Na Thuwaiba Habibu , Zanzibar
Ushiriki wa wanawake katika siasa umekuwa ukikua kwa kasi katika nchi mbalimbali barani Afrika, licha ya changamoto nyingi zinazowakabili.
Katika miaka ya hivi karibuni, mataifa kama vile Rwanda, Ethiopia, Liberia, Tanzania, yameshuhudia ongezeko la idadi ya wanawake wanaochukua nafasi za uongozi wa kisiasa, ambao kwa kiasi fulani wamevunja vikwazo vya kijamii, kiuchumi na kisheria.
Rwanda, ni nchi pekee iliyoweka historia ya kuwa na idadi kubwa zaidi ya wanawake wabunge duniani, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya viti vya bunge vinashikiliwa na wanawake, Ethiopia pia imepiga hatua kwa kumteua Sahle-Work Zewde kuwa Rais wa kwanza mwanamke, huku akihimiza usawa wa kijinsia katika nafasi za juu za uongozi.
Nae Ellen Johnson Sirleaf kutoka Liberia aliandika historia kama Rais wa kwanza mwanamke kuchaguliwa kidemokrasia barani Afrika (2006–2018), Naye Samia Suluhu Hassan, ndiye Rais wa kwanza mwanamke kutoka Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania kuanzia 2021.
Viongozi hawa ni chachu ya mabadiliko ya kijinsia, na ishara kuwa wanawake wana nafasi kubwa katika kuleta maendeleo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Kutokana na muamko huo Tanzania ikiwa inaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, wanawake wanaonesha nia na ari kubwa ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, kuanzia ngazi za chini hadi juu. Hata hivyo, safari ya mafanikio yao bado inakumbwa na vizingiti ambavyo wapo tayari kupambana navyo kuhakikisha wanashinda katika uchaguzi huo.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2022 inaonesha kuwa zanzibar ina jumla ya wakaazi 1,889,773 wanaumme 915,492 na wanawake 974,281.
Licha ya idadi kubwa ya wanawake na kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi ni lazima kwao kutengeneza fursa za kushinda vikwazo ili kufanikiwa kwa urahisi katika uchaguzi wa 2025.
Mgombea nafasi ya Udiwani kutoka wadi ya Muembe Makumbi kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Siyasahau Mussa Haji amesema tunatakiwa kuwa karibu na wananchi wa maeneo yetu ambayo tumegombea ili tutambulike hata kama itatokea ulihama katika eneo hilo.
"Mimi mwanzoni wadi ilinikataa na kusema sikai katika eneo hilo kutokana na kuolewa sehemu nyengine ila nilionesha vielelezo vyangu vya kuishi hapo na sasa nimekubaliwa na nimehamia kabisa"ameeleza Siyahau
Ameongoza kuwa wanawake wasikubali kubebwa kwenye siasa kwani ni chanzo kinachochea udhalilishaji bali Tunatakiwa kupambana kutafuta njia za kufanya kampeni kwa nguvu zetu wenyewe.
"Siasa si sehemu ya kuoneana huruma hatuwezi kusimama kama tutakuwa tunasubiri misaada"ameeleza
Amina Bakari Mohd kutoka Chama Cha Sauti ya Umma (SAU) amesema wanawake hawatakiwi kuiga kuingia katika uongozi kwani wakifanya hivyo kunapelekea wao kuishia njiani na kukatika ndoto zao.
"Lazima tujitoe kwa moyo kuingia katika siasa na sio kufata mkumbo wa ndugu jamaa na marafiki"
Aidha amesema hatutakiwi kusimama katika uchama wakati tunapoomba kura kwani baada ya kupata uongozi hatuwi kiongozi wa chama bali ni wa wote.
"Chama kisitumike kama chombo cha ubaguzi, bali kiwe ni utambulisho wa kisiasa".
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia Mkataba wa Maputo mwaka 2007.
Huu ni mkataba wa Umoja wa Afrika (AU) unaolenga kulinda na kukuza haki za wanawake barani Afrika
Kifungu cha 9 cha Mkataba huu kinasema:
“Wanawake na wanaume watakuwa na haki sawa ya kushiriki katika mchakato wa kisiasa; wanawake watakuwa na haki ya kushiriki na kushika nafasi za uongozi katika ngazi zote.”
Mashavu Bakari mgombea wa ubunge kwa tiketi ya Chama Cha ACT WAZALENDO amesema wanawake kushika nafasi za uongozi ni haki kisheria na kikatiba hivyo ipa haja kuwa tayari na kujitoa katika siasa kwa kusimamia vipaumbele vyetu kwani wana uwezo mkubwa wa kuongoza na kuleta maendeleo katika maeneo yao hasa wao ndio wanaozijuwa shida zilizopo ndani ya jamiii zilizo wazunguka.
"Sisi ndio tunaelewa changamoto nyingi na tuna nguvu zaidi ya kuyatatua matatizo bila ya kusaidiwa na wanaume"
Amesema mashirikiano ni kitu kizuri kwa kila mwanamke anagombea katika nafasi tofauti za uongozi kwa kuwa pamoja na wanaume kubadilishana mawazo ili kupata uzoefu zaidi wa kuongoza.
“Ninashirikiana na wanaume kupiga kampeni nyumba kwa nyumba. Sisi wanawake ndio wapambanaji wakubwa, tunahitaji kusimama wenyewe.”
Mgombea ubunge Jimbo la Amani Khamis Silima Ame amethibitisha kuwa wanawake wana uwezo mkubwa katika kuongoza kwani wao ndio wenye hamasa ya kuelimisha jamii na wana nguvu kubwa na mbinu za kushinda katika uongozi.
Aidha amesema licha ya kuwa mimi ni mwanaume na nimegombea lakini mwanawake wana maono makubwa ya kimaendeleo katika majimbo yao na ipo haja na jamii kuwapigia kura ili kuona utekelezaji wao mzuri wa kazi unatavyo leta maendeleo kwa nchi.
“Wanawake wana maono makubwa ya maendeleo na uwezo mkubwa wa kuhamasisha jamii na kuleta mabadiliko chanya. Tunapaswa kuwapa kura.”
Khadija Juma Abdul-rahma mkaazi wa chumbuni amesema muda umefika kuwaunga mkono wanawake wenzao kwani wao ndio watetezi wao katika masuala ya maendeleo.
"Tuwe na hamu na hamasa ya kuunga mkono wanawake wezetu kwani wao ni watetezi wetu"
Tume ya uchaguzi ya Zanzibar ZEC katika uchaguzi wa mwaka 2015 imebainisha kuwa wapiga kura wote 503196 wanawake 268651 na wanaumme 234,545 . Na uchaguzi mkuu wa2020 takuwimu zimeeleza kuwa wapiga kura wote walikuwa 566,352 na wanaume 272,121 na wanawake 294,231.
Kwa takuwimu hizi za uchaguzi wa miaka iliyopita inaonesha uwezekano mkubwa wa wanawake kuweza kukamata nafasi za kuongozi endapo tu watapata kuungwa mkono wanawake wenzao kwa kuwapigia kura.
Nae Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA-ZNZ Dkt. Mzuri Issa amesema huu sio mda tena wa kusubiri wanaume washinde na wanawake wawe wapongezaji.
“Wanawake si wapiga makofi kwenye mikutano ya kampeni, ni viongozi wa kweli wenye uwezo wa kubadilisha jamii. Tunachohitaji ni kuamini uwezo wetu, kushikana mikono na kupaza sauti zetu kwa maendeleo ya wanawake na Taifa.”
0 Comments