Ticker

6/recent/ticker-posts

Dkt. Mwinyi Awataka Wahandisi Wanawake Kuwa Chachu Ya Maendeleo Nchini

 


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ametoa wito kwa Wahandisi wanawake kushirikiana na kuhakikisha wanachangia vilivyo maendeleo ya nchi kufikia malengo ya kuwa na uchumi wa juu, wa kati ifikapo mwaka 2025.

Dk. Mwinyi alitoa wito huo kwenye ufunguzi wa Kongamano la nane la Wahandisi wanawake, ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema,Serikali za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar, zinatambua na kuthaminimchango wa Wahandisi wanawake nchini kutokana na kazi za uhandisi wanazozifanya.

Alisema,Makangamano kama hayo yamekuwa na mchango mkubwa wa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuendeleza ubunifu wa sanyansi na kuleta chachu ya maendeleo ya Taifa ikiwemo ujenzi wa viwanda.

Dk. Mwinyi aliongeza,Serikali zote mbili zinajitahidi kushirikisha wanawake kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kuwawekea mazingira wezeshi ya kujiajiri, kuhamasisha utambuzi wa fursa mbalimbali kupitia rasilimali zilizopo nchini, kurejesha stadi za ujuzi, elimu ya uanagenzi vyuoni na kutenga bajeti kwa ajili ya kufanikisha shughuli za utafiti na ubunifu wa fani tofauti.Alisema,fani ya uhandisi ina umuhimu mkubwa kwa ustawi wa nchi pia ni uti wa mgongo wa shughuli nyingi za kiuchumi. Hivyo aliwataka vijana na wanawake kuzitumia fursa ziliopo ili kuyafikia malengo yao.

Pia, aliwashauri wahandisi wanawake kufungua kampuni na kujiajiri kupitia ukandarasi na uhandisi nakueleza hatua hiyo itachangia sana maendeleo ya nchi kwa kujenga miundombinu imara itakayodumu kwa muda uliokusudiwa.

Aidha, alieleza kutokana na idadi ndogo ya wahandisi iliopo nchini, Serikali za SMZ na SMT zinaendelea kuweka mipango madhubuti ya kuongeza idadi ya wahandisi wanawake namafundi sanifupamoja na kuhakikisha wanasaidiwa vizuri wasichana wanaosoma masomo ya Sayansi katika elimu za Sekondari, vyuo vya mafunzo ya amali na vyuo vikuu, hatua ambayo bila shaka itasaidia kuongeza idadi ya wahandisi wanawake nchini.  

Hata hivyo, alihimiza ushirikiano baina ya wahandisi wanawake wa Zanzibar na Kitengo cha Taasisi ya Wahandisi Tanzania Barakwa madhumuni ya kuendeleza sekta ya uhandisi nchini Tanzania.

Akizungumza kwenye kongamano hilo kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Mhandisi Aisha Amour alisema Serikali inatambua mchango wa wahandisi katika kukuza uchumi wa taifa  uanzishwaji wa viwanda mbalimbali.

Naye, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Muhamed alieleza kongamano la nane la wahandisi wanawake linaloendelea visiwani Zanzibar litaongeza hamasa na uelewa kwa vijana na kuwashajihisha zaidi wanafunzi kuendelea kupenda masomo ya sayansi ili kujijengea kada zenye tija na utaalamu, kwani bado mahitaji ya wahandisi wanawake bara na Zanzibar yanahitajika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa taasisi ya wahandisi Tanzania, kitengo cha wanawake, Rihanna Juma aliisihi jamii kuachana na mitazamo potofu juu ya wahandisi wanawake kwa kuangalia mapungufu yao yanayotokana maumbile ya jinsia zao zikiwemo uzazi na uhalisia wao, hivyo aliwataka waajiri kuona umuhimu wao na kutambua mchango wao kwa maendeleo ya taifa kwa kuwatumia kwenye kazi za vitendo badala ya kuwapa kazi za ofisini pekee.

Uzinduzi wa Kongamano la nane la wanahandisi wanawake Tanzania kwa mwaka huu, 2023 ulikwenda sambamba kaulimbiu isemayo“Nguvu ya Ushirikishwaji na Uhusishwaji wa Wanawake katika kazi za Kihandisi”

 

Post a Comment

0 Comments