Ticker

6/recent/ticker-posts

Wanawake Wahimizwa Kutumia Vyombo Vya Habari Kutangaza Kazi Zao


Na Mwandishi Wetu:

Meneja miradi kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) Nairat Abdulla amewaomba wanawake kutumia vyombo vya habari kwa lengo la kutangaza kazi zao wanazozifanya.

Akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wakulima viongozi kutoka shehia nne (4) za Unguja, juu ya umuhimu wa kutumia vyombo vya habari, yaliofanyika ofisi za TAMWA-ZNZ Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, amesema wanawake wanajishughulisha na harakati mbalimbali zikiwemo za uzalishaji pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi lakini bado sauti zao hazisikiki ipasavyo kupitia vyombo vya habari.

Hivyo amewaomba wanawake hao kutumia vyombo vya habari hasa mitandao ya kijamii, kuelezea mafanikio na changamoto zinazowakabili katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi ili kufikisha ujumbe kwa wahusika na hatimae kupatiwa ufumbuzi.

Akiwasilisha mada inayohusu vyombo vya habari, Meneja Mawasiliano kutoka TAMWA ZNZ, Sofia Ngalapi amesema wanawake wakulima viongozi wanafanya kazi nzuri ya kutunza mazingira na kukabiliana na mbadiliko ya tabianchi, hivyo wapaze sauti kutangaza kazi wanazozifanya kupitia vyombo vya habari kwa lengo la kuhamasisha jamii kuwa vinara kupitia masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Khairat Haji, Afisa mawasiliano kutoka TAMWA ZNZ akiwasilisha mada inayohusu mitandao ya kijamii, amesema mitandao ya kijamii ni njia moja wapo ya kujitangaza endapo itatumika ipasavyo hasa katika dunia hii ya sayansi na teknolojia.

Aidha amesema ili kuepuka udhalilishaji kupitia mitandao ya kijamii, ni vyema kuepuka kuchapisha taarifa na picha zinazohusu maisha yao binafsi kwa kulinda usalama wao na badala yake kuitumia kama njia moja ya kujiongezea kipato.

Nao wakulima viongozi kutoka shehia nne (4) za Unguja, Mkoa wa Kusini, ambazo ni Bungi, Unguja Ukuu, Uzi na Ng’ambwa wamesema wamefarajika kupata mafunzo hayo kupitia program ya Zanzadapt na wameahidi kuwa mabalozi wazuri kwa kufikisha ujumbe kwa jamii.

Mradi unaohusu nafasi ya mwanamke kiongozi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, (Zanzadapt) umejikita kuangalia maeneo manne yakiwemo uhifadhi wa mikoko, kilimo mseto, wanawake viongozi na masuala ya jinsia ambao unatekelezwa kwa pamoja na TAMWA ZNZ, Jumuiya ya misitu Pemba (CFP), Jumuiya ya misitu Kimataifa (CFI) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Canada.


Post a Comment

0 Comments