Ticker

6/recent/ticker-posts

Ubakaji Na Mimba Za Mapema Bado Ni Tatizo Zanzibar

Anna AthanasPaul Naibu waziri wa maendeleo ya jamii,jinsia,wazee na watoto Zanzibar


Mbali na Jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar za kuongeza umakini katika upatikanaji wa haki za watoto wa kike lakini bado watoto hao wanaendelea kukabiliwa na changamoto za kubakwa na mimba za mapema.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma alisema hayo katika hotuba yake iliyosomwa  na Naibu waziri wa Wizara hiyo Mhe. Anna Athnas Paul katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike, yaliofanyika jana katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil, Kikwajuni, Unguja.

Alisema  Serikali imekuwa ikifanya jitihada kuongeza umakini katika upatikanaji wa haki za watoto wa kike lakini bado watoto wanaendelea kukabiliwa na changamoto zinazohusu usalama wao ikiwemo kubakwa na mimba za mapema.

Aliezea kwamba jumla ya matukio 1,081 ya Ukatili na Udhalilishaji yameripotiwa katika kipindi cha Januari hadi Agost 2023 kwamujibu wa takwimu za Mtakwim Mkuu wa Serikali. Alisema  kati ya Matukio hayo matukio  838 yanahusu  watoto wa kike.

“Vitendo hivyo hupunguza nguvu kazi ya jamii katika ukuzaji wa shughuli za maendeleo, kukatiza ndoto zao za maisha na kudumaza ukuaji wao na maendeleo kwa ujumla” Alisema waziri huyo.

Alisema katika kukabiliana na changamoto hiyo Serikali imeendelea kuboresha huduma za malezi ya watoto wakiwemo wasichana kwa kutoa mafunzo ya malezi mazuri kwa wazazi na walezi kwa nia ya  kuwezesha makuzi bora ya watoto katika Shehia, Wilaya na Taifa.

Alifafanua kwamba  familia 530 na watendaji wapatao 60 wamejengewa uwezo wa elimu ya malezi ili waweze kuzifikia jamii kwa ujumla. Hivyo hatua hiyo imetoa mchango mkubwa katika kuhamasisha jamii kuachana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.

Naye Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Siti Abass Ali amewataka watoto wa kike kufanya bidii katika masomo yao ili waje kuwa viogozi katika nyanja mbali mbali.

Alisema Sheria ya mtoto namba  sita ya mwaka 2011 imekusanya haki za mtoto ikiwemo haki ya kupata matibabu, kupatiwa amani na ulinzi, kupata elimu hivyo mtoto wa kike anawajibu wa kusoma, hivyo amewataka watoto  hao kuwa na msimamo wa kutokujiingiza katika vitendo viovu  na  kujiamini kwamba wanaweza kuwa viongozi katika bunge, kampuni, jamii, nk.



Naye mtoto wa Kike jina limehifadhiwa ambaye ni mwanafunzi wa skuli ya msingi Kiswandui ameishauri Serikali kwamba mtu yeyote anayefanya kitendo kibaya kwa mtoto afungwe jela maisha kwasababu akitolewa ataanzisha makundi maovu katika jamii.


Post a Comment

0 Comments