Ticker

6/recent/ticker-posts

Naibu Katibu Mkuu Wizara Ya Habari Z’bar Aguswa Na Sheria Ya Habari

 


Na Ahmed Abdulla Othman

 

NAIBU Katibu mkuu Wizara ya habari Zanzibar Khamis Said amesema wakati umefika wa sheria ya habari Zanzibar kufanyiwa marekebisho kwa kuwa sheria inayotumiwa sasa imekua na changamoto mbalimbali ambazo ni kikwazo kiutendaji.

 

Aliyasema hayo katika mkutano maalumu uliowashirikisha wajumbe wa kamati ya ustawi wa jamii ya Baraza la wawakilishi na maafisa mbalimbali wa Serikali  ulioandaliwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na Internews Tanzania.

 

Alisema kwa miaka mingi Zanzibar imekua ikitumia sheria hio ya habari ambayo kwa mazingira yaliopo sasa haiendani na wakati na kwamba Serikali kupitia Raisi Mwinyi imeshafungua milango ya wadau kutoa maoni juu ya mabadiliko ya sheria hiyo.

 

Sambamba na hayo alisema wadau wana wajibu wa kujadili na kutoa maoni pale wanapoona kuna changamoto za kisheria ili Serikali iweze kuzifanyia kazi.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya ustawi wa jamii ya Baraza la wawakilishi Mohamed Ahmada alisema wao kama wajumbe wamepata wakati mzuri wa kufanyiwa mafunzo hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yamewajengea uwezo.

Alisema kwa kuwa Baraza la Wawakilishi linawajibu wa kujua sheria nyingi ili waone mapungufu ya sheria hizo hatimae waongeze nguvu katika kutetea mabadiliko ya sheria mpya.

Alisema kupitia mafunzo hayo waliopatiwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na Intenrnews yamefungua na kuwafanya wawe na uelewa mpana kuhusu sheria ya habari inayoendelea kutumika hadi sasa Zanzibar.

Alisema mara baada ya kupatiwa elimu hio watahakikisha mswaada wa sheria hio utakapopelekekwa Baraza la wawakilishi watajenga hoja imara ambazo zitasaidia kuwaeleza wajumbe wengine umuhimu wa sheria mpya ya habari.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ Dkt,Mzuri Issa alisema haki ya kupata habari ni haki ya kikatiba ambayo inapaswa kuheshimiwa na kila mmoja.

Alisema si sahihi kuona hadi leo hii licha ya kuwa kupatikana kwa habari ni haki ya kikatiba lakini ikawa inakinzana na sheria ambazo zimewekwa kupitia sheria ya habari.

Alisema sekta ya habari ni muhimu na chanzo cha maendeleo na kufungua fursa zaidi kimataifa hivyo inapaswa kuwa huru na kuheshimiwa.

Post a Comment

0 Comments