Ticker

6/recent/ticker-posts

Mchakato Wa Kuundwa Sheria Mpya Unavyochelewesha Uhuru Wa Vyombo Vya Habari

 


Thuwaiba Habib, Zanzibar:

Muhitaji hachoki ni msemo wa Kiswahili uliotumiwa sana kipindi cha nyuma na watu walipokuwa wakisaka maendeleo ya nchi.

Na kwa kuwa watu wote walikuwa na nia ya dhati ya kulifanikisha hilo kwa kiwango kikubwa basi liliwezekana.

Vile vile msemo huo ulibainika  tena  mwaka 2023 baada ya wadau wa masuala ya habari kujikusanya na kuangalia mapungufu yaliyomo ndani ya sheria ya habari ambayo ina kandamiza uhuru wa habari na kujieleza   na kutaka  kuona mwafaka wa sheria hiyo hapa  Zanzibar.

Mwandishi wa habari kutoka Zenji Fm Berema Suleiman anasema kuchelewesha kwa mchakato wa kuundwa kwa sheria mpya na rafiki za habari visiwani Zanzibar kunasababisha hofu kwa waandishi na vyombo vya habari, kunadumaza demokrasia na utawala bora.

"Nchi ambayo haina sheria rafiki za vyombo vya habari inaweza kuchelewa kupata maendeleo kwa sababu changamoto zinazowakabili wananchi haziwezi kuibuliwa na kufika kwa haraka kwa mamlaka," anasema Berema.

Mwandishi wa habari  wa gazeti  la  Mwananchi Jesse Mikofu anasema Mchakato wa kuundwa kwa sheria mpya unachelewesha upatikanaji wa uhuru wa habari kwa sababu dana dana za kufanyiwa kazi jambo hilo zimekuwa nyingi kwani ni zaidi ya miaka 20 jambo hilo linazungumzwa na ufumbuzi haujapatikana.

"Suala hili linachelewesha uhuru wa habari kwasababu sheria rafiki haipo na sheria ndio inayoongoza kila kitu na kama huna sheria mzuri huwezi kufanya kitu kizuri kutokana na kuwapo sheria inayowabana waandishi ndiyo utendaji kazi wao unapopungua kasi"

Katibu Mkuu wa Zanzibar Press Club (ZPC) Mwinyimvua Abdi Nzukwi anasema kitu kikubwa ambacho pia kinahamasisha waandishi kutaka sheria mpya kwa haraka ni kupitiwa na wakati kwa sheria hii ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu ambayo imetungwa mwaka 1988 kufanyiwa marekebisho madogo 1997.

"Ni muhimu sheria ya habari rafiki ipatikane na iweze kuendana na mazingira ya sasa ambayo haitakuwa na vithibiti vingi vinavyokwaza uhuru wa habari na wa kujieleza"

Kutokana na ahadi mbali mbali kutoka serikalini moja ya kauli kutoka kwa kiongozi ilisema ya kuwa sheria habari   zipo kwa makatibu wakuu na zinafanyiwa kazi.

Waziri ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar Tabia Mwita aliwapa matumaini wanahabari kwenye mahojiano maalum hivi karibuni kwamba tayari vikao na wadau vimeshafanyika kuhusu sheria hizo na kwamba kwa sasa Serikali iko kwenye hatua ya mwisho ya mchakato wa maboresho ya sheria husika.

Serikali imepokea maoni ya wadau na muswada [wa marekebisho ya sheria] upo katika ngazi ya Makatibu Wakuu, Tabia alisema kwenye mahojiano hayo. Hivyo, kama Serikali tunajitahidi kuweka mazingira rafiki kwa waandishi ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi.

Mwanasheria na Mtetezi wa masuala ya Habari, Juma Khamis Juma anasema Mchakato wa sheria mpya ya habari ulianza zaidi ya miaka 20 iliyopita. Wadau mbalimbali kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania, walianzisha mchakato huu kwa pande zote mbili za Muungano, lakini wenzetu Tanzania Bara wakafanikiwa kupata sheria ya Huduma za Habari mwaka 2016.

" Ingawa ina kasoro za msingi lakini angalau kuna sheria mpya. Kwa upande wa Zanzibar juhudi mbalimbali zimechukuliwa na wadau, lakini hadi sasa bado sheria mpya haijapatikana.

“Upande wa Serikali unaeleza hatua inazochukua kuhakikisha sheria mpya inapatikana lakini wadau wanaona hatua bado ni za kusuasua, lakini naamini siku moja tunaweza kuwa na sheria bora ya habari itakayokata kiu ya kila mdau,” anasema Juma.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania, Zanzibar (TAMWA - ZNZ), Dkt. Mzuri Issa anasema mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari umekuwapo kwa miaka mingi lakini bado sheria hizo ambazo nyingi ni za muda mrefu zimekwama kurekebishwa.

Sisi wengine tangu tuko waandishi chipukizi tunazungumzia kupata hizi sheria mpya za habari, tangu 2008 kwa kweli ni muda mrefu, tunahitaji kusimamia jambo hili kwa umoja wetu na hatimaye tupate sheria mpya

Serikali visiwani hapa imebainisha kwamba inayasikia malalamiko ya wadau wa habari kuhusu uwepo wa sheria kandamizi za habari na zilizopitwa na wakati, ikisema kwamba iko mbioni kuzifanyia maboresho sheria hizo.

Afisa Programu wa TAMWA ZNZ, Zaina Mzee, amewataka wanahabari kuendelea na harakati za kutaka kuwapo kwa sheria mpya rafiki za habari. “Sheria hizi si tu zitahakikisha uhuru wa kujieleza bali pia zitaimarisha utoaji wa huduma za jamii na maendeleo kwa ujumla,” anasema Zaina.

Post a Comment

0 Comments