Ticker

6/recent/ticker-posts

TANESCO YADAI 187 BILIONI KWA TAASISI ZA UMMA, WAZIRI AAGIZA KUKATWA UMEME KATIKA TAASISI HIZO


Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesisitiza wafanyakazi wa wizara hiyo kufanya Kazi kwa Ubunifu na Usahihi ili kuona kwamba wananchi wananufaika na Rasilimali za taifa lao.

Dkt. Kalemani ameyasema hayo  Desemba 12, 2020 katika kikao kazi cha kwanza kilichojumuisha Wakuu wa Bodi, Menejimenti, Idara, Vitengo na Taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kilichofanyika katika ofisi za wizara hiyo zilizopo Mji wa kiserikali Mtumba Dodoma kilichokuwa na lengo la kufahamiana na kutoa maagizo na maelekezo mbalimbali ya msingi ambayo yanapaswa kutekelezwa katika Serikali ya awamu hii.

 

“Nimewaita kwa mambo mawili tu, jambo la kwanza ni kufahamiana ndilo jambo lililonifanya niwaite wajumbe wa bodi zote za wakurugezi na menejimenti pamoja na uongozi wa wizara na kufahamishana mambo ya msingi ya kufanyia kazi na jambo la pili ni kuwaarifu kuwa tumeanza kufanya kazi na kikao hiki sio kikao tu bali ni kikao cha kwanza cha kazi” Alisema Kalemani

 

Dkt. Kalemani alielezea utekelezaji wa kauli mbiu itakayotumika kwa kipindi cha miaka mitano ambayo ni Kasi, Ubunifu na Usahihi na amezidi kuwataka watumishi wote wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa kasi kubwa huku wakizingatia ubunifu na kwa usahihi wa kazi huku akiwaasa watumishi hao kutimiza wajibu wao na akaendelea kutoa rai ya kupambana na mtu ambaye hatatimiza wajibu wake katika kazi.

 

“Nitangulie kusema tunakwenda na kauli mbiu ifatayo, ndio kaulimbiu yetu kwa miaka hii mitano ya kipindi cha pili cha awamu ya tano. Kauli mbiu yetu ni Kasi, Ubunifu na Usahihi, kila mmoja atakachoelezwa hapa akifanye kwa kasi kubwa, Ubunifu na Usahihi” Alieleza Waziri huyo

 

Dkt. Kalemani aliongezea kwa kuliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wahakikishe wanatekeleza majukumu yao yote kwa ufasaha huku akiwaagiza wakurugezi wote wa Shirika hilo nchi nzima kuendelea kushugulikia na kutatua kero mbalimbali kama kukatika kwa umeme mara kwa mara na kero nyingine pamoja na kuhakikisha miradi yote inayosimamiwa na Shirika hilo inatekelezwa kwa wakati.

 

Aidha, Dkt. Kalemani aliendelea kutoa maagizo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) la kukata umeme kwa wadaiwa wote nchi nzima bila kujali Taasisi binafsi wala Taasisi za umma huku akiwataka wakurungezi wote kuhakikisha wanakusanya mapato kutoka kwa wateja wao.

 

“Lazima TANESCO tukusanye mapato kutoka kwa wateja wetu maana jana nilipoingia ofisi nimepokea taarifa mpaka sasa tunadai zaidi ya Bilioni 182 kwa Taasisi za umma na wateja wa kawaida Bilioni 3.6, Mwenyekiti wa bodi nakuagiza kwa tunaemdai kata umeme, acha nilaumiwe mimi kwanza, kwahiyo kuanzia leo kama kuna mteja au Taasisi iwe ya Umma au ya binafsi tunayoidai naelekeza kwa bodi ya TANESCO katieni umeme kuanzia leo” Alisisitiza Waziri Kalemani

 

Nae Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato aliendelea kuwasisitiza watumishi wote wa Wizara hiyo kutimiza wajibu wao huku akiwasihi kutekeleza kikamilifu maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri na yatakayoendelea kutolewa na viongozi wa Wizara hiyo na Serikali nzima kwa ujumla.

 

Post a Comment

0 Comments