MKURUGENZI Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, TAMWA ZNZ
kwa niaba ya ZAFELA na PEGAO ametoa shukrani za dhati kwa wote waliochangia
kufanikisha hafla ya utoaji tuzo kwa waandishi wa habari iliyofanyika Jumamosi,
Machi 9, 2024, katika Ukumbi wa SHAA mjini Unguja.
Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari huko ofisi za
TAMWA ZNZ Tunguu, Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri Issa ametoa
pongezi kwa waandishi wote waliowasilisha kazi zao kwa ajili ya kushiriki tunzo
za umahiri wa waandishi wa habari za wanawake na uongozi.
Tuzo hizo zilitolewa katika vipengele vinne tofauti ikiwemo Radio
Jamii, Radio za kitaifa, magazeti pamoja na mitandao ya kijamii ambapo habari
zilizowasilishwa zilikua zikiangazia maeneo mbalimbali ya kupigania haki za
wanawake na mabadiliko.
Washindi wa tuzo hizo walizawadiwa zawadi ya vyeti, ngao pamoja na
fedha taslim ambapo mshindi wa jumla ni Amina Masoud aliyezawadiwa hundi yenye
thamani ya shilingi milioni moja na laki tatu za Kitanzania, ikionesha
kutambuliwa kwa mchango wake wa kipekee katika tasnia hiyo.
Akizungumza wakati wa mkutano huo Jaji Mkuu wa Tuzo hizo
Dkt. Abdalla Mohammed Juma alisema waandishi wa habari wanawake wameonesha
muamko mkubwa katika kuwasilisha kazi zao ambapo katika waandishi wote
walioleta kazi wanawake walikua ni 379.
Dkt. Abdalla aliongeza kuwa kazi hiyo ya kuwatafuta washindi
wameifanya kwa uadilifu mkubwa kuhakikisha washindi waliopatikana ni wale
waliowasilisha kazi zenye ubora.
“Kazi tuliyopewa tumeifanya kwa uadilifu mkubwa, na kama kuna mapungufu
ni sisi majaji tunayabeba mapungufu hayo kwa asilimia 100”, Dr. Abdalla
Mohammed alisema Jaji.
Bi Nasra Mohammed, mwandishi wa habari mkongwe ambae pia alikua ni
miongni mwa majaji amewahimiza waandishi kuandika kazi zao katika viwango vya
juu ili kuweza kuisaidia jamii katika masuala hayo ya takwimu.
"Sisi waandishi wa habari tufanye kazi kwa bora na zenye viwango
kila siku ili kuweza kuipasha jamii taarifa sahihi zilizoshiba na kuleta tija
katika jamii." Alisema Bi Nasra
Mwisho Dkt Mzuri alitoa wito kwa waandishi wa habari kuendelea kuandika
habari zinazohusiana na wanawake, ikiwa ni pamoja na changamoto zinazokwamisha
upatikanaji wa nafasi za uongozi.
Huu ni mwaka wa tatu mfululizo kufanyika kwa tuzo hizi, na kwa mwaka
huu kumekua na ongezeko kubwa la idadi ya kazi zilizowasilishwa ambapo jumla ya
kazi 529 kutoka vyombo vya habari mbalimbali Zanzibar ziliwasilishwa.
Tuzo hizi zinafanyika ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa kuongeza
ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi ambao unatekelezwa na TAMWA
ZNZ, ZAFELA na PEGAO kwa ushirikiano mkubwa na ubalozi wa Norway ambapo
Kaulimbiu ya Tuzo hizi ni "Kalamu Yangu, Mchango Wangu kwa Wanawake"
inayoakisi dhamira endelevu ya waandishi wa habari kuongeza sauti za wanawake
na kuchangia katika maendeleo yao.
0 Comments