Na Ahmed Abdulla
Mwenyekiti wa kamati ya Jukwaa la Usawa wa Kijinsia (GEF) Tanzania Bibi
Angellah Kairuki amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuwekwa kwa mikakati imara ya
uwepo wa usawa wa kijinsia katika pande zote mbili za Jamuhuri ya Muungano
Tanzania kwa lengo la kurahisisisha kufikia usawa wa kizazi cha jinsia katika
uchumi pamoja na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Aliyasema hayo wakati alipokua akizungumza na Spika
wa Baraza la Wawakilishi (BLW) Mh. Zuber Ali Maulid kufuatia ziara maalumu ya
kujitambulisha iliyofanywa na kamati hiyo ndani ya ukumbi wa Baraza la
wawakilishi Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Alisema kamati hiyo ambayo imelenga kushughulikia
mambo 11 imejiwekea tayari mpango kazi wake wa miaka mitano ambao wadau
watapata fursa pia kuuchangia ili kuhakikisha kuwa inapata mpango mzuri na
wenye maono mapana.
Kamati hiyo yenye wajumbe 26 kutoka Bara na Zanzibar
imetokana na juhudi za kimataifa za kuelta usawa wa kijinsia ambapo imeundwa na
kuzinduliwa mwaka jana na Mh Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Samia
Suluhu Hassan ambaye ndiye kinara wa masuala ya usawa wa kiuchumi kwa Afrika.
Mwenyekiti Angela, akiyataja mambo hayo 11 alisema
ni pamoja na vituo vya kulea watoto ili mama waweze kufanyakazi vizuri na
kuhudumia watoto, upatikanaji wa maji safi, umeme, teknolojia rahisi, kukuza
ajira zenye stara, kuzalisha bidhaa zenye ushindani, uwekezaji katika elimu
hasa kwenye masomo ya sayasansi, hesabu na uhandisi, kuimarisha mifuko ya kina
mama, kuhamasisha mabadiliko ya mila potofu, kuimarisha mifuko ya fedha
jumuishi, ulinzi wa hifadhi ya jamii na utambuzi wa kazi zisizo kuwa na malipo
hasa majumbani (unpaid works).
Hivyo, Mwenyekiti amesema maeneo hayo yatahitaji
kuwa na takwimu za kuanzia katika kila sekta na pia kuwa na ripoti za maendeleo
yake kila mwaka ambapo wadau wa sekta zote kutoka kwenye Serikali na wasio na
Serikali wakiwemo na wajumbe wa BLW wanahitaji kushiriki kikamilifu.
Mmoja miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo Bibi
Abeida Rashid Abdalla ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Ustawi wa
Jamii,Wazee,Jinsia na Watoto,alimuomba Spika wa Baraza la wawakilishi
Zanzibar(BLW) kuwashauri wajumbe kuzingatia usawa wa kijinsia katika bajeti
pamoja na ripoti zinazowasilishwa Barazani hapo ili kufikia malengo hayo ya
usawa wa kijinsia.
Kwa upande wake Spika wa Baraza la wawakilishi
Zubeir Ali Maulid alisema ameipokea kamati hiyo na ameishauri kutenga muda
maalum wa kuonana na wajumbe ili kuwaeleza vizuri mikakati ya kufikia usawa huo
wa kizazi cha kijinsia.
Amesema pia Baraza liko tayari katika kushiriki
katika utekelezaji wa mpango huo wa miaka mitano kwa sasa ili kutoa mchango
wake unaostahiki na hivyo kuwa ni sehemu muhimu ya utekelezaji.
Kwa upande wa Zanzibar kamati hiyo inahusisha Naibu
Spika wa BLW Mh Mgeni Hassan Juma, Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Jinsia Bibi Abeida Rashid, Mkurugenzi Mtendaji Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Dk Mzuri
Issa, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wanawake , Najma Hussein na
aliyekuwa Mkurugenzi wa NMB, Zanzibar Bw Abdalla Duchi Hassan Khatib ambae ni Mkurugenzi wa mwevuli
wa Asasi za kiraia Zanzibar (ANGOZA).
0 Comments