Ticker

6/recent/ticker-posts

Marekebisho Sera Ya Utangazaji Iwe Chachu Ya Kuleta Usawa Wa Kijinsia katika Vyombo Vya Habari



Na Ahmed Abdulla, Zanzibar:

Katibu Mtendaji tume ya Utangazaji Zanzibar Suleiman Abdalla amesema wapo katika hatua ya kufanya marekebisho ya Sera ya Utangazaji ya mwaka 2008 ili kuondosha changamoto zilizopo katika vyombo vya habari  ili kuendana na mahitaji ya sasa.  

Akizungumza katika uzinduzi wa muongozo wa sera ya jinsia ya vyombo vya habari katika ofisi za tamwa zanzibar amesema sera hiyo ni ya zamani hivyo kufanyika kwa marekebisho itasaidia kutanua wigo kwa vyombo vya habari ili kuwepo kwa usawa wa kijinsia

Amesema kwa mujibu wa dunia ya sasa Sera ya Jinsia katika vyombo vya habari haiwezi kuepukika kutokana na utandawazi hivyo kupitia hatua hiyo itakuwa chachu ya kufanikisha kuanzishwa kwa kitengo hicho na  kuona kinafanyakazi katika kuwatetea wanawake na kufikia kwa asilimia 50% kwa 50%.

Amefahamisha kuwa Sera ya Jinsia katika vyombo hivvo  ni muhimu kwani itatoa fursa wanawake kupaza sauti zao katika harakati mbalimbali wanazozifanya sambamba na changamoto zinazowakabili.

Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wamiliki wa vyombo vya habari kutumia muongozo huo katika vyombo vyao ili kufikia malengo ya nchi na kidunia ya kufikiwa kwa usawa wa kijinsia.

Akizindua muongozo huo mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania TAMWA,ZNZ, Dk Mzuri Issa aliwaomba wadau wa Taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi pamoja na vyombo vya habari kuutumia muongozo huo ili kuleta usawa katika maeneo yao ya kazi.

“Muongozo huu umebainisha kila kitu,utawasaidia hata wanaume ambao hawapendi wake zao kufanya kazi kwa kuhofia kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji wakiwa kazini, imani yetu vitendo hivyo vitapungua katika maeneo ya kazi,”alisema.

Amesema kuwepo kwa muongozo huo utasaidia kuimarisha hali za wanawake na kuondosha udhalilishaji katika maeneo hayo.

Amesema Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Tanzania imesaini mikataba mbalimbali duniani ya kuleta usawa wa kijinsia ikiwemo mkataba wa mwaka 1979 wa kuondosha aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake (sedaw), itifaki ya Afrika na Maputo 2003 pamoja  na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika Sadec.

“Tafiti nyingi zinaonesha nafasi ya wanawake katika uongozi bado ipo chini kwani ni 30% tu, uwepo wa sera hii ya jinsia katika vyombo vya habari utasaidia kupaza sauti zao na kuinua haki za wanawake,wasichana na makundi yaliyopo pembezoni,”alisema.

Nae Mkaguzi wa Polisi Dawati la Jinsiakutoka  makao makuu ya Polisi Zanzibar, Mohamed Seif Fadhil, amevitaka vyombo vya habari kushuka katika jamii ili kulisaidia Jeshi la Polisi hasa katika  kuibua matukio ya udhalilishaji wa jinsia ili kuwasaidia wananchi ambao hawana uwelewa juu ya masuala hayo na kupata haki zao.

Wakichangia ripoti hiyo washiriki kutoka Taasisi mbalimbali walisema katika maeneo ya kazi kunachangamoto  mbalimbali za udhalilishaji na kuwakosesha fursa wanawake hivyo kuwepo kwa sera hiyo  itasaidia kuleta usawa wa kijinsia.

“Elimu ndio jambo la msingi, ni lazima elimu iwafikie walengwa wakiwemo wanafunzi na viongozi wa taasisi inayohusiana na mambo ya jinsia ili kupunguza wimbi la udhalilishaji katika sehemu za kazi,” alisema.

Uzinduzi wa muongozo wa Sera ya Jinsia ufamefanywa na TAMWA,ZNZ  ikiwa ni moja ya utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi unatekelezwa kwa pamoja baina ya  TAMWA,ZNZ , ZAFELA na PEGAO chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Norway.

 

 

Post a Comment

0 Comments