Ticker

6/recent/ticker-posts

Vishawishi, Dhana Potofu, Mifumo Kandamizi Vikwazo Vikuu Wanawake Kushika Uongozi Zanzibar

 


NA AHMED ABDULLA:

Ikiwa Wadau wa kupigania usawa wa kijinsia kwenye nafasi za uongozi wakiendelea na juhudi za kuhakikisha Zanzibar inapata usawa wa kijinsia kwenye nafasi za uongozi lakini bado wanawake wanakabiliwa na vikwazo mbalimbali vinavyokwamisha kufikia lengo hilo.

kwa mujibu wa Takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 inaonesha kuwa Zanzibar ina watu 1,889,773, ambapo wanawake ni 974,281 (asilimia 51.6) na wanaume 915,492 (asilimia 48.4).

Hata hivyo, idadi kubwa ya wanawake haiendani na nafasi walizonazo katika uongozi, hali inayodhihirisha changamoto kubwa katika utekelezaji wa usawa wa kijinsia.

Mfano wa haya ni katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020, takwimu za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) zilionesha kuwa wanawake walikuwa asilimia 51.9 ya wapiga kura waliojiandikisha.

Licha ya kuwa kundi kubwa la wapiga kura, nafasi za uongozi walizoambulia wanawake bado zilikuwa chache ukilinganisha na idadi yao.

Katika nafasi za uwakilishi majimboni, wanawake 8 pekee walichaguliwa kati ya jumla ya majimbo 50, huku wanaume wakichukua nafasi 42. Kwa ubunge, wanawake walikuwa 4 pekee kati ya wanaume 46. Hali hiyo ilijirudia kwa madiwani, ambapo wanawake walikuwa 25 tu kati ya wanaume 110.

Tatizo hili la kukosekana usawa wa kijinsia linatokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kwenye mamlaka za uteuzi ndani ya vyama vya siasa kutofuata matakwa ya wanachana wa eneo husika Jine Shaame, mwanachama wa CUF aliyewahi kuomba ridhaa ya kugombea jimbo la Chonga lililopo Kusini mwa Pemba, alibainisha kuwa wanawake wanakabiliwa na changamoto za upendeleo wa kijinsia ndani ya vyama vya siasa.

Alisema: “Niliondolewa kwenye orodha ya wagombea licha ya kuwa na uhakika wa kushinda, jambo ambalo lilipelekea wananchi wa jimbo langu kukasirika na kushindwa kumchagua mgombea wa chama.”

Suala la rushwa ya ngono nalo ni changamoto nyengine katika kufikia usawa wa kijinsia ambapo Asha Abdalla Mussa, Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda alisema wakati mwengine mwanamke anarudi nyuma kwenye kugombea nafasi mbalimbali kutokana na vishawishi vingi vikimuhitaji kutoa rushwa ya ngono ili apate nafasi hiyo. 

“Licha ya vishawishi vingi lakini nilisimamia msimamo wangu wa kupambana kwa uwezo ili kushika nafasi hii” Amesema Asha huku akitaja kikwazo kingine kuwa ni “Mfumo dume na kukatishwa tamaa kwa kuchafuliwa katika baadhi ya mazingira navyo nilikutana navyo lakini havikunirudisha nyuma bali nilisonga mbele na nikashinda na najivunia kuwa hapa kama kiongozi mwanamke“ Ameiomgezea Asha kwa sauti ya Uthubutu.

Dhana potofu za zinazonathibishwa na dini pia imekuwa kikwazo. Watu wengi wamekuwa wakidai kuwa dini zinakataza wanawake kuwa viongozi, jambo ambalo linapingwa vikali na viongozi wa dini.

Sheikh Khamis Abdulatif, kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja, alisema: “Hakuna sehemu katika dini inayokataza mwanamke kuwa kiongozi. Mtume Muhammad (S.A.W) aliwataka watu wachote elimu hata kutoka kwa Bibi Aisha, jambo linalodhihirisha imani kwa wanawake.”

Kwa upande wake, Askofu Michael Hafidh wa kanisa la Minara Miwili Zanzibar anasema: “Kuwanyima wanawake nafasi za uongozi kwa kisingizio cha dini ni kuwanyima haki zao za msingi. Hakuna dini inayokataza mwanamke kuwa kiongozi.”

Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Wilaya ya Kusini Mustafa Mohammed Haji ambaye pia ni Diwani wa Wadi ya Muyuni yeye alibainisha ubora wa wanawake kwenye vyombo vya maamuzi na kusema kuwa kwenye baraza analoliongoza madiwani wanawake kumekuwa na mchango mkubwa katika kuibua miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo Kiwanja cha Kufurahishia watoto cha Paje, Stendi ya Magari Michamvi pamoja na Masoko yaliyojengwa maeneo mbalimbali.

“Wanawake hawa wamekuwa mstari wa mbele katika katika kuchangia mikakati ya kuona tunapata fedha za kukidhi mahitaji ya miradi ambayo tumejipangia kwenye Bajeti ya mwaka husika” Alisema

Kwa kuzingatia changamoto zilizoelizwa, ni muhimu kuweka mikakati thabiti ya kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika nafasi za uongozi.

Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ, Dkt. Mzuri Issa, Alisema: “Tumeendelea kufanya kazi kubwa ya kuwajengea wanawake ujasiri na uwezo wa kushiriki kwenye siasa. Hata hivyo, jitihada zaidi zinahitajika kuhakikisha jamii inabadilika na kuwapa wanawake nafasi zinazostahili.”

Hafid Ali, mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar, aliongeza kwa kusema kuwa “Wanawake wanapaswa kujiingiza katika shughuli za ujasiriamali ili kujipatia kipato na kujitegemea kifedha. Hii itawawezesha kuendesha kampeni zao bila changamoto za kifedha.”

Serikali nayo ni sehemu ya kutafuta muarobaini wa changamoto hizo ambapo Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Anna Atanas Paul alisema atashangaa sana kusikia kama bado kuna familia zinamuona mwanamke ni mtu duni hasa visiwani Zanzibar.

“Kama zipo familia zinazofanya hivyo ziondokane na dhana hizo kwani taifa linataendelea kupiga hatua za maendeleo ikiwa jinsia zote zitashirikiana hivyo uwezo wa wanawake katika uongozi na kuleta Mabadiliko utaonekana dhahiri” Alisema Naibu Waziri Anna na kuzitaka jamii kutoa fursa sawa baina jinsi zote mbili kwani ni mwanamke ni muhimu kuwepo katika kila setka zote ili watoe mchango wao na kusaidia jamii.

Juhudi za kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi ni jukumu la kila mmoja.Wananchi, vyama vya siasa, mashirika ya kiraia, na Serikali wanapaswa kushirikiana kuhakikisha falsafa ya hamsini kwa hamsini inatimia.

Hilo linaweza kufanikishwa tu ikiwa jamii itaondokana na Dhana potofu, mifumo kandamizi, na ukosefu wa rasilimali zinazowazuia wanawake kufikia ndoto zao za uongozi.

Wanawake ni nguvu ya mabadiliko, na bila ushiriki wao, maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla yatabaki kuwa ndoto isiyotimia.

Post a Comment

0 Comments