Katika mchakato wa uchaguzi ujao, takwimu kutoka vyama vikuu zinaonyesha uwakilishi mkubwa wa wanawake waliotia nia ya kugombea nafasi za uongozi, lakini changamoto ya kupata nafasi halisi bado ipo.
Kwa mujibu wa taarifa za hivi karibuni, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeorodhesha wanachama 2,089 kuchukua fomu za kugombea nafasi za Ubunge, Uwakilishi, Udiwani na viti maalum, kati yao wanawake ni 855.
Chama cha ACT Wazalendo kimeeleza kuwa kati ya wanachama 607 waliochukua fomu, wanawake ni 40 tu, wakigombea nafasi mbalimbali katika majimbo 50 ya uchaguzi.
Wadau wa masuala ya wanawake na uongozi wanatoa wito kwa vyama vya siasa kuhakikisha wanawake waliokidhi vigezo, wenye maadili na dhamira ya kuwahudumia wananchi wanateuliwa na kupata nafasi halisi za kushindana katika uchaguzi.
“Huu ni wakati muhimu wa kuonesha kwa vitendo dhamira ya kweli ya usawa wa kijinsia katika uongozi wa taifa letu,” imesema taarifa hiyo.
Wadau hao wanasisitiza kuwa wanawake wasiachwe nyuma baada ya kuchukua fomu, bali wajumbe wa vikao vya uteuzi wawapigie kura wakati wa mchakato wa kuwapata wagombea wa mwisho.
“Tunawashauri na kuwaomba wajumbe wa vikao vya uteuzi kuwapigia kura wanawake na kuwa sehemu ya mabadiliko kwa kutumia kura zao kama silaha ya kupigania usawa wa kijinsia,” wamesisitiza.
Aidha, mashirika yanayohusika na masuala ya wanawake yanatoa wito kwa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kufuatilia mchakato huu kwa karibu ili kuzuia rushwa na hila zinazoweza kuathiri usawa wa kijinsia.
Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW) unaipa Tanzania wajibu wa kuchukua hatua zote za kuondoa ukatili na kuunga mkono usawa wa kijinsia.
Mashirika kama Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO), na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) wanawahimiza wanawake wasikate tamaa bali waendelee kupigania nafasi za uongozi.
“Wanawake wote waliotia nia waliopita, waliopo kwenye mchakato na ambao hawajapita wasikatishwe tamaa na waendelee kushikilia uthubutu na misimamo yao,” imesema taarifa hiyo.
0 Comments