Ticker

6/recent/ticker-posts

TAMWA –ZNZ, Yawakutanisha Wanafunzi,Wadau Na Walimu Kwenye Mbio Za Kusheherekea Siku Ya Mtoto Wa Afrika

 


Na Najjat Omar Na Ahmed Abdulla:


Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Idara ya Michezo, Jumuiya ya Wanasharia Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Taasisi ya Maendeleo ya Ujerumani (GIZ) na Kituo cha Mijadala kwa Vijana (CYD), wanatarajia kuadhimisha siku ya kimataifa ya Mtoto wa Afrika tarehe 29 Juni 2024 kwa kuandaa mashindano ya riadha kwa wanafunzi wa skuli mbalimbali visiwani hapa.

Katika kusheherekea siku hio zaidi ya wanafunzi 70, watashiriki katika kukimbia mbio zitakazo anza Forodhani hadi Viwanja vya Mnazi Mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa TAMWA – Z, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Sophia Ngalapi amesema “Tukio hili muhimu linalenga kuhamasisha usawa wa kijinsia katika michezo na litawaleta pamoja wadau kutoka taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali ikiwemo wanafunzi kutoka skuli mbalimbali za Unguja, wanamichezo, walimu wa michezo, na wadau wote wa masuala ya usawa wa kijinsia.” Ameendelea kusema kuwa maadhimisho haya yanatoa fursa kwa wasichana kuonyesha vipaji vyao na uwezo wao wa kushiriki katika michezo mbalimbali pamoja na kujadili changamoto na vikwazo vinavyowazuia kushiriki katika michezo na kuhimiza uanzishwaji wa madawati ya jinsia katika taasisi za michezo.

“Tunaamini kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kuleta usawa wa kijinsia na kuwawezesha watoto wa kike na wa kiume kujifunza stadi za maisha, kujenga ujasiri, na kushirikiana kwa amani na kuheshimiana.Tunawaalika wanahabari, wazazi, walezi, na wananchi wote kujitokeza kwa wingi kushuhudia na kuunga mkono tukio hili la kihistoria katika kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha watoto wote kufikia ndoto zao katika Nyanja mbali mbali bila vikwazo vyovyote.” Amemaliza Sophia.

Wadau wa maadhimisho haya wamekubalina kuwa kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Wakati ni sasa! Wekeza katika elimu na michezo kwa watoto wote’.  

Akiongeza kuhusu maadhimisho hayo Afisa Mradi wa Masuala ya  Michezo kwa Maendeleo Khairat Haji amesema mara kadhaa TAMWA –Z wamekuwa wakiadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika kwa kuzungumza masuala ya udhalilishaji na kuwashirikisha wadau ila mara hii tutazungumza na watoto wa jinsia zote kushiriki kwenye michezo “Mwamko na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuweka nafasi sawa watoto wote kushiriki katika michezo, bila kujali jinsia zao. Mashindano hayo yatatoa washindi watatu zaidi wanawake na watatu wanaume na kutambuliswa rasmi.” Amemaliza Khairat.


Siku ya Mtoto wa Afrika ni siku inayosherehekewa kila mwaka 16 Juni tangu mwaka 1991 ilipotangazwa  na Umoja wa Afrika katika kuenzi michango ya watoto walioshiriki katika maandamano kwenye mji wa Soweto, Afrika Kusini mwaka 1976 pamoja na kuijengea jamii uelewa juu ya umuhimu wa elimu bora kwa watoto.

Kwa mwaka 2024 kaulimbiu nchini Tanzania ni ‘Elimu Jumuishi kwa Watoto Izingatie Maarifa, Maadili na Stadi za Kazi’. Ikumbukwe kwamba tarehe Juni 16,2024 Rais Samia alisherehekea siku hio na watoto Ikulu jijini Dar es Salaam na kusisitiza umuhimu wa serikali, familia na jamii kushirikiana kuhakikisha watoto wanapata malezi bora yenye maadili mema.

Post a Comment

0 Comments