Ticker

6/recent/ticker-posts

TAMWA Zanzibar Yazindua Tuzo Ya Uandishi Kwa Ajili Ya Usawa Wa Kijinsia, "Media For Gender Equity Awards"

 


Na Ahmed Abdulla:

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), kikishirikiana na Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Jumuiya ya Wanasharia Wanawake Zanzibar (ZAFELA), na Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO), kimetangaza rasmi uzinduzi wa Tuzo ya “Media for Gender Equity Awards” yenye lengo la kutambua mchango wa vyombo vya habari katika kuendeleza usawa wa kijinsia.

 

Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa, alitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari katika hafla iliyofanyika Tunguu, akisisitiza kuwa tuzo hii itakuwa na ujumbe wenye nguvu, “Kalamu Yangu, Mchango Wangu kwa Wanawake.”

 

Hii ni hatua muhimu inayolenga kutambua na kuthamini juhudi za waandishi wa habari wanaoangazia maudhui ya wanawake katika uongozi, changamoto wanazopitia, na mchango wao katika jamii, na hivyo kujenga uandishi wenye kuchochea mabadiliko chanya kwa usawa wa kijinsia.

 

Kwa mujibu wa Dkt. Issa, lengo kuu la tuzo hiyo ni kuhamasisha vyombo vya habari na waandishi kuongeza nguvu katika kuwakilisha sauti za wanawake. Kupitia hatua hii, TAMWA inatarajia kuchochea ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi, kuimarisha nafasi zao, na kuzibainisha uwezo wao katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

 

Dkt. Issa alisisitiza kuwa vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kukuza mabadiliko ya kijamii kwa kuonesha mifano halisi ya wanawake wanaofanikiwa katika majukumu ya uongozi.

 

Tuzo hiyo, ambayo imepangwa kutolewa kwa mara ya nne, inalenga kuenzi vyombo vya habari vinavyoonesha juhudi za dhati katika kuendeleza usawa wa kijinsia kwa kuwa na sera thabiti za kijinsia, dawati maalum la kijinsia, na mifumo ya tathmini inayosaidia kufuatilia habari zinazohusu wanawake.

 

Miongoni mwa vigezo vya kushiriki ni kuwa na taarifa nyingi zinazoonesha ushawishi na nafasi ya wanawake katika uongozi pamoja na idadi ya wanawake waandishi katika vyombo vya habari husika.

 

Dkt. Issa alitangaza kuwa waandishi wa habari wenye kazi zinazowakilisha vigezo hivi wanaweza kuanza kuwasilisha kazi zao hadi Januari 5, 2025. “Kazi zote zinazostahili kuwasilishwa ni zile zilizochapishwa kati ya Januari na Desemba 2024, na zinaweza kuwasilishwa moja kwa moja katika ofisi za TAMWA zilizopo Tunguu na Mkanjuni, Pemba” alisisitiza Dkt. Mzuri.

 

Tuzo hizo zinadhaminiwa na Ubalozi wa Norway kupitia mradi wa Kuwajengea Wanawake Uwezo katika Uongozi (SWIL), mradi unaolenga kuwawezesha wanawake na kuimarisha uwakilishi wao katika uongozi.

 

Post a Comment

0 Comments