Na Ahmed Abdulla:
Kwa zaidi ya miongo miwili sasa, Zanzibar imeendelea kukosa sheria mahsusi ya huduma za habari licha ya mahitaji makubwa yanayoongezeka kwa uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa taarifa.
Juhudi za awali zilizowahi kufanywa ndani ya Baraza la Wawakilishi kupitia viongozi wa kisiasa na wataalamu mbalimbali, bado hazijazaa matunda.
Profesa Omar Fakih Hamad, ambaye ni mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia jimbo la Pandani, anasema alifanya jitihada nyingi ikiwa ni pamoja na kuanzisha hoja za mswaada wa sheria ya habari, lakini ziligonga mwamba.
“Tulifanya jitihada kubwa barazani. Tulileta hoja tukazungumza umuhimu wa sheria ya huduma za habari, lakini serikali haikuwahi kuwasilisha muswada rasmi. Sheria ya sasa ni ya kikoloni na inalenga kudhibiti, si kuwezesha,” alisema Prof. Omar.
Alifafanua kuwa kwa sasa Zanzibar bado inategemea sheria ya Wakala wa Habari Magazeti na Vitabu ya mwaka (1988), akikitaja, Kifungu cha 30(1) cha sheria hiyo kinampa Waziri mwenye dhamana ya habari mamlaka ya kufungia gazeti lolote bila hata ya idhini ya mahakama, kwa madai ya kulinda usalama wa taifa au maadili.
“Wanahabari hawawezi kufanya kazi kwa uhuru wakiwa chini ya vitisho vya vifungu vya sheria hii. Tunahitaji sheria mpya ya kisasa, ya maridhiano, na inayolinda haki ya kupata taarifa,” aliongeza Prof. Omar.
Kwa upande wake Abdalla Mfaume, mjumbe wa Kamati ya Kitaalamu ya Masuala ya Sheria za Habari Zanzibar (ZAMECO), anakiri kuwa sheria hiyo inampa waziri mamlaka makubwa mno, jambo linalovuruga mizani kati ya maslahi ya taifa na uhuru wa habari.
“Ni kweli tunahitaji mabadiliko ya sheria hii ili kulinda uhuru wa vyombo vya habari, lakini pia hatuwezi kupuuza athari za maudhui yanayochochea chuki. Suluhisho ni kuwa na tume huru ya habari,” alisema Mfaume.
Kwa upande mwingine, Shadida Omar, kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), anasema sheria hiyo inakinzana moja kwa moja na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania – na Zanzibar – imeridhia.
“Sheria hii inatoa mianya ya kudhibiti vyombo vya habari visivyoegemea upande wa serikali. Tunapaza sauti kudai mabadiliko ya haraka ya sheria hii,” alisema Shadida.
Anaongeza kuwa ni haki ya kila mmoja kufanya kazi bila hofu, na ni wajibu wa serikali kuhakikisha mazingira hayo yanakuwepo kwa kuweka sheria mpya inayolinda haki za msingi.
Machano Othman Said ni Mjumbe wa baraza la wawakilishi Zanzibar anayewkilisha jimbo la Mfenesini anasema kuwa ni ukweli usiofichiksa kuwa sheria za habari zilizopo hajiendani na matakwa ya teknolojia iliyopo kwa sasa huku akiwasihi wanau wa sekta ya habari kuendelea na mchakato wa kudai sheria mpya ya habari kwa njia za amani.
“Sisi waheshimiwa wawakilishi hatuwezi kusema kuwa sheria hii ni nzuri, sheria ipo ila ina mapungufu mengi hivyo niwashauri endeleeni kudai sheria mpya kwa utaratibu wa utulivu na amani”
Kwa kauli zao, Prof. Omar na wadau hawa wanaonesha kwa pamoja kuwa kuna haja ya haraka ya kuandika upya sheria ya habari Zanzibar. Sheria hiyo inapaswa kuendana na Katiba ya Zanzibar, muktadha wa sasa wa kidijitali, na mikataba ya haki za binadamu ya kimataifa.
0 Comments