Serikali imesema haitofumbia macho Shirika lolote Lisilo la
Kiserikali litakalofanya kazi kinyume na Katiba zao na dhumuni la Shirika
husika.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis alipofanya ziara
katika Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma kukagua shughuli mbalimbali za Mashirika
Yasiyo ya Kiserikali Wilayani humo.
Naibu Waziri Mwanaidi amesisitiza kuwa lengo la Mashirika Yasiyo
ya Kiserikali ni kusaidia pale ambapo Serikali haijafika katika kutoa huduma
kwa jamii na sio vinginevyo.
"NGOs hizi zinasajiliwa kwa mujibu wa Sheria sasa niziombe
tu zifanye kazi kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizopo hatutofumbia macho
ukiukwaji wowote wa Sheria na taratibu" alisema Mhe. Mwanaidi
Aidha ameongeza kuwa zipo changamoto nyingi katika jamii ikiwepo
vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa mimba za utotoni ambazo zimekuwa
zikikatisha ndoto za watoto wa kike walio wengi katika meneno mbalimbali
nchini.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tunduru ambaye ni Mkuu
wa Wilaya ya Namtumbo Mhe. Dkt. Julius Kenneth Ningu amesema watahakikisha
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanayofanya kazi katika Wilaya ya Tunduru na
Mkoa kwa ujumla yanafanya kazi kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizopo.
"Tutahakikisha NGOs zinafuata Sheria na zinafanya kazi kwa
mujibu wa usajili wao na kuwanufaisha wananchi" alisema Dkt. Ningu
Ameongeza kuwa Wilaya itasimama vizuri katika kuhakikisha
inawachukulia hatua wanaosababisha kuwepo kwa mimba za utotoni
Akizungumza Mratibu wa Mradi wa Afya Mama na Mtoto Katibu wa
Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Masasi Phares Lihewe amesema mradi huo
umechangia katika kutoa elimu na vifaa vya kunawa mikono ikiwa ni hatua za
kujikinga na UVIKO 19 katika Shule mbalimbali za Sekondari Wilayni Tunduru.
Katika ziara yake Wilayani Tunduru Naibu Waziri Mwanaidi
amekabidhi vifaa vya kunawa mikono kwa baadhi ya Shule za Sekondari Wilayani
humo na kukagua shughuli za kiuchumi za wanawake wajasirimali.
#COVID19
#NGOs
0 Comments