Na Ahmed Abdulla, Zanzibar:
Kwa zaidi ya miongo miwili, wadau wa
habari visiwani Zanzibar wamekuwa wakidai kwa nguvu sheria mpya ya habari
itakayokuwa rafiki kwa vyombo vya habari na kulinda haki ya kupata taarifa.
Licha ya ahadi nyingi kutoka kwa
viongozi wa serikali, sheria hiyo bado haijafika mezani mwa Baraza la
Wawakilishi hali ambayo inaibua maswali kuhusu dhamira ya kweli ya kutaka
kulinda uhuru wa habari na kuchochea utawala bora.
Katika tukio muhimu la mwaka 2022
Pale Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi alipokutana na
Waandishi wa Habari, alikiri bayana kuwa sheria za habari za Zanzibar zimepitwa
na wakati na hazina ufanisi unaotakiwa katika mazingira ya sasa ya
kidemokrasia.
“Sheria
za habari za Zanzibar ni za muda mrefu, na Serikali anayoiongoza ipo tayari
kushirikiana na wadau wa habari kuzifanyia kazi kulingana na mapendekezo
yatakayotolewa,” alisema Rais Mwinyi, na kuongeza: “Pendekezo lenu la kwamba Zanzibar imefika
wakati wa kupata sheria nzuri, tutalifanyia kazi.”
Kauli hiyo iliongeza matumaini katika
mioyo ya wanahabari na watetezi wa haki za binadamu, lakini hatua za
utekelezaji zinaendelea kuwa za kusuasua.
Katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya
Habari duniani, Mei 3, 2023, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya
Golden Tulip, Uwanja wa Ndege Rais Mwinyi aliendeleza msimamo wake wa kuunga
mkono uhuru wa vyombo vya habari.
“Serikali
zote mbili zitaendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vyote vya habari
katika kuhakikisha changamoto zinazowakabili wanahabari zinatatuliwa,” aliahidi Rais huyo mbele ya wanahabari, wanaharakati na
viongozi wa serikali.
Ahadi hiyo ilirudiwa na Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia
Maulid Mwita, ambaye alitangaza kuwa mchakato wa maandalizi ya sheria
mpya ya habari ulikuwa umefikia asilimia 80.
“Serikali
yenu ni sikivu. Tunawahakikishia kuwa na sheria nzuri zitakazokidhi matakwa ya
sasa. Tutaiwasilisha Baraza la Wawakilishi na taratibu nyingine ziendelee,” alisema Waziri Tabia huku akiwasihi wadau kuwa na subira.
Aidha, Waziri huyo aliongeza
matumaini kwa kusema:
“Tuna
Baraza la Mapinduzi na tunategemea kwenda kuisoma sheria yetu mpya ya habari na
tutaipeleka Baraza la Wawakilishi ambako matarajio ni kutungwa na kuwa sheria
mpya,” alieleza Tabia Maulid Mwita, akiashiria
kuwa mchakato huo uko hatua za mwisho kabla ya kuwasilishwa rasmi.
Mwandishi Mkongwe wahabar ambaye pia ni Mwalimu wa Uandishi wa
Habari Tanzania na Afrika Mashariki, Salim Said Salim alisema demokrasia sahihi
hutegemea kwa kiasi kikubwa uhuru wa vyombo vya habari katika nchi, kwa sababu
vyombo vya habari vina dhima ya kuchangia maendeleo ya nchi kwa kupaza sauti na
kuwawajibisha viongozi wanaotumia mamlaka kinyume cha sheria.
“Hii Sheria ya Habari ina miaka takriban 20 sasa tokea kuanza
kuilalamikia, tunapewa ahadi kila siku lakini bado hatujaona utekelezaji wake.
Kama ni mtoto tayari angekuwa anasoma chuo kikuu,” anasema veterani aliyeanza
kuwa mwandishi wa habari mwaka 1965.
Kwa upande wa Muandishi nguli wa habari Viziwani
Zanzibar Salum Vuai alisema kwa msisitizo “Chombo cha habari kinaandika na
kutangaza ikiwa ni pamoja na kufichua baadhi ya maovu, jambo ambalo baadhi ya
viongozi hawapendi hivyo afisa wa polisi anaweza kutumia fursa hiyo kwenda
kukamata gazeti; hii haingii akilini katika ulimwengu huu wa utandawazi”
Amour Khamis ni Mhariri wa Zanzibar Cable TV alisema uwepo sharia
zisizorafiki katika uhuru wa habari kunapelekea waandishi washindwe kuandika habari zinazokosoa mamlaka au watu
waliopewa mamlaka jambo linaloweza kuondosha utawala bora nchini.
“Kwa mara nyingi hutumika neno ‘maslahi ya umma’ bila kufafanua ni yapi hayo maslahi ya umma, tunaweza kuingizwa hatiani kwa kutumia haya maneno yaliyopo kwenye vifungu vya sharia zetu za habari hivyo hapa dhana ya utawala bora inaweza kupotea” alisema Amour
Afisa Programu kutoka chama cha
waandishi wa habari wanawake Zanzibar Zaina Mzee alisema taifa haliwezi kupata
maendeleo ya haraka kukiwa hakuna sharia bora zinazowapa uhuru waandishi wa
habari.
“Maendeleo ya haraka haji hivihivi
pasi na kuwa na sharia bora ya habari inayotulinda sisi wanahabari.” Alisema
Mfano wa sharia hizo ni Sheria ya Tume ya Utangazaji No. 7 ya 1997
kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria No. 1, 2010 kifungu cha 27 (2).
alisema kuwa Kifungu hiki kimempa Waziri
mamlaka makubwa ya kuchukua maamuzi yoyote kwa chombo cha utangazaji ikiwa
kimetangaza jambo lolote kinyume na usalama wa taifa na maslahi yaumma.
0 Comments