Ticker

6/recent/ticker-posts

Nyumba 72 Za Makaazi Ya Watu Zaanza Kujengwa Zanzibar


Na Salma Lusangi Zanzibar 

 Mkurugenzi Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) Mwanaisha Ali Said amesema ZHC imeanza harakati za ujenzi wa nyumba 72 za makaazi katika eneo la Mombasa kwa Mchina Unguja  ili kuwaletea wananchi wa Zanzibar makaazi bora.

Akizungumza  katika mahojiano maalumu na muandishi wa habari hizi, Mkurugenzi huyo amesema  harakati za Ujenzi wa nyumba hizo zimeanza Mwezi Machi mwaka huu ambapo shirika hilo limefunga mkataba wa ujenzi na Mkandarasi Simba Developers Ltd. Hivyo Mkandarasi huyo ameanza kazi rasmi.

Mkurugenzi Mwanaisha amesema ujenzi huo utagharimu shilingi za Tanzania bilioni tisa nukta nane (9.8) hadi kumalizika kwake kati ya fedha hizo shilingi bilioni tatu (3) zitatoka katika mfuko wa ZHC na fedha zingine zimetoka katika mfuko wa Serikali kuu kwa maana ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Dkt, Hussein Ali Mwinyi.

Alifahamisha kwamba ZHC imekubaliana na Mkandarasi huyo katika kipindi cha muda wa miezi 15 kuanzia Machi 2023 nyumba hizo ziwe zimekamilika ili shirika liweze kuziuza nyumba hizo kwa wananchi mbali mbali ambao watahitaji kununua.

“ Lengo letu ni kuziuza nyumba hizo kwa mwenye kuhitaji, pesa za ujenzi Bilioni tatu tumetoa ZHC na fedha zingine tumepewa na Serikali kuu, nyumba zote zitakua 72 mtu pesa zake tu”. Alisema Mwanaisha.

Mkurugenzi Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) Mwanaisha Ali Said (kati) na Meneje Mkuu wa Kampuni ya Simba Developers Ltd Nurdin Hussein wakisaini  Mkataba wa ujezi wa Nyumba za Makaazi zinazojengwa eneo la Mombasa kwa Mchina Unguja

Aidha Mkurugenzi Mwanaisha amesema bei ya kuziuza nyumba hizo zitatofautiana kwa sababu kutakuwa na nyumba za vyumba vitatu na zingine vyumba viwili ila kiwango cha bei itapangwa na Serikali baada ya ujenzi kukamilika.

Naye Meneja Mkuu wa kampuni ya Simba Developers Ltd Nurdin Hussein ameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuiamini kampuni yake na kuipa dhamana ya kujenga nyumba hizo. Hivyo ameahidi kwamba kampuni yake itafanya kazi  kwa ufanisi na kwa wakati muwafaka kama walivyokubalina na ZHC.

Kwa Upande wa wananchi wa Zanzibar, akizungumza Bi Asha Ali Kombo (51) Mkaazi wa Fuoni Uwandani ameishukuru Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa uamuzi wa kujenga nyumba mpya  kwani ni wazi kwamba Nyumba za Maendeleo Zanzibar ni chache na kongwe hivyo hatua hiyo itasaidia kuondoa malalamiko kwa Shirika la Nyumba Zanzibar.

Naye Omar Ali Issa (48) Mkaazi wa Rahaleo ameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuweka mpango wa kuwauzia watu kwa kulipa fedha kidogo kidogo kwa wenye kipato cha chini. Alieleza kwamba kutokana na kipato tofauti baadhi ya watu hawataweza kutoa kiwango kikubwa cha fedha kwa pamoja ila kwa kulipa nusu nusu wataweza.

Mkurugenzi Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) Mwanaisha Ali Said (Kulia) na Meneje Mkuu wa Kampuni ya Simba Developers Ltd Nurdin Hussein Wakibadilishana  Mikataba ya ujezi wa Nyumba za Makaazi zinazojengwa eneo la Mombasa kwa Mchina Unguja


@Ikuluzanzibar
@WizaraArdhiZanzibar
@MillardAyo

Post a Comment

0 Comments