudi wanazozifanya ni kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kuhudhuria klinik mapema huku wakiongozana na wenza wao ili waweze kujua matatizo na changamoto wanazozipitia mama wajawazito wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.

‘’Tunapoona baba akienda klinik na mke wake,jamii nzima hupata somo kuwa malezi ya mtoto yanaanza tangu tumboni jambo ambalo linapelekea kujua hali ya afya ya mwenz wake inavyoendelea’’ alieleza Mwanajuma Othman.

Tafiti zinaonesha kuwa akina baba wanaoshirikiana tangu mama akiwa mjamzito hupunguza migogoro ya kifamilia na visa vya ukatili hivyo klinik ya pamoja inajenga mshikamano wa ndoa na malezi bpra ya mtoto.

Hudhurio la klinik na mwenza wako si jambo la hiyari bali ni jukumu la familia na jamii nzima inapaswa kuhamasika katika mashirikiano ya pamoja ya kuhudhuria klinik ili kuweza kuhakikisha matatizo wanayopitia mama wajawazito yanaweza kutatuliwa kwa pamoja.

Post a Comment

0 Comments