Katika kijiji cha Uzi, Mkoa wa
Kusini Unguja, kuna familia ya watu sita baba, mama na watoto wane ambayo
imeamua kusimama tofauti na desturi za muda mrefu juu ya nafasi ya mwanamke
katika jamii.
Wakati sehemu kubwa ya jamii katika visiwa
vya Unguja na Pemba bado inaamini kuwa mwanamke ndiye mtu wa kukaa nyumbani,
familia hii imeamua kuvunja ukuta huo.
Nasra Hussein Abdalla, mkazi wa
kisiwa cha Uzi na mama wa watoto wanne, ameibuka kuwa mfano wa mwanamke jasiri
ambaye anaandika ukurasa mpya kupitia shughuli za kilimo msitu. Kupitia mradi
wa ZanzAdapt, Nasra ametambulika kama mhamasishaji wa jamii (TOT)
katika masuala ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Nasra anasema kilimo anachokifanya
leo hakifanani kabisa na kile alichokizoea miaka ya nyuma.
“Baadhi ya mazao yameshaanza kuzaa, hivyo tuna imani tutauza na kubadilisha
maisha yetu,” anasema kwa matumaini.
Anabainisha kuwa mafanikio haya si
ya ghafla, bali yametokana na mshikamano wa familia yake.
“Mume wangu amekuwa mstari wa mbele juu ya matumaini haya. Anachimba
mashimo, mimi napanda miche, na sasa tumefika hapa,” anaeleza.
Nasra anasema hata watoto wake
wawili kati ya wanne hushiriki kikamilifu kwenye shughuli hizo za kilimo msitu,
jambo lililofanya kazi kuwa nyepesi na ya furaha zaidi. Kuhusu suala la umiliki
wa ardhi, Nasra anasema bado hajafikia hapo, lakini anaamini mavuno yakianza
kuwa mazuri, ataweza kumiliki shamba lake mwenyewe.
Ame Khatib Ame, mume wa Nasra, naye
ana mtazamo chanya unaoendelea kuwa hamasa kwa wanaume wengi katika eneo hilo.
Akizungumza na Zanlight Blog, alisema: “Furaha yangu ni kuona malengo ya mke
wangu yanatimia. Hili si jambo lake peke yake ni maendeleo ya familia yetu.”
Ame anaamini kuwa mabadiliko ya
tabianchi hayatagusa wanawake pekee, bali familia nzima; hivyo kushiriki kwa
pamoja ni wajibu, si hiari. Anasema jamii itabadilika tu kama wanaume
watafahamu umuhimu wa kuwa bega kwa bega na wake zao.
Sinahila Abdulrahman Ali, mmoja wa
TOT, anasema nguvu ya mwanamke katika mapambano ya mabadiliko ya tabianchi
huongezeka maradufu anapoandamana na ushirikiano wa mumewe.
“Kazi tunazofanya kupanda miche,
kutengeneza vitalu, kuhifadhi mikoko zinahitaji nguvu na muda. Mume akikuunga
mkono, unafika mbali. Lakini akikuacha mwenyewe, unajikuta unachoka haraka,” anasema Sinahila.
Subira Ali Mwalimu, TOT mwingine,
anasema mabadiliko mapya yanaonekana wazi wanaume wameanza kufahamu kuwa
kushiriki ni uwekezaji wa familia.
“Wanaume sasa wanaanza kuona faida.
Tunapopata mazao, mapato yanaenda kwenye familia. Watoto wanapata chakula bora,
na ardhi yetu inakuwa imara zaidi. Kwa hiyo, wanaume wengi katika kijiji chetu
wameanza kuiga,” anasema Subira.
Anabainisha kuwa mabadiliko ya
tabianchi yanapunguza uzalishaji wa mazao, kuharibu mwambao wa bahari, na
kupunguza maeneo ya malisho, hivyo jambo hilo si suala la wanawake pekee.
“Sote tuna wajibu. Lakini wanawake
tukipewa nguvu kupitia sapoti ya waume zatu, matokeo yanakuwa makubwa zaidi,” anasisitiza.
Mkurugenzi mkuu wa community Forest Pemba (CFP) Mbarouk
Mussa Omar anasema wakati dunia ikihitaji wanawake wasio wategemezi hakuna budi
wanaume kuwaunga mkono wanawake wenye ndoto za kuleta mabadiliko katika jamii
zao.
“Tukiwa tuko katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya
tabia nchi wanaume tunatakiwa tuwaunge mkono wanawake wenye maono ya kuiweka jasmii
iliyo salama” anasemamkurugenzi huyo
Aidha aliongeza kuwa ili malengo mahsusi ya mradi wa
ZanzAdapt yaweze kufikiwa kuna kila haja kwa kila mwanajamii bila kujali jinsia
kuhakikisha anatumia kila nyenzo katika
kukabiliana na mabadiliko hayo na kuwakwamua wanawake na janga la utegemezi.
Mwenendo unaoonekana katika vijiji
kama Uzi unaonyesha mwelekeo mpya: wanaume wameanza kutambua umuhimu wa
kuwaunga mkono wake zao katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Kupitia shughuli za kilimo msitu,
utunzaji wa mikoko, uzalishaji wa miche, na ujasiriamali wa mazao ya misitu,
familia zinajiimarisha kiuchumi na kijamii.
Nasra, Sinahila, Subira na wanawake
wengine kama wao wanaonesha kuwa mabadiliko yakiungwa mkono nyumbani, jamii
nzima inanufaika.



0 Comments