Ticker

6/recent/ticker-posts

Teen For Teens Yazindua Harambee Kukamilisha Ujenzi Wa Hospitali Ya Zop



Na Ahmed Abdulla, Zanzibar

Vijana wa mpango wa kijamii Teen for Teens wametangaza kuandaa harambee kubwa kwa lengo la kuchangia ujenzi wa Hospitali ya ZOP inayojengwa Mpendae, mjini Unguja. Harambee hiyo itafanyika katika viwanja vya Kariakoo na inatarajiwa kuvuta mamia ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Unguja.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za ZOP Academy, Kiembe Samaki Michungwani, wawakilishi wa vijana hao walisema msimu huu wa tatu wa Teen for Teens umebeba ujumbe wa mshikamano na mshirikiano wa kijamii kwa mustakabali wa afya ya wananchi.

Kwa mujibu wa vijana hao, siku ya harambee kutakuwa na viingilio vya aina mbalimbali vitakavyonogesha tukio hilo, sambamba na burudani na matukio maalum ya kijamii. Aidha, wajasiriamali wametaarifiwa kutumia nafasi hiyo kutangaza bidhaa na huduma zao kwa kukodi meza zitakazopatikana. “Tunataka hii harambee isiwe tu ya kuchangia, bali pia kuwa jukwaa la maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” walisisitiza.

Kwa upande wa uongozi wa taasisi ya ZOP, kupitia Dkt. Naofal na Ndugu Fahmi, imesisitizwa kuwa ujenzi wa hospitali hiyo ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za afya Zanzibar. Wameeleza kuwa mara itakapokamilika, hospitali hiyo itakuwa na kliniki maalum ya Saratani ya Matiti, huduma ambayo kwa sasa inapatikana kwa changamoto kubwa visiwani.

“Hospitali ya ZOP itarahisisha upatikanaji wa huduma muhimu za afya kwa wananchi, hususan wanawake na watoto. Ni hospitali ya kijamii, inayojengwa kwa nguvu za wananchi na wadau mbalimbali, na tunawaalika wote kushiriki katika harambee hii,” alisema Dkt. Naofal.

Hospitali ya ZOP inatajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kijamii inayotekelezwa na taasisi binafsi kwa kushirikiana na jamii, ikiwa ni kielelezo cha mshikamano wa wananchi katika kuwekeza kwenye afya na maisha bora. Harambee ya Teen for Teens inatarajiwa kuwa chachu ya kukamilika kwa awamu muhimu ya mradi huo.


Post a Comment

0 Comments