JESHI LA POLISI ZANZIBAR limezitoa
hofu Asasi za Kiraia zinazoendelea kusimamia
haki za Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu ZNZ ambapo limesema
litaendelea kuhakikishia Haki, Ulinzi na
Usalama kwa makundi hayo katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu Mwaka huu 2025
zinalindwa kikamilifu.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa
Jeshi la Polisi Zanzibar, Khamis Kombo Khamis alipokuwa akizungumza na
wawakilishi wa Asasi za Kiraia
zinazotetea haki za Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu
zilizofika katika Afisi kuu za Jeshi
hilo Ziwani Wilaya ya Mjini Unguja
katika kikao maalum cha kujadili mustakbali wa ulinzi na usalama wa makundi
hayo wakati wa Uchaguzi.
Aidha Kamishna Khamis ameziasa
asasi hizo kufikia pia wadau na taasisi nyengine muhimu nchini ili kwenda
sambamba na azma hiyo.
Alizitaja taasisi nyengine kuwa ni
pamoja na Vyama vya Siasa, Vikosi vyengine vya Ulinzi na Tume ya Uchaguzi.
Alieleza pia kuna haja ya kuwaelimisha wananchi jinsi ya kujiepusha na vitendo
vya uvunjaji wa sheria ili kujiweka katika hali ya usalama.
Kamishna amesisitiza pia kuwa Jeshi
la polisi lina utaratibu mzuri wa kuwawajibisha maafisa wake pindi wakienda
kinyume na utaratibu wa kazi.
Wakizungumza katika kikao wana Asasi
hao wameliomba Jeshi hilo kuendelea kuwa msimamizi namba moja wa amani wakati wa
uchaguzi sambamba na kuwalinda Wanawake
pamoja na Watu wenye Ulemavu ili waweze
kuwa salama na kushiriki kikamilifu
katika mchakato huo wa kidemokrasia kama
wapiga kura, wagombea na mawakala.
Walisema mwaka 2020 baadhi ya Wanawake, Vijana na Watu wenye
Ulemavu walipatwa na kadhia ya uvunjifu wa haki zao kutoka kwa Vikosi vya
Ulinzi na Usalama nchini kama wagombea na mawakala na hivyo kujenga hofu kuhusu
ushiriki wao kwa mwaka 2025.
Asasi hizo zimeahidi kuendelea
kutoa mashirikiano kwa Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo kwa
makundi hayo na kufatilia ushiriki wao
katika kipindi hicho cha Uchaguzi Mkuu.
Kikao hicho kilichofanyika Mei 2
huko katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi hilo zimewakutanisha Wawakilishi
kutoka Asasi za Kiraia Zanzibar zinazotetea, kulinda na kusimamia haki za Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu
zikiwemo Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO) Jumuiya ya
Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Jumuiya inayoshughulika na
Changamoto za Vijana Zanzibar (ZAFAYCO) na Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ).
0 Comments