Mkurugenzi TAMWA ZNZ Dkt. Mzuri Issa |
Mkurugenzi wa Chama cha
Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA ZNZ) Dkt. Mzuri Issa amesema kuwa ni muhimu
kuwa na sheria nzuri za habari ambazo zinapelekea kuwepo kwa uhuru wa habari na
uhuru wa kujieleza kwa jamii.
Amesema hayo wakati wa
mkutano wa kutoa mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya tume ya utangazaji ya
Zanzibar (No. 7, 1997), ambao uliwashirikisha kamati ya masuala ya habari
(ZAMECO), asasi za kiraia na tume ya kurekebisha ya sheria uliofanyika katika
ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mtakwimu mkuu wa serikali Mazizini Zanzibar.
Dkt. Mzuri
aliongeza kuwa ipo haja ya kufanyiwa marekesbiso sheria hiyo ili kutoa
fursa ya uhuru wa kujieleza ambao ndio chanzo kikuu cha maendeleo ya nchi.
“ Uhuru wa habari na haki
ya kupata habari pamoja na uhuru wa kujieleza ni mambo ya msingi katika
maendeleo ya nchi na inaleta hata furaha ya mtu binafsi”, amesisitiza Dkt.
Mzuri Issa, katika mkutano huo wa siku moja ulioangaliwa na ZAMECO kufuatia
hatua ya Tume ya Mabadiliko ya Sheria kuipitia sheria hiyo.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa tume ya kurekebisha sheria Zanzibar, Ndugu Khadija Shamte
amesema kuwa muda umefika sasa kuwa na sheria zinazokwenda na wakati na tume
iko tayari kushirikiana na wadau kwenye kupokea maoni ya kurekebisha sheria ili
kutoa fursa kwa vyombo vya habari kukua na kuwa na ushindani katika kusambaza
taarifa.
“Tunahitaji kushirikiana
kwa pamoja na mwisho kupata sheria bora na nzuri ambayo italeta mabadiliko
katika tasnia ya habari Zanzibar”, Khadija Shamte, M/kiti Tume ya Kurekebisha
Sheria.
Wakizungumza katika
mkutano wadau wa habari Zanzibar wamesisitiza tume kuifanyia kazi
mapendekezo yote yaliyotolewwa na hatimaye kupatikana kwa sheria yenye kukidhi
vigezo na inayoikwenda na wakati.
Mwenyekiti wa Klabu ya
Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Abdullah Mfaume amesema mapendekezo ya
sheria ya habari inarahisisha upatikanaji wa habari katika ukusanyaji,
usambazaji wa taarifa kwa waandishi wa habari na itakuwa tija na maslahi kwa
jamii.
Ameiomba Tume ya Mabadiliko
ya Sheria pamoja na watendaji wengine kuitumia ZAMECO katika kujadili sheria
zozote zinazohusiana na masuala ya uandishi wa habari ili kupata taarifa zaidi
kuhusiana na hali halisi na masuala mbali mbali yanayoathiri sekta hiyo.
0 Comments