Ticker

6/recent/ticker-posts

Uhusiano Kati Ya Serikali Na Vyombo Vya Habari Katika Kutoa Taarifa

 


Na Thuwaiba Habibu, Zanzibar:

Mara tu baada ya kushika usukani wa kuiongozi Zanzibar karibu miaka mitano iliopita Rais Hussein Mwinyi alionyesha ushirikiano mkubwa na vyombo vya habari

Matamshi  na hatua yake ya kuonana  na waandishi  mara kwa mara katika miaka mitatu ya kwanza ya uongozi wake yalitoa sura ya kuimarika mashirikiano kati ya serikali na wadau wa habari.

Msingi wa kuaminiana ukawekewa zege na kilichosubiriwa ni ujenzi utaopelekea maelewano hayo kuwa mazuri zaidi siku hadi siku.

Wakati huo waandishi na wadau wa habari wakawa na matumaini makubwa ya kilio chao cha zaidi ya miaka 20 sasa cha kuwa na wigo mpana wa uhuru wa habari, haki ya kujieleza na mazingiza bora ya kazi kwa wana wa taaluma ya habari kimesikika.

Ndoto hii ilionekana karibu kutiumia Dk. Mwinyi alipoagiza mara kwa mara  kuchukuliwa hatua za kisheria na utendaji  kwa taasisi za serikali na mashirika ya umma kuwa karibu na vyombo vya habari ili umma upate taarifa  sahihi za shuhuli za serikali yao.

Katika msisitizo wake alisema  wataowakwepa waandishi au kukataa kutoa ufafanuzi juu ya masuala mbali mbali hawafai kuwemo katika serikali yake.

Lakini kwa bahati mbaya kauli zote zile zimeonekana kupotea hewani kama moshi huku waandishiwa habari wakiendelea kuambiwa wavumilie  na wakati wowote ule wataona mabadiliko.

Hivi sasa bado Zanzibar yapo malalmiko na masikitiko ya wanahabari kunyimwa taarifa juu ya masuala ambayo wananchi wanataka wapatiwe maelezo au ufafanuzi.

Mwanahabari wa kujitegemea,  Muhammed Khamis, anakumbusha haki ya  kikatiba na kisheria kwa waandishi wa  habari kupatiwa taarifa na hii imeainishwa wazi wazi katika Katiba yaZanzibar  ya mwaka ( 1984) katika Ibara ya 18(1) na (2) inayoeleza kwamba  Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta kupokea nakutoa habari na dhana kupitia chombo chochote, bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.

Vile vile imeelezwa kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbali mbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwajamii.

 Lakini unapokwenda kwa muhusika wa kukupa taarifa anakakataa kutoa taarifa, alieleza.

 Mara nyingi udhibiti uliopo katika sheria ziliopo Zanzibar hivi sasa umeweka mazingira ya wanaohusika na kutoa taarifa na wao kutoruhusiwa kuzungumzia masuala ya taasisi zao.

Hapa ndipo kwenye utata, kama mtu anaambiwa anao uhuru uliotamkwa ndani ya katiba wa kupata taarifa  sasa inakuwaje kuwepo sheria na kanuni zinazokiuka katiba za kuzuwia upatikanaji wa taarifa?

Mwandishi wa habari wa The Chanzo, Najjat Omar, ambaye amekuwa akikutana na kadhia hiyo anasema kikwazo cha waandishi kukosa taarifa ni utendaji usio mzuri wa baadhi ya maafisa wa serikali ambao hawataki kutekeleza wajibu wao wa kujibu changamoto za wananchi ambazo  wao ndio wahusika wa kuzishughulikia.

"Waandishi wanashindwa kufanya uwiano wa habari wanazoziandika kutokana na kukosa taarifa kwa baadhi ya watumishi wa serikalini. Hii inatokana na woga ama kwa kuweka vikwazo vya kupeleka maswali au barua,"aliongeza.

Suala la kupeleka maswali kwa maadishi kama vile mtu anajaza fomu ya maombi si la kawaida katika sekta ya habari katika nchi ambazo zinaendesha shughuli zake kwa misingi ya kidemokrasia

Jambo jengine ambalo mfumo huu unapelekea umma kukosa habari kwa wakati ni kwa sababu baadhi ya mambo huwa yanahitaji maelezo ya haraka kwa vile usumbufu wake unaathiri maisha ya kila siku ya wananchi.

Mifano halisi ni kama ya kuwepo eneo la makazi ya watu kujaa taka ambazo hazijakusanywa kwa muda mrefu na kuhatarisha maisha.

Lakini wakati huo huo maofisa wa Manispaa au Halmashauri wanasumbua wananchi kwa kukusanya malipo ya usafi wa mazingira, yaani fedha za usafi zinakusanywa lakini taka haziondolewi.

Hapo  mandishi anapokwenda kutaka maelezo anaambiwa apeleke kwa maandishi. Mbona makusanyo ya malipo ya usafi wa mazingira hayapelekewi maombi kwa wananchi kwa maandishi?

Kwa kweli mtindo huu wa kudai maandishi kwanza ni sawa na kumwambia mwenye njaa  andike barua ya maombi ya kueleza ana njaa na anataka chakula. Kwa mwenendo huu, si ajabu pakazuka masuala ya kumtaka mwenye njaa aseme aina gani ya chakula anaomba.

Huu sio mwendo mzuri na   pale panapokuwapo na sheria nzuri za habari na haki ya kujieleza ndio usumbufu wa aina hii  unaohatarisha maisha ya watu ndio utaondoka au angalau kupungua.

Serikali ya Zanzibar inapswa kutambua waandishi wa habari ni washirika muhiumu wa maendeleo na wanapodadisi lengo ni kuwahimiza watumishi wa umma kufanya kazi kwa uwadilifu na wanaofanya uzembe kuwajibika.

Najjat ameiomba serikali iwekeze nguvu kwa  maafisa wa habari waliopo katika wizara na idarakwa na mamlaka ya kuwasaidia waandishi ambao hawako katika sekta ya habari serikalini  kupata majibu ya maswali ya wabnayotaka wapatiwe ufafanuzi.

Hayo masuala huo ndio mwananchi wa kawaida huwa anauliza na kwa kuwa haiwezekani kila mtu kwenda wizarani kupeleka masuala ndio maana kazi hio hufanywa na waandishiwa habari kwa niaba ya umma.

Zulfa  Juma Silima mwandishi kutoka  Tiffu Tv amesema uhusiano  kati ya serikali na wanahabari  hauridhishi na unapaswa kuangaliwe ili pawepo mazingira mazuri ya kisheria ili mashirikiano yawe mazuri kwa maslahi ya nchi.

Mara nyingi Serikali hukimbilia kuviita vyombo vya habari  ikitaka kupeleka ujumbe wa aina moja au nyengine kwa jamii na hasa kufikisha taarifa muhimu.

Lakini wana habari wanapoona dosari maeneo fulani wamekuwa wazito au kukataa kabisa kutoa ushirikiano na mara nyengine hata kuweka vikwazo na visingizio huwa vingi. Hasa panapokuwepo masuala ya kisiasa, usalama wa raiya na mali zao au panapotakiwa maelezo juu ya matumizi ya fedha za umma.

"Kwa Zanzibarkupata baadhi ya taarifa inakuwa ni rahisi na kwa matukio mengine inakuwa shida aliongeza.

Mwanaharakati na Mtetezi  wa Masuala  ya Habari, Juma  Khamis Juma, anasema anavyoona ni muhimu kuwa uhusiano mzuri kati ya serikali na vyombo vya habari na pasiwepo vikwazo katika kutoa taarifa.

Alisisitiza kwamba uwazi ni nguzo umuhimu katika kuimarisha utawala bora na wa kidemokrasia.

Alisema pale ambapo hapana vikwazo inakuwa rahisi kwa waandishi wa habari kuisaidia Serikali yao na jamii kuibua vitendo vyenye harufu ya rushwa na ufisadi na umma kuwa na uelewa mzuri wa shughuli za serikali zinavyoendesha.

 

Uwazi pia unasaidia kupunguza uvumi usiokuwa na tija kwa nchi, aliongeza.

Amesema ni vizuri kuwa sheria mpya na rafiki za vyombo vya habari ambazo zitaiyafanya uhusiano kati ya serikali na wanahabari kuwa mzuri..

Hii itasaidia waandishi kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kwa umma na wakati huo Serikali kupokea maoni ya jamii ili mwisho wa siku yasaidie kuiletea Zanzibar maendeleo.

 Mwandishi na mwalimu wa aTasnia ya habari ndani na nje Zanzibar ambaye naye amekuwa mstari wa mbele kutaka mabadliko ya sheria za habari, Salim Said Salim, amesema wigo mpana wa uhuru habari ni nyenzo nzuri ya kujenga utawala bora na kuimarisha demokrasi katka nchi.

Amesema pale ambapo shughuli za serikali zinaendeshwa kwa uwazi, kama alivyoahidi Dk. Mwinyi aliposhika nafasi ya uongozi, imani ya wananchi kwa serikali yao huongezeka na hutoa mashirikiano mazuri.

Amesema sheria za hivi sasa sio rafiki hata kidogo kwani zinabana uhuru wa habari na kujieleza na hii haina maslahi mazuri kwa Zanzibar.

Aliitaka Serikali kutimiza ahadi yake na kuangana nchi kadha za Afrika zikiwemo jirani ambazo leo zinapigiwa mfano wa kuwa nasheria nzuri za habari.

Aliitaka Serikali kutokuwa na hofu na kupanua uhuuru wa vyombo vya habari kwani lengo la waandishi ni kutaka sheria zitazowawezesha kufanya kazi zao kwa uweledi na kutetea maslahi ya watu wa Zanzibar na sio kumkomoa mtu au kikundi cha watu.

Alisema Kenya, Rwanda, Namibi ,Ghana na hata Uganda na  Tanzania Bara zimefanya mabadiliko ya sheria ambayo anagalau kama sio mapana sana, lakini sio yale yanayowabana waandishii mbavu na koo.

Sasa  ni karibu miaka 20 tokea kilio cha kutaka sheria rafiki za habari na kila panapotolewa ahadi ya mchakato kuwa mbioni au kufikia tamati ndio kitabu hufungwa na kazi huanza upya ya alifu kwa kijiti.

Wiki chache ziliopita tulisikia kazi imemalizika zaidi ya asilimia 80 na wakati wowote marekebisho ya sheria yatafikishwa Baraza la Wawakilishi.

Ghafla upepo ulibadilika , kama ilivyo katika bahari inayovizunguka visiwa vya Ungua na Pemba, kwa kuambiwa pole pole ndio mwendo na kwahivyo waandishi na wadau wa habari wa subiri mwakani, mwaka ujao au mine au mitano itayofuata na sio kabla ya kufanyika uchaguzi wa mwezi Oktoba , mwaka huu.

Miaka 20 imepita na kila siku hali ni kama ile nyimbo ya taarabu isemayo  Kila siku waniamnbia kesho, keshokwa nini ukweli hutaki nambia.

Ni vizuri kwa ziliotolewa kila kukicha zikatelekezwa. Ahadi ni deni na Waarabu wansema “Laa takliful miaad, yaani usiende kinyume na ahadi yako”.

Utawala bora huimarika panapokuwepo uwazi, uhuru wa habari na haki ya kujieleza na papokosekana huwepo mashaka na kutoamini.

Ni miuhimu kwe sheria hii kupewa umuhimu kama zilivyo sheria zinazohusu taaluma nyengine

Post a Comment

0 Comments