WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa
yote nchini wahakikishe kuwa watendaji wote wa Mikoa, Wilaya, Halmashauri
wasiende likizo ya sikukuu ya Krismas na mwaka mpya kwa mwaka huu, badala yake
wakasimamie ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na madawati na wawe
wamekamilisha ifikapo Februari 28, 2021.
“Suala hili nitalifuatilia mwenyewe ili kuhakikisha wanafunzi
wote waliochaguliwa chaguo la kwanza na la pili wawe wameingia madarasani
kufikia Machi Mosi mwaka 2021. Ukamilishaji wa vyumba hivyo pamoja na madawati
ufanyike kwa kutumia vyanzo vyenu vya ndani vya fedha.” Alisema Mhe, Majaaliwa
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Desemba 7, 2020)
alipozungumza na Wakuu wa Mikoa, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI. Kikao hicho ambacho Waziri Mkuu
alikiongoza kwa njia ya televisheni akiwa ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma
kilihusu upokeaji wa taarifa ya maandalizi ya kupokea wanafunzi wa kidato cha
kwanza, 2021.
Waziri Mkuu ameiagiza Ofisi ya Rais-TAMISEMI ihakikishe kazi
hiyo inakamilika kwa wakati na amewataka watendaji hao wahakikishe
ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa na utengenezaji wa madawati
unafanyika usiku na mchana.
Awali, Naibu Katibu Mkuu
Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Gerald Mweri alisema kati ya wanafunzi
wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021, wanafunzi 970
watapangwa kwenye shule maalumu, 1,059 shule za ufundi, 1,280 bweni kawaida,
803,326 watapangwa katika shule za sekondari za kutwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Bw. Juma Homera alisema katika mkoa
wake wanafunzi wote waliofaulu watapata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza
2021 kwa sababu awali walikuwa na upungufu wa vyumba 42 vya madarasa, ambapo
wamejenga shule mpya saba zenye vyumba 26 vya madarasa na wamekamilisha maboma
56 na hivyo kuwa na ziada ya vyumba 36 vya madarasa.
Kiongozi huyo alisema kuwa mkoa umeweka mkakati wa kuwapeleka
wanafunzi wote waliofeli katika vyuo vya maendeleo ya wananchi ili kuwawezesha
kupata stadi za maisha zitakazowawezesha kujitegemea.
“Mpango huu tunautekeleza kwa awamu ya pili sasa.”Alisema mkuu
wa mkoa huyo
Naye, Mkuu wa Mkoa wa
Lindi, Bw. Godfrey Zambi alisema mkoa wake ulikuwa na upungufu wa vyumba 400
vya madarasa, hadi sasa tayari wamekamilisha ujenzi wa vyumba 380 na kwamba
watahakikisha hadi Januari 30, 2021 watakuwa wamekamilisha ujenzi wa vyumba
vilivyosalia na wanafunzi wote watachaguliwa katika awamu ya kwanza.
0 Comments