Ticker

6/recent/ticker-posts

Suleiman Mbarouk Achaguliwa Kuwa Mwenyekiti Wa Chama Kikuu Cha Ushirika Zanzibar.

 

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika Zanzibar-CUZA wamemchagua Suleiman Ame Mbarouk kuwa mwenyekiti wa Chama hicho katika mkutano kuu uliofanyika Ukumbi wa Jumuiya ya watu wenye Ulemavu Zanzibar - JUWAUZA uliopo Kikwajuni Mkoa wa Mjini Magharib.

Akitangaza matokeo hayo Mwenyekiti wa Uchaguzi Nassor Said amesema hakuna kura iliyoharibika kwenye uchaguzi huo “ Wajumbe wamepiga kura na hakuna kura iliyoharibika kwa upande wa kura za Mwenykiti “ Amesema Nassor.

Suleiman ameshinda kuwa Mwenyekiti wa CUZA kwa kupata kura 27 kati ya 42 huku akimshinda aliyekuwa Mwenyekiti wa zamani Hafidh Hamid Soud ambaye alipata kura 17.

Akitoa shukrani baada ya kutangazwa mshindi amesema “Nafasi hii itanipa nguvu ya kutafuta fursa nyingi za kukisaidia chama kuwa na miradi wezeshi ili kukiwezeshe kufikia malengo makubwa” Amesema Suleiman.

Mkutano huo ambao ulihudhuria na wajumbe kutoka Unguja na Pemba ambao ni zaidi ya 40 walikuwa wanajadili juu ya masuala kuongeza wanachama ,kuongeza kipengele cha kanuni ambayo itaongeza Makamo Mwenyekiti kwenye Chama ,mapato na matumizi .

Akifungua kikao hicho Mwenyekiti mstaafu Hafidh Hamid Soud amesema Chama bado kina wanachama kidogo ni vyema viongozi waliopo kwenye mikoa na wilaya kuwashirikisha viongozi wa vyama vyengind kujiunga kwenye ushirika “Ni lazima tuwahamasishe viongozi wa vyamaa vilivyopo kwenye maeneo yetu wajiunge ili tuwe na nguvu ya kuomba miradi” Amesema Hafidh.

Haroun Ilias Mohd ni Afisa Ushirika mkuu wa divisheni ya Saccos amesema kuna changamoto kubwa sana kwenye Chama Kikuu cha Ushirika Zanzibar kama suala la kubuni na kupata vyanzo vipya ya mapato “ Changamoto kubwa ni elimu ya kuendesha na kubuni miradi ya kupata pesa ” Ameendelea kusema kwamba ni vyema viongozi wapate nafasi ya kutoka na kujifunza nje ya Zanzibar .” Kutoka ni kujifunza na kufahamu jinsi ya wenzao wanavyofanya ili kupata uzoefu na mbinu” Amemaliza Haroun.

Hadi kufikia Machi mwaka huu Ofisi ya Mrajisi wa vyama vya Ushirika Zanzibar imesajili vyama 5,713 huku kati ya hivyo 217 ni saccos za kuweka na kukopa na 5,496 ikiwa ni vyama vya uzalishaji.

Licha ya uchaguzi wa wenyeviti wajumbe hao waliwapigia kura wajumbe saba ambao watawawakilisha katika vikao vya maamuzi ,Khadija Abdallah Mtwana ni miongoni mwa wajumbe hao amesema ataendelea kuwasaidia wanawake kujiunga na vikundi vidogo vya ushirika “Mimi haswa lengo langu ni kuwasaidia wanawake na nishaanza kufanya hivyo na nitaendelea kwa sababu nimepata tena nafasi ya kuwa mjumbe “ Amesema Khadija.

Post a Comment

0 Comments