Na Mwandishi Wetu:
Mratibu wa Mradi wa mfumo wa chakula, matumizi na urejeshaji wa ardhi, Miza Suleiman Khamis, amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea kuimarisha misitu katika maeneo yaliyoharibiwa, ili kuongeza uzalishaji na usalama wa chakula.
Akiwaslisha andiko la mradi wa mfumo wa chakula na matumizi ya ardhi kwa wadau mbali mbali katika Ukumbi wa Wizara ya kilimo Maruhubi, alisema mradi huo utashughulika na maeneo yaliyokatwa miti, kilimo kisichofaa na kuweka mifumo bora ya maji na ardhi.
Miongoni mwa wadau walioshiriki mkutano huo ni Maafisa Kilimo, Watendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar (ZARI), Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), Halmashauri za mkoa wa Kaskazini Unguja na Ofisi ya Makamu wa Kwanza katika kitengo cha Idara ya Mazingira.
Miza ambaye pia ni Afisa Mkuu katika Idara ya Misitu, amesema lengo la mradi huo ni kukuza usimamizi jumuishi wa rasilimali ardhi, maji, urejeshaji wa mnyororo wa thamani wa zao la mpunga ili kuzuia ukataji wa miti na uharibifu wa ardhi.
Aidha ameeleza kuwa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar inaendelea na hatua za awali za utekelezaji wa mradi huo ikiwemo kukamilika kwa kikao cha kwanza cha kamati ya uendeshaji ambacho kilipokea na kupitisha mapendekezo ya mpango wa utekelezaji ikiwemo bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Hivyo alieleza kukamilika kwa hatua hiyo kumetoa fursa ya kuanza kwa utekelezaji wa shughuli za mradi huo unaotarajiwa kusaidia maeneo yaliyoharibika yakiwemo ya hifadhi za misitu na maeneo ya kilimo cha mpunga.
Pia mradi huo utashughulikia makinga maji ambayo yatasaidia kuimarisha uzalishaji zaidi wa mpunga kutokana na athari zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Mapema mmoja ya waandaji wa mradi huo, Saleh Kombo Khiar, amesema mradi huo umebeba dhana mpya ambao utaweza kuangalia mandhari nzima ya eneo ambao utajumuisha katika sekta tofaut.
Alizitaja badhi ya sekta hizo kuwa ni kilimo, misitu, umwagiliaji maji, mifugo na maji hivyo wananchi watarajie mafanikio makubwa ya kuweza kuboresha maeneo yaliyoharibika na kua na mtazamo wa maendeleo katika mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kwa upande wake Afisa Uzalishaji kutoka Idara ya Umwagiliaji, Rukia Wahabi Mohamed, amesema mradi huo utakua na fursa nyingi kwa Wazanzibari kutokana na malengo yake ya kukuza matumizi bora ya ardhi na mnyororo wa thamani wa zao la mpunga ambapo wakulima wa mkoa huo wataweza kuzalisha tani zaid kwa hekta.
Mradi wa kuendeleza mifumo ya chakula, matumizi na urejeshaji wa ardhi unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii Tanzania na Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kupitia Idara ya Misitu.
Aidha mtradi huo utatekelezwa katika wilaya za Kaskazini ‘A’ na ‘B’ Unguja kwa upande wa Zanzibar unafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) na Global Trust Fund ambapo dola za Marekani 2,351,754 zitatumika kwa mda wa miaka mitano ya utekelezaji wake.
0 Comments