Ticker

6/recent/ticker-posts

ACT-Wazalendo Wataka Mamlaka Kamili Zanzibar

 


Na Nafda Hindi, Zanzibar

Makamo Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Othman Masoud Othaman amesema Zanzibar ili iweze kujisimamia kiuchumi inahitaji kupata mamlaka kamili kwa lengo la kuinua hali za wananchi wake kiuchumi.

Ameyasema hayo wakati wa kongamano la vijana wa chama hicho ililofanyika katika ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa ndege Zanzibar.

Othman amesema Zanzibar ina rasilimali za kutosha ambazo zinaweza kubadilisha maisha ya Wazanzibar kiuchumi endapo kutakuwa na mifumo mizuri katika usimamizi hali ambayo italeta maendeleo ya haraka kwa mtu moja mmoja na Taifa kwa ujumla.

“Wazanzibari wanahitaji kufanya kazi za heshima zinazolingana na kipato cha sasa kulingana mfumo wa maisha ya leo, hivyo suala la Zanzibar kuwa na mamlaka kamili si suala la hiari bali ni lazima”, alisema Othman.

Akizungumzia suala la utoaji wa haki kwa upande wa Mahakama amesema Mahakama ndio mama wa haki katika nchi hivyo ipo haja ya kubadilisha mfumo mzima wa upatikanaji wa haki wenye lengo la kuitumikia nchi na wananchi wake.

Mapema mshauri wa Vijana wa Chama hicho Mansour Yussuf Himid amewataka vijana kupambana kwa kukijenga chama pamoja na kusimamia na kudai haki zao kwa lengo la kuleta mabadiliko na maendeleo katika Taifa la Zanzibar.

“Lengo la Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 ni kumkombowa mzanzibar na njia sahihi nim kupata katiba mpya ambayo itaakisi ama kukidhi matumaini ya Wazanzibari,” Mansour alisema.

Nae Mjumbe Kamati Kuu Taifa ya chama hicho Ismail Jussa Ladu amesema muda umefika kwa Wazanzibar kupata Katiba mpya yenye mamlaka kamili ambayo itatowa fursa sawa kwa kila Mzanzibar bila ubaguzi wowote.

“Ajira ndio msingi wa maisha na ajira ndio kipato na bila ya kipato huwezi kupata maendeleo hivyo vijana lazima muhakikishe Zanzibar inarejea katika hadhi yake kama ilivyokuwa zamani kwa kuwa na mamlaka kamili,” Jussa alisema.Nao vijana wa Chama cha ACT Wazalendo wamesema tatizo kubwa wanalokumbana nalo ni ukosefu wa ajira jambo ambalo linawarejesha nyuma kimaendeleo na huchangia baadhi yao kujiunga katika makundi maovu.

Kongamano la vijana wa chama cha ACT Wazalendo limewashirikisha vijana wapatao 300 kutoka Mikoa mine ya Zanzibar lenye lengo la ufafanuzi wa ahadi ya chama hicho na Zanzibar yenye mamlaka kamili.

Post a Comment

0 Comments