Na Ahmed Abdulla,Zanzibar
Katika mwambao wa bahari ya Uzi na Ng’ambwa ambako kilimo na uvuvi vimekuwa uti wa mgongo wa maisha ya wengi katika maeneo hayo ambapo wananchi wa jamii hiyo hujitafutia riziki na kipato kupitia shuhuli za uvuvi na kilimo.
Kupitia shuhuli hizo hususan katika sekta ya kilimo kumekuwa na mabadiliko makubwa ya mafanikio yaliyochochewa na mradi wa Zanziadapt ambao kwa upande wa kisiwa cha Unguja unatekelezwa katika shehia nne zikiwemo shehia ya Uzi na Ng’amba wilaya ya kati mkoa wa kusini Unguja.
Mradi huo umeleta nuru mpya kwa wakulima wa vijiji hivyo ambao awali walitegemea kilimo cha kawaida kisichoweza kupambana na athari za tabianchi na mageuzi ya kilimo.
Akizungumza na makala hii Asha Ramadhan Bakar mkaazi wa Uzi alisema miongoni mwa mafanikio aliyoyapata kupitia mradi huo ni kupata mafunzo na njia bora ya uzalishaji wa mazao katika kilimo kwani hapo awali alikuwa hana uwezo na utaalamu wa kulitayarisha shamba na namna gani ya kuweza kufanikiwa katika uzalishaji.
‘’Kabla ya kupata mafunzo ya ZanzAdapt nilikuwa nalima zao moja moja na mara nyingi mavuno yalikuwa hafifu,kupitia mafunzo ya kilimo mseto niliyopewa, sasa nalima mazao tofauti katika shamba moja na hata nikipata changamoto kwa zao moja mengine hunisaidia alieleza’’
Alisema maisha yangu na familia yangu yamebadilika kipato kimeongezeka na nina uhakika wa chakula hivyo ni vyema kwa wakulima kufuata utaratibu na miongozo ya mafunzo tuliyopewa kwa mafanikio ya uzalishaji wa mazao katika shamba.
Nae Subira Ali Mwalimu mkulima wa kilimo mseto shehia ya Uzi alisema miongoni mwa mafanikio aliyoyapata ni kupata elimu bora ya ukulima na kujifunza kupitia shamba darasa ikiwemo Kizimbani, Kidichi kikaongoni,Bungi na maeneo mengine tofauti jambo ambalo lilimfanya kuwa na hamasa zaidi katika kilimo kutokana namna uzalishaji wa mazao yake yalivyokuwa yanaimarika na kupata mazao kwa wingi kwa wakati mmoja.
Alisema kuwa kitu kikubwa ninachojivunia kupitia mradi wa ZanziAdapt ni kujengewa uwezo wa kupanda miche mbalimbali kwa ubora zaidi katika eneo moja hii imemfanya kuwa mwanamke wa harakati zaidi katika kilimo”.
‘’Nawashauri wanawake wenzangu tusivunjike moyo bali tuendelee kujituma na kuwa na bidii katika shuhuli za kilimo kwani kilimo ni njia moja wapo muhimu ya kujikwamua kiuchumi kwa familia na jamii kwa ujumla.’’
Pamoja na hayo makala hii ilizungumza na Lulu Ramadhan Hija mkulima wa Ng’ambwa alisema mradi wa ZanzAdapt umeleta mageuzi makubwa katika kilimo hususan katika kilimo cha minanasi kwani hapo awali kilimo hicho muamko wake ulikuwa mdogo sana kilimo cha minanasi hakikuwa na uzalishaji kwa wingi kutokana na ukosefu wa mbinu bora za kilimo na mabadiliko ya tabia nchini.
Alisema kupitia mafunzo ya kilimo mseto matumizi ya mbegu bora na mbinu rafiki kwa wakulima kumeweza kuongezeka kwa uzalishaji na kuboresha ubora wa mazao yao hali inayochangia ongezeko la uzalishaji wa mazao hayo.
‘’Zamani minanasini tulipanda lakini haikuzalisha vizuri lakini kupitia mradi wa ZanziAdapt tunaona mavuno makubwa ikiwemo migomba na muhogo ambayo imetupa uhakika wa chakula na kipato alieleza.’’
Issa Ramadhan Issa mkulima wa Nga’mbwa yeye alisema mradi huo umemfanya kupiga hatua zaidi katika kilimo kwa kubadili mbinu bora za uzalishaji wa mazao ambayo hapo awali uzalishaji wake ulikuwa wa kawaida tu.
Aidha alieleza kuwa kupitia mafunzo na uhamasishaji wa mradi ameendeleza juhudi za kushirikiana bega kwa bega na wanawake katika maandalizi ya shamba na njia bora za uzalishaji wa mazao.
‘’Mradi wa ZanziAdapt umenifundisha kwa kulima kilimo chenye mafanikio kinahitaji ushirikiano hivyo kufanya kazi na wanawake kumeongeza uzalishaji na kuleta mafanikio zaidi katika kilimo alieleza.’’
Kwa upande wake mtaalamu wa wataalamu wa kilimo Zanzibar Salum Rehan alisema taasisi binafsi zimekuwa mstari wa mbele katika kutoa mafunzo ya vitendo kwa wakulima kuhusu kilimo mseto matumizi ya mbinu bora kwa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha aliongezea kuwa uwepo wao mashambani umeongeza uelewa wa wakulima kuimarisha uzalisha na kusaidia kubadili kilimo cha kujikimu kuwa kilimo cha biashara hali inayochochea uchumi wa vijijini.
‘’Wizara ikishirikiana na tasisi binafsi katika harakati zozote zaujuzi unawafikia wakulima moja kwa moja na kupelekea kilimo kuwa ni chanzo cha kuwakomboa wananchi kiuchumi hususan katika maeneo ya vijijini alieleza.’’
Kwa upande wake Meneja utekelezaji wa mradi wa ZanzAdapt kwa upande wa Unguja Ali Said Juma alisema muamko mkubwa wa wanawake katika kilimo ni miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana hivyo pia mradi huo umeleta mabadiliko ya wazi katika maisha ya wakulima na ustahamilivu wa mifumo ya kilimo dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.
Alisema kupitia mafunzo ya kilimo kinachozingatia hali ya hewa usambazaji wa mbegu bora na uhamasishaji wa kilimo wa mseto wakulima wameweza kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali kama vile minanasi midimu migomba na mihogo na mengineyo huku baadhi ya maeneo yakianza kutoa mafanikio ya uzalishaji ambayo hapo awali uzalishajhi wake ulikuewa ni mdogo.
Aidha alisema kuwa nguvu ya mradi huo haupo tu katika uzalishaji bali pia kwenye mashirikiano na wadau na ushiriki wa jamii hivyo wanawake na vijana wamepewa kipaumbele kushiriki katika mradi huo.
Mradi wa Women in Climate adaptation - ZanzAdapt unaotekelezwa na Community Forest Pemba,Community Forest International
Na Chama Cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania kwa upande wa Zanzibar TAMWA –ZNZ)chini ya ufadhili wa Global Affairs Canada kwa kiasi kikubwa umewasaidia wanawake vijijini kujikomboa kiuchumi kupitia kilimo.
Kwa mujibu wa takwimu za mradi huo katika shehia ya Uzi na Nga’mbwa wameweza kuwafikia wanufaika ikiwa wanawake 434 na wanaume 197 katika shehia ya Uzi na Nga’mbwa wanawake 244 na wanaume 67.


0 Comments