Na Nihifadhi Abdulla:
Wanawake wa Zanzibar wameendelea kupiga hatua muhimu katika sekta mbalimbali, lakini bado nafasi zao katika uongozi ni ndogo ikilinganishwa na wanaume. Changamoto hizi zimeibua wito kutoka kwa wadau mbalimbali, wakitoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa uchaguzi wa mwaka 2025 unaleta uwakilishi wa haki sawa kwa wanawake katika uongozi visiwani Zanzibar.
Salma Sadati, ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar JUWAUZA, amesema kuwa ni muhimu kubadili mitazamo katika kijamii kuhusu wanawake wanaojitoa kwa ajili ya kugombea nafasi za uongozi “Wanawake wengi wana uwezo wa kuwa viongozi bora, lakini hofu na vikwazo vya kijamii vinawazuia kujipambanua kwenye suala hilo. Salma ameongeza kuwa ni lazima tuanzishe kampeni za kijamii za kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa usawa wa kijinsia katika uongozi. ”Vyama vya siasa viwapa wanawake nafasi zaidi katika orodha za wagombea na kuhakikisha kuwa wanawake wanashiriki kikamilifu katika maamuzi ya vyama na kuwasaidia kuwanadi kwa wananchi” Amemaliza Salma juu ya maoni ya kuhusu mbinu za kuongeza wanawake viongozi kwenye uchaguzi wa mwaka 2025.
Sensa ya watu na maakazi yam waka 2022 inaonyesha kuwa Zanzibar ina jumla ya wakaazi 1.8,huku idadi ya wanawake ikiwa ni 974,281 wanawake wa mjini wakiwa ni 482,814 na wa kijini ni 491,467.
Idadi ya wanawake ni kubwa zaidi kuliko ya wanaume, jambo ambalo linaonyesha kuwa wanawake wana nguvu kubwa ya kuleta mabadiliko katika siasa. Licha ya idadi yao kuwa kubwa, ushiriki wa wanawake katika nafasi za juu za uongozi bado ni mdogo. Wadau wanashauri kuwa kampeni za kuhamasisha wanawake kugombea nafasi za kisiasa zizingatie kutumia takwimu hizi kama msingi wa kuonyesha umuhimu wa usawa wa kijinsia.
Dkt Mzuri Issa, Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA-Zanzibar, amesema kuwa vyama vya siasa vina jukumu kubwa katika kuhakikisha wanawake wanapewa fursa za uongozi. “Vyama vya siasa vinapaswa kubadili mtazamo ya kutumia wanawake kama wafuasi au mashabiki wa wagombea wa kiume”. Dkt Mzuri ameongeza kuwa vyama vinapaswa kuwapa wanawake nafasi za kugombea kwa usawa. “Kuna umuhimu wa kuwa na sera za vyama zinazoimarisha uwiano wa kijinsia na kuweka nafasi maalum kwa wanawake kwenye orodha za wagombea wa uchaguzi”.
Kwa mujibu wa mchambuzi wa siasa na utawala bora Almas Ali, wanawake wanahitaji maandalizi ya kimkakati ili kushinda nafasi za uongozi. “Vyama vya siasa vinaweza kuanzisha programu za mafunzo kwa wanawake ili kuwapa ujuzi wa kuendesha kampeni”.
Almas ameongeza kuwa ushindani wa kweli dhidi ya wagombea wa kiume ni mkubwa kwenye dhana ya kujieleza na hata ya kifedha hivyo wanawake wawezeshwe katika hilo.” Ikiwa lengo letu ni hilo basi vyama vya siasa viweke bajeti maalum ya kusaidia kampeni za wagombea wanawake ili kuhakikisha wanapata rasilimali fedha sawa na wanaume.”
Wananchi wanaona kuwa kuna ulazima wa mshikamano kati ya wanawake ,Fatma Seif ni mkaazi wa Tunguu hapa Zanzibar amesema kuwa wanawake wanapitia changamoto nyingi lakini wanapaswa kuwa na ujasiri wa kuzikabili. “Kuna haja ya kuwa na mshikamano kati ya wanawake ili kupeana msaada wa kimkakati wakati wa kampeni.”Amesema Fatma huku akiongeza kuwa wanawake wanaposhirikiana, wana nafasi kubwa zaidi ya kushinda.
Vilevile, Asha Bakari, ambaye pia ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi-CCM, amesema kuwa wanawake wanaposhika nafasi za uongozi, wanatoa kipaumbele kwa kijamii tofauti na wanaume.” Shida yam aji mfano ukiwa na kiongozi mwanamke anasaidia haraka maana anajua umuhimu wake tofauti na wanaume” .Amesema Asha ambaye anaona jamii, vyama vya siasa vitoe nafasi kwa wanawake kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2025
0 Comments