Ticker

6/recent/ticker-posts

TAMWA ZNZ Kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Redio kwa Kutathmini Mchango wa Vyombo vya Habari


Na Mwanduahi Wetu:

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania – Zanzibar (TAMWA ZNZ) kitaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Redio kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa habari ili kujadili mchango wa Redio katika maendeleo ya jamii.

Hafla hiyo itafanyika Februari 12 huko katika ofisi za TAMWA ZNZ, Tunguu, ikiwakutanisha viongozi wa vyombo vya habari, wahariri, waandishi wa habari, na wadau wa sekta ya habari kutoka Unguja na Pemba.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Redio na Mabadiliko ya Tabianchi”, ikilenga kuangazia nafasi ya redio katika kuelimisha jamii juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi na mbinu za kukabiliana nazo.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na TAMWA ZNZ mwaka 2024, ni vipindi 11 pekee kati ya 2,600 vilivyohusu mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni sawa na asilimia 0.9%.

Kutokana na takwimu hizo, TAMWA ZNZ imezihimiza Redio na vyombo vyengine vya habari kutoa nafasi zaidi kwa mijadala inayohusu athari za mabadiliko ya tabianchi, hasa kwa kuangazia sauti za wanawake na nafasi yao katika kutafuta suluhisho.

Kwa mwaka 2024, kupitia ushirikiano wake na vyombo vya habari, TAMWA ZNZ ilifanikiwa kurusha habari 778 kwenye vyombo mbalimbali vya habari, zikiwemo habari 101 zilizorushwa kupitia Redio. Habari hizo zilihusu masuala kama vile udhalilishaji wa kijinsia, haki za wanawake na watoto, ushiriki wa wanawake katika uongozi, uhuru wa habari, na maendeleo ya kiuchumi kwa wanawake.

Kwa kuadhimisha Siku ya Redio Duniani, TAMWA ZNZ imevishukuru vyombo vya habari na wanahabari wote kwa mchango wao wa kuhakikisha jamii inapata habari sahihi kwa wakati.

Aidha Chama hicho kimezipongeza Redio zote kwa kazi yao muhimu ya kuhabarisha na kuhamasisha maendeleo, huku kikizitaka kuendelea kuipa kipaumbele mijadala inayohusu usawa wa kijinsia na masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Siku ya Kimataifa ya Redio huadhimishwa kila tarehe 13 Februari tangu ilipotangazwa rasmi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mwaka 2011, na baadaye kupitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2013.


Post a Comment

0 Comments