Ticker

6/recent/ticker-posts

Wazee 25,000 Kupatiwa Vitambulisho Zanzibar

 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma   akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maoni, ushauri na mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Ustawi wa Jamii  ya Baraza la Wawakilishi,   katika kikao cha 8, mkutano wa 12 wa Baraza la Wawakilishi huko Chukwani Mjini Unguja, siku ya Septemba 22, 2023

Na Salma Lusangi WMJJWW

Waziri wa Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Zanzibar Mhe. Riziki Pemba Juma amesema wizara hiyo inatarajia kutoa vitambulisho 25,000 vya wazee wote wanaopokea pencheni jamii ili viweze kutumika katika huduma mbali mbali ikiwemo wakati wa kupokea pencheni jamii.

Kauli hiyo ameitowa mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maoni, ushauri/ Mapendekezo ya kamati ya kudumu ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar mwaka wa fedha 2022/2023, huko Chukwani, Unguja. Amesema Jumla ya vitambulishoa 25,000 vinatarajia kupatikana katika mwaka wa fedha 2023/2024 ambavyo watapewa wazee wote wanaopokea pencheni jamii.

Amesema Wizara ya Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumza za SMZ wanaendelea na utaratibu wa kuwatengenezea vitambulisho hivyo.

Hata hivyo Waziri huyo amesema jumla ya vitambulisho 3,668 tayari vimeshatolewa kati ya walengwa 28,776 hadi kufikia mwezi June mwaka huu.

Aidha amesema wizara yake imetowa mafunzo ya utowaji wa huduma za mpango wa Pencheni jamii kwa masheha wapya 31 wa Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja na masheha 30 wa wilaya Wete na Micheweni, Pemba ikiwa ni juhudi za kuwajengea uwezo katika utowaji wa huduma za pencheni jamii.

Amesema Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatumia njia mbali mbali kuelimisha jamii elimu inayohusiana na pencheni jamii kwa kutumia mitandao ya kijamii ikiwemo, facebook, twitter, Instagram na Youtube Pamoja na kushiriki katika matamasha ya maonesho mbali mbali.

Wakati huo huo amesema wizara yake imekamilisha uhakiki wenye lengo la kujiridhisha uwepo wa wazee hivyo,  jumla ya wazee 11,850 kwa upande wa Unguja, na wazee 4,388 ni wanufaika wa Mpango wa pencheni jamii.

‘ Uhakiki huo ulifanyika nyumba kwa nyumba kwa upande wa Unguja katika wilaya zote na Pemba kwa wilaya ya Mkoani, Wete na Micheweni,, hivyo tumejiridhisha uwepo wa wazee wanaonufaika na mpango wa pencheni jamii’ Alisema Waziri Pembe.

Sambamba na hayo Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar mwaka wa fedha 2022/2023, Mhe. Sabiha Filfil Thani amesema kamati hiyo inaipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kuweza kukamilisha zoezi la uhakiki wa wazee wanaonufaika na pencheni jamii , pamoja utengenezaji wa vitambulisho.

“ Mheshimiwa spika  katika kukuza hadhi na majukumu ya Idara ya Ustawi wa jamii na Jinsia kamati ilishauri wizara kuharakisha upatikanaji wa vitambulisho vya wazee waliyofikia umri. Kamati inaishukuru wizara kwa kupokea ushauri huo na kuufanyika kazi kuanza kuwapatia wazee vitambulisho hivyo” alisema Thani. 

Mwisho


Post a Comment

0 Comments