Ticker

6/recent/ticker-posts

Wadau Waja Juu Mporomoko Wa Maadili Yapewa Maombi Kudhibiti

 


Na Nafda Hindi

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeombwa kudhibiti hali ya mporomoko wa maaadili inayoathiri Mila,Silka na Utamaduni wa Mzanzibar.

Hayo yamebainika wakati wa kongamano la kuporomoka kwa maadili lililoandaliwa na MadrasatAnnour Hayaat Saadat Addaarayn liliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Wilaya ya Mjini Unguja. Wakichangia katika kongamano hilo wananchi wamesema Serikali ina nafasi kubwa ya kuzuia mambo machafu yanayoendelea kufanyika katika kisiwa cha Zanzibar endapo sheria zilizowekwa zitatekelezwa kwa vitendo.

“Sisi wananchi tunakemea machafu yanayofanywa katika mitaa yetu kama vile madanguro,ulevi, uvaaji wa nguo zisizo za stara ila hatuoni hatua zinazochukuliwa ndio maana watoto wetu wanaharibika kwa kuona hadharani yanayofanywa,” waalisema wachangiaji hao.

Aliongezea kwa kusema wakati wa Uongozi wa Hayati Karume ambae alikuwa Rais wa awamu ya kwanza wa Zanzibar sheria ziliktekelezwa kwa vitendo na wananchi walikuwa si rahisi kuvunja sheria ovyo ovyo.

“Tulikuwa tunaona hata wageni wakiingia Zanzibar wakipewa nguo wajistiri ili kuendana na mazingira halisi ya wazawa na hata wachezaji wa mpira walikuwa hawaruhusiwi kuvaa suruwali fupi(bukta) hadharani na lilikuwa ni kosa kisheria wanabeba kwenye mkoba na kuvalia Uwanjani,” walisisitiza.

Mapema Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh Mgeni Hassan Juma amesema malezi ya pamoja yanahitajika pamoja na kufuata miongozo ya dini ili kuondokana na mambo machafu na kuwa na taifa bora.

Naibu huyo alisema licha ya serikali kulisimamia suala hilo kwa nguvu zote na kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali lakini bado kumekuwa na mporomoko mkubwa wa maadili hivyo ni vyema kurudi kwa Allah na kufuata miongozo yake ili kuwa na mustakabal mzuri wa jamii.

“ Hivi sasa jamii imekumbwa na mporomoko mkubwa wa maadili ikiwemo vitendo vya udhalilishaji na mapenzi ya jinsia moja, hivyo mashirikiano ya pamoja na kufuata miongozo ya dini itasaidia kujenga taifa bora,”alisema.

Nae Mkurugenzi Mtendaji kutoka Madrasat Annour Hayaat Saadat Addaarayn, Ukht Saada Mohamed, alisema lengo la kongamano hilo ni kuibua hisia za waislamu na jamii kwa ujumla wanaoguswa na mporomoko wa maadili kupaza sauti zao na kushirikiana kwa pamoja ili kukomesha matukio hayo.

Akiwasilishamada katika kongamano hilo mwakilishi kutoka UKWEM, Wanje Haji Gora amesema mporomoko wa maadili unachangiwa na mambo kadhaa yakiwemo wazazi kutokuwa na muda na watoto wao,muhali,ongezeko la talaka,utandawazi na kuiga mambo yanayokwenda kinyume na Utamaduni wa Mzanzibar.

Ofisa Kutoka Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA-ZNZ) Zaina Abdalla Mzee , alisisitiza jamii kusoma zaidi ili kupata uelewa juu ya njia sahihi ya kulea watoto katika maadili mema.

Alisema kwa mujibu wa utafiti mdogo uliofanya na taasisi hiyo hivi karibuni katika masuala ya udhalilishaji ulibaini kwamba watu wa karibu ikiwemo baba, mjomba na wengine wanaongoza kufanya vitendo hivyo kwa kiasi kikubwa.

Nae mwakilishi kutoka Chama cha wanasheria wanawake ZAFELA Hamisa Mmanga amesema Zanzibar inaongoza kwa kuwa na sheria nyingi na nzuri ila tatizo linakuja kwenye utekelezajin wa sheria hizo kivitendo.

“Sheria ya kumlinda mtoto Zanzibar (2011),sheria hii imepata tunzo ya kimataifa lakini ipo kinadhariatu,”alisema.

Kongamano hilo liliambatana na dua ya kuiombea nchi liliandaliwa na Madrasat Annour Hayaat Saadat Addaarayn iliopo Kikwajuni.

Post a Comment

0 Comments