Ticker

6/recent/ticker-posts

RC KUSINI AIBUA MADUDU SKULI YA MSINGI NA SEKONDARI JUMBI MARA BAADA YA KUMALIZA KIKAO NA WADAU WA ELIMU CHA KUTAFUTA MUARUBAINI WA KUMALIZA TATIZO LA MATOKEO MABOVU MKOANI HUMO.



Mkuu wa mkoa wa kusini unguja Mh, Rashid Hadid Rashid amewasisitiza wadau wa elimu mkoani humo kufikiria kwa makini na  kubuni mikakati madhubuti itakayosaidia kupunguza tatizo la kupata matokeo mabaya kwa wanafunzi wa kidato cha nne katika skuli mbalimbali za mkoa huo.

Akizungumza na wadau hao huko afisi ya mkoa huohuko Tunguu mkuu huyo wa mkoa amesema hakuridhishwa na hali ya matokeo ya wanafunzi kwa mwaka uliopita 2020 kwa kupata asilimia 52  na kuwa ni miongoni mwa mikoa iliofanya vibaya ambapo jumla ya wanafunzi 1187 kushindwa kuendelea na masomo kati ya 2502 waliofanya mitihani hiyo.

Amefahamisha kuwa Serikali imekuwa ikiendelea na jitihada zake za kuimarisha sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuongeza majengo ya kisasa na   maabara, hivyo ipo haja kwa wadau wa elimu kujipanga upya ili kuona kiwango cha ufaulu mwaka huu kinaongezeka.


Aidha mkuu huyo amewataka walimu wa skuli za mkoa  huo kujiendeleza kielimu ili waweze kutoa elimu iliyo bora sambamba na  kuwasisitiza walimu na wazazi  kuendeleza mashirikiano yaliopo  pamoja na kuzidisha mwamko katika kuwasimamia watoto wao kujikita katika elimu ili waweze kukabiliana vyema na mitihani yao ya Taifa mwaka huu.


Nao baadhi ya wadau hao wamesema kushuka kwa kiwango cha ufaulu ndani ya mkoa huo kunachangiwa na mambo mbali mbali ikiwemo mwamko mdogo wa wazazi kwa kuwafatilia maendeleo ya watoto wao, kukosa mbinu za ufundishaji, uhaba wa mfumo wa ajira na mitaala.


Mara baada ya kikao hicho mkuu wa mkoa huyo alifanya ziara ya kushtukiza katika skuli ya msingi na sekondari Jumbi ili kuona ni namna gani wanafunzi wanapata elimu katika mazingira gani ambapo aligundua uwepo wa walimu ambao hawajawahi kuingia madarasani kwa lengo la kuwafundisha wanafunzi tokea kufunguliwa kwa skuli pamoja na uwepo wa changamoto ya wanafunzi kupandisha mashetani wanapokuwa maeneo ya skuli.


Kufuatia uwepo wa kadhia hiyo amewataka walimu wakuu wa skuli hizo kuwasilisha ofisini kwake taarifa za kuna zenye sababu za kutokufundisha kwa walimu hao pamoja na sababu zinazopelekea wanafunzi hao kupandisha mashetani mara kwa mara wanapokuwa katika mazingira ya skuli.

 

Post a Comment

0 Comments