Na Thuwaiba Habibu, Zanzibar
Tangu enzi za mababu zetu,wanawake wamekuwa na nafasi ya kipekee katika familia. Wamekuwa ni walimu wa kwanza kwa watoto, wasimamizi wa rasilimali za nyumbani, na mara nyingi, wasuluhishi wa migogoro ya kifamilia.
Uongozi huu wa ndani ya familia umekuwa wa asili, japokuwa haukuwa ukitambuliwa rasmi kama uongozi wa kisiasa au wa kiutawala.
Pia historia inaonyesha kuwa wanawake wamekumbana na vizingiti vingi katika harakati za kupambana kuingia katika uongozi ikiwemo ubaguzi wa kijinsia, ukosefu wa elimu na fursa sawa, tamaduni na mila kandamizi.
Katika miaka ya hivi karibuni, dunia imeanza kushuhudia mabadiliko makubwa ambapo wanawake wameanza kuingia na kushika nafasi za uongozi wa juu, wakiwemo marais, mawaziri, wabunge, na viongozi wa vyama.
Na hii inatokana na wadau mbali mbali wa masuala ya wanawake na uongozi kutafuta haki ya wanawake kushiriki katika uongozi.
Ikumbukwe kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi ilitia saini Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW) mwaka 1980 na kuuridhia rasmi mwaka 1985.
Huu ni mkataba wa Umoja wa Mataifa unaotambua haki ya wanawake kushiriki kikamilifu katika maisha ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Kifungu cha 7 cha CEDAW kinasema
"Nchi wanachama zitachukua hatua zote kuhakikisha wanawake wanapata haki sawa na wanaume kushiriki katika kutunga sera za serikali, kushika nyadhifa za kuchaguliwa, na kushiriki katika mashirika ya kiraia na ya serikali nchini."
Kutokana na tamko hilo limeweza kuwapatia wanawake fursa wa kuingia katika siasa kwa wingi ili kulifikia lengo la kuwa na usawa wa kijinsia.
Mariyamu Suleiman Bakari, Mgombea wa Ubunge kupitia chama cha United Democratic Union (UMD) anasibitisha hili kwa kusema wanawake wanatumia juhudi kubwa kuhakikisha wanapata nafasi ya kuingia katika uongozi.
“Tumekuwa tukipambana kwa nguvu ili kuhakikisha usawa wa kijinsia unapatikana"
Pia amesema kuwa taasisi za kiraia zimekuwa msaada mkubwa kwa wanawake na zinawapigania kukamata uongozi kwa kuwapatia mafunzo .
“Mafunzo yametufanya tujitambue, tujiamini na tuwe na ujasiri wa kuingia kwenye siasa kwa nguvu.”
Kwa upande wake Ghanima Sultan kutoka Chama Cha wananchi (CUF) amesema bado kuna mitazamo mibaya kwa jamii kuhusu wanawake lakini watahakikisha wote wanaamini uwezo wa wanawake.
“Katika jamii yetu bado kuna mitazamo hasi kuwa mwanamke hawezi kuongoza. Tutafanya mabadiliko ya kifikra ili wanawake waone uongozi ni haki yao" amesisitiza Ghanima.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2022 inaonesha kuwa Zanzbar ina jumla ya wakaazi 1,889,773 wanaumme 915,492 na wanawake 974,281.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa wa Chama cha Mapinduzi. (CCM)kutoka Tawi la Tomondo Ali Hamadi Juma amesema wanawake waendeleze kasi hiyo hiyo ya kuingia kwa wingi katika uongozi na wasiwe na hofu katika kampeni zao ili kuonesha utayari wao katika suala la uongozi na maendeleo ya nchi
"Wanawake wasiwe na hofu, waendelee kuingia kwa wingi katika uongozi."
Idadi ya ushiriki wa nafasi za uongozi wa wanawake kwa Zanzibar katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025. Zinaonesha kuwa bado idadi ya wanawake ni ndogo na ipo haja ya kuongozeka ili kuwe na ushiriki wa 50/50 katika uongozi.
Katika uchaguzi wa mwaka 2020, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lilikuwa na jumla wajumbe 76 (wawakilishi) Wanawake waliokuwa wawakilishi walikuwa 29,sawa na asilimia 38.2 ya wajumbe wote.
Wanawake 8 tu walishinda kwa kura za moja kwa moja kwenye majimbo yao sawa na asilimia 10.5
Na waliobaki (kati ya 29), yaani 21, waliteuliwa kupitia mfumo wa viti maalum. Hii ndiyo njia ambayo inasaidia kuongeza uwakilishi wa wanawake.
Kwa madiwani wanawake waliogombea nafasi za udiwani na walikuwa 135 kati ya wagombea 601 wote. Sawa asilimia 22.4 ya wagombea wote. Na Idadi ya wanawake walioshinda kwenye nafasi za udiwani ilikuwa ndogo sana chini ya 10, huku Zanzibar ina zaidi ya 300 shehia.
Wanawake waliopo kwenye nafasi ya Sheha ni 49 tu, sawa na asilimia 16.45 ya masheha wote.
Ikiwa na maana kila masheha 100, ni wanawake 16 tu wanaoshikilia nafasi hizo, na 84
Khadija Khamis Abdallah kutoka Chama Cha ACT WAZALENDO amesema wanawake wamejitokeza kuchukua fomu za uongozi kuhakikishia jamii kuwa wanaweza kuwa viongozi.
“Tumejitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali katika siasa ili kuvunja ile imani potofu kwa baadhi ya wanaume kwamba wanawake hatuwezi kuongoza."
Aidha, amesisitiza kuwa changamoto bado zipo, lakini wanawake hawapo tayari kurudi nyuma bali wameamua kupambana nazo.
“Tunapaswa kuondoa kabisa vizingiti vilivyobaki ili wanawake wafanye mageuzi ya kweli kwenye siasa"
Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA-ZNZ Dk Mzuri Issa amepongeza Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa uamuzi wa kupunguza ada wa wagombea wa nafasi za uongozi kwani umezingatia hali halisi ya kijamii na kiuchumi inayowakumba wanawake wengi Zanzibar.
“Tumeshuhudia ongezeko la wanawake wanaogombea nafasi za uongozi baada ya ZEC kupunguza ada ya kugombea. Hili ni jambo la kupongezwa kwa kuwa linaboresha ushiriki wa wanawake kisiasa.”
0 Comments