Ticker

6/recent/ticker-posts

"WANANCHI TOENI TAARIFA SERIKALINI MNAPOBAINI UZEMBE NA KUTOKUWAJIBIKA KWA WATUMISHI WA UMMA" DKT. MWINYI


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, DK. Hussein Ali Mwinyi amewataka Wananchi  kutoa taarifa serikalini endapo watabaini uzembe na kutowajibika kwa watumishi wa umma.

 

Alisema kuna baadhi ya watendaji wa umma hawawajibiki ipasavyo hasa katika maeneo ya vijijini na kusababisha kukwama kwa baadhi ya mipango ya maendeleo.

 

katika maelezo yake Dk.Mwinyi,amewakumbusha pia mabalozi wa mashina na viongozi wote ndani ya CCM kuwa na wao wanalojukumu la kutatua kusaidia utatuzi wa kero za Wananchi kwa kutoa taarifa na kuisimamia na kuelekeza Serikali katika masuala ya kiutendaji.

 

DK. Mwinyi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmashauri kuu ya CCM Taifa aliyasema hayo jana wakati akizungumza na mabalozi, viongozi na wanachama mbali mbali wa CCM, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kutoa shukrani kwa wanachama wa CCM katika mkoa wa Kaskazini Pemba.

 

"Nipeni taarifa ya watu wasiowajibika, kule vijijini kuna mambo ambayo hayafanyiki inavyotakiwa hivyo tupeni taarifa mapema, kila mmoja ambaye yupo serikali anatakiwa kuwajibika," alisema.

Alisema, Chama cha Mapinduzi kinatakiwa kuwa pamoja na serikali kuhakikisha shughuli za kiutendaji zinatekelezwa kwa wakati mwafaka ili Wananchi wanufaike na kasi ya utendaji wa Serikali ya awamu ya nane.

 

Alisema, kuna uzembe mwingi sana unafanyika mijini na hasa vijijini huko kuna miradi mingi haiendelezwi na watu fedha wanakula, hivyo aliwasisitiza Wana CCM  kutolifumbia macho vitendo hivyo. 

"Ipo miradi mingapi ya maji ambayo sasa hivi maji hayatoki?, zipo barabara ngapi zikishajengwa baada ya muda mfupi tu mashimo yanaanza? sasa mambo kama haya tusipoyachukulia hatua mapema ahadi zetu zote tutashindwa kutekeleza," alihoji

 

Alisema, anaeleza hayo fedha za serikali ni kwa ajili ya maendeleo ya watu na sio kwa ajili ya mtu fulani kuchukua fedha hizo na kujinufaisha yeye mwenyewe.

 

Katika hatua nyengine Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK. Hussein Ali Mwinyi alisema, anataka kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa ni eneo maalum la uwekezaji na kuwa na vivutio maalum.

 

alisema, anataka kuweka vivutio vya uwekezaji Pemba kuwa nafuu zaidi ili kuwavuta wawekezaji wengi waweze kuja Pemba, ili kisiwa hicho kiwe na wawekezaji wengi zaidi.

 

Alisema, lazima miundombinu ya Kisiwa cha Pemba iboreshwe, bandari ya Pemba iwe bora zaidi, uwanja wa ndege pia uboreshwe, pamoja na barabara, na kuwa na maeneo maalum ya uwekezaji wa viwanda.

 

"Nimeshazungumza na wawekezaji wengi na nikawaambia nataka nitoe vivutio maalum kwa Pemba na kwamba zile ajira tulizozisema laki tatu basi tunataka na Pemba zipatikane kwa vijana wote," alisema.

 

Alisema, muwekezaji akitaka kujenga Kiwanda Pemba basi atapunguziwa kodi zaidi ukilinganisha na akijenga kiwanda Unguja.

 

Katika hatua nyengine juzi majira ya saa 8:00 mchana huko Kusini Pemba katika ukumbi wa Fidel Castro, wakati akizungumza na makundi mbali mbali yakiwemo ya wafanyabiashara, wavuvi, wakulima, wafugaji, wajane, wanawake, watu wenye ulamavu na wajane Rais Mwinyi aliziainisha njia zitakazo yasaidia makundi mbali mbali yakiwemo ya wafanya biashara wa dogo wadogo kujikwamua kiuchumi na kuondokana na janga la umasikini.

 

Alisema, wakati wa kampeni alitoa ahadi kuwa akifanikiwa kuwa rais wa Zanzibar basi atafanya kazi na makundi yote hayo ili kuweza kuondoa changamoto zinazowakabili.

 

"Sasa uchaguzi umekwisha kilichobaki ni kufanya kazi, mimi nipo tayari kufanyakazi na nina amini wale wote nilowateua watafanya kazi na nawahakikishieni hilo," alisema.

 

Akianza na na kundi la wakulima Rais Mwinyi alisema, kipindi cha kampeni alisikia changamoto mbali mbali zinazowakabili wakulima hao wakiwemo wa karafuu, viungo, mwani na wengine na kuahidi kuzitatua changamoto hizo.

 

Alisema, amekuja kutoa maelekezo na kwamba makundi yote ya wakulima yaandae changamoto zao na kuyapeleka kwa mkuu wa mkoa na mawaziri husika ili kazi ya kuondoa changaoto hizo ifanyike.

 

"Natambua baadhi ya changamoto ilikuwa ni mitaji, na kwa bahati nzuri toka nilivyoingia madarakani nimeshakutana na mabenki mengi na wapo tayari kuwasaidia wajasiriamali na wakulima wadogo wadogo kwa kuwapa mikopo ya masharti nafuu pamoja na kuwapa elimu wafanya bishara hao," alisema.

 

Alisema, mabenki hayo yamekubaliana na masharti yote waliyowapa na kwamba wapo tayari kufanya kazi na serikali kuhakikisha kwamba wakulima na wafanya biashara wadogo wadogo wanatolewa walipo ili maisha yao yawe bora zaidi.

 

Akizungumzia kuhusu kundi la wavuvi, DK.Mwinyi alisema, ameshaanza kupata wawekezaji watakaowekeza kwenye uvuvi mkubwa wa bahari kuu lakini watajenga gati za uvuvi, watajenga viwanda vya kusarifu na kusindika samaki na watajenga viwanda vya kuzalisha nyavu.

 

Alisema, alikubaliana na wawekezaji hao kuwasaidia wavuvi wadogo kuwapa dhana za kisasa ili waweze kwenda kuvua mbali zaidi kuliko wanapoenda sasa hivi ili waweze kupata samaki wengi zaidi na wakubwa.

 

"Mimi naamini kwa mtindo huu tukiuanza basi tutaweza kundokana na uvuvi ule wa dhana duni na uvuvi uliokosa soko la uhakika na kuondokana na uvuvi ambao hauna tija kwa mvuvi," alisema.

 

Hivyo alisema yale ambayo alokuwa akiyasema kipindi cha Kampen mwanga wake unaonekana kwa sababu tayari wawekezaji wameanza kujitokeza kwa wingi.

 

Akizungumzia kuhusu vijana wa gereji alisema, walikubaliana kuwa shida yao ni dhana ili waweze kufanya kazi, hivyo aliwataka wake pamoja na wawaeleze mahitaji yao yote na kuwahakikishia kuyatekeleza.

 

Kuhusu kundi la wajane DK. Mwinyi alisema, aliwata kundi hilo kukaa pamoja na kuona ni njia gani nzuri ya kuwasaidia  na wao kupitia mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi na kupitia wafadhili mbali mbali basi watasimamia ili kuweza kupata biashara na kazi mbali mbali ili waondokane na umasikini.

 

Kundi la wanamichezo alisema, ameshakutana na wadau wa michezo na kukubaliana kudhamini michezo kwani michezo ili iendelee inahitaji fedha.

 

Akizungumzia kuhusu kundi la wajasiriamali wadogo wadogo alisema, walikuwa na changamoto ya maeneo mazuri ya kufanyia kazi, kuwaondolea utitiri wa kodi na kupata mitaji.

 

Alisema, amezungumza na watu na kwamba hayo yote yataweza kutimia na kusema, watajenga masoko ya kisasa, wataweka vituo vya mabasi vya kisasa na kuhakikisha kwamba wajasiria mali wadogo wanapata vitambulisho pamoja na kulipa kodi mara moja kwa mwaka, ili biashara zao ziwe zenye tija.

 

Aidha aliwaambia wafanyabiashara wa Pemba kuwa wakati sasa umefika wa kuiboresha bandari ya Pemba na kwamba hakuna sababu ya kushusha mizigo Mombasa, Dar es Salaam wala Unguja na badala yake ije moja kwa moja Pemba.

 

"Tunataka kupunguza gharama za kufanya biashara hapa Pemba kwa kushusha mizigo sehemu mbali, tuonde utitiri wa kodi nilipata kuzungumza na wafanyabiashara hapa walinambia kuna kodi za kila aina na tulikubaliana kuwa nitaziweka kodi chache," alisema.

 

Akizungumzia kuhusu kundi la boda boda alisema, wakati sasa umefika ataanza kuyatekeleza yale ambayo walubaliana kama vile kuwawekea mazingira mazuri ya kufanyia biashara zao, kuwapatia bima ya afya pamoja na kuwapatia mitaji.

 

Alisema, analisema hilo kwa sababu boda boda imeshaanza kuwa biashara kubwa kwani kila sehemu wapo wengi hivyo haiwezekani kuona kama ni kikundi kidogo cha watu, hivyo ni lazima wajenge umoja wao na kutafuta njia za kuwasaidia.

 

Makundi mengine kama Kundi la walemavu, vijana, na watoto na wanawake alisema, atahakikisha atawasaidia ili kuhakikisha wanajikwamua kimaendeleo na kuwapatia ajira.

 

"Tumejipanga kuleta viwanda vingi sana kwa ajili ya kupatia vijana wetu ajira na kuhakikisha makundi yote haya tunayasaidia ikiwemo walemavu kwa sababu na wao wana shida maalum," alisema

 


Post a Comment

0 Comments