Na Ahmed Abdulla, Zanzibar:
Lishe bora ni msingi wa afya njema kwa kila mtu, lakini inapokuja kwa mama mjamzito, lishe huwa nguzo imara ya maisha mapya.
Mama mjamzito anayepata lishe bora huwa na uwezo wa kubeba ujauzito kwa afya njema, kujifungua kwa usalama na kumlea mtoto mwenye nguvu na kinga thabiti ya mwili.
Aidha, lishe bora humsaidia mtoto kupata virutubisho vya msingi kama protini, madini ya chuma, kalsiamu na folic acid ambavyo ni muhimu kwa ukuaji wa mifupa, ubongo na kinga ya mwili.
Daktari wa masuala ya wanawake katika hospitali ya wilaya ya Ijtimai Magharibi ‘B’, Nicodemus Kikoti, alisema mama anapopata Mama anapopata chakula chenye madini ya chuma, protini, folic acid na vitamin kwa kiwango sahihi, hupunguza hatari ya upungufu wa damu na matatizo ya ukuaji wa mtoto, kwani lishe ni kinga ya kwanza ya maisha ya mama na mtoto aliyeko tumboni
“Ni muhimu kina mama wajawazito kuepuka vyakula visivyo na virutubisho na kuzingatia zaidi ushauri wa kitaalamu wanaopewa na madaktari” Alisema
Kwa upande mwingine, makala hii ilizungumza na Asma Mohd Hamad, mkaazi wa Mtofani Mwera ambaye pia ni mama mjamzito ambaye yeye alikiri kuwa mwanzoni hali yake haikuwa nzuri kutokana na upungufu wa damu uliosababishwa na kukosa hamu ya kula kwa wakati.
“Nilipoanza kula vyakula vya kujenga mwili kama samaki, maziwa na mbogamboga za majani, nilihisi nguvu mpya na kurudisha kiwango sahihi cha damu, hivyo niliweza kufuata ushauri wa daktari katika utumiaji wa vyakula sahihi vya lishe.” Alisema kwa msisitizo
Vilevile, muhudumu wa afya ngazi ya jamii (CHW) katika shehia ya Bububu, Fatma Ali Khamis, alieleza juhudi wanazozifanya kuhakikisha mama wajawazito wanapata huduma bora.
“Tunapita nyumba hadi nyumba kuwahimiza mama wajawazito kuhudhuria kliniki mapema, kuwashauri wale vyakula bora vikiwemo mbogamboga za majani na matunda ili kuhakikisha afya zao zinaimarika sambamba na kufuata maelekezo wanayopewa na daktari wanapokwenda hospitali.”
Fatma Ali Said, ni mratibu wa masuala ya lishe Zanzibar katika kitengo cha lishe chini ya Idara ya Kinga, Wizara ya Afya Zanzibar, alisema kuwa kipindi cha ujauzito ni cha kipekee na kinahitaji umakini zaidi katika upatikanaji wa lishe bora.
“Kipindi cha ujauzito ni cha kipekee kinachohitaji zaidi virutubisho vya kutosha vinavyosaidia ukuaji wa mtoto tumboni pamoja na kumlinda mama dhidi ya maradhi.” Alisema na kuongeza kuwa
“Ni jukumu la familia na jamii kwa ujumla kuhakikisha mama mjamzito hapati upungufu wa chakula bora hukua akipaswa kupewa muda wa kupumzika na kuhakikisha anapata mlo kamili mara tatu kwa siku pamoja na matunda.”
Kwa ujumla, mama mjamzito anapopata lishe bora, sio tu kwamba anaimarisha afya yake pekee, bali pia anahakikisha mtoto anayekuja duniani anapata mwanzo mzuri wa maisha.
Hivyo lishe sahihi ni ufunguo wa kuzuia matatizo ya afya, kuongeza kinga ya mwili na kuhakikisha ukuaji wa mtoto unakuwa wa kawaida.
0 Comments