JUKWAA la walimu
Wanawake wa kiafrika upande wa Zanzibar (FAWE-ZNZ) limesema litaendelea kutoa elimu ya
jinsia kwa walimu kwasababu bado baadhi yao hawana uelewa wa kuwasaidia
watoto pale wanapokuwa katika majukumu yao ya kazi.
Mjumbe wa Bodi ya FAWE
Zanzibar Khadija Bakar Juma alisema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya
kuwajengea uwezo namna bora ya ufundishaji unaozingatia jinsia kwa
wanafunzi wanaosoma kada ya Ualimu kutoka Chuo cha Kiislam Zanzibar.
Alisema hatua hiyo
itasaidia walimu kuwaelewa wanafunzi na kuweka ustawi mzuri wa watoto hao na
kufikia ndoto zao.
Mjumbe huyo
alifahamisha kuwa ni vyema walimu kujifunza usimamizi wa mabadiliko ya
wanafunzi katika ukuwaji wao, mahusiano baina ya walimu na wanafunzi ili kujua
tabia za wanafunzi wakati wakiwa darasani.
Aidha aliwataka
wanafunzi hao kuongeza matumizi ya lugha katika masomo yao na kujifunza dhana
za kufundisha ili kutekeleza vyema majukumu yao kwasababu uzoefu unaonesha
kwamba baadhi ya wanafunzi wanapokuwa skuli hukabiliwa na vikwazo mbalimbali na
kushindwa kumudu vyema masomo yao.
Mbali na hayo alitumia
fursa hiyo kuwataka mafunzo walioyapata kwenda kuwafundisha na wenzao ili elimu
hiyo iwafikie watu wengi na kuweza kuweka ustawi mzuri wa watoto na taifa kwa
ujumla.
Kwa
upande wake Mratibu wa FAWE Zanzibar Winnifred Yatuwa Mamawi alisema mradi wa
ufundishaji unaozingatia jinsia ni mradi wa majaribio unaotekelezwa na FAWE
Unguja na Pemba kwa lengo la kuondosha matukio ya udhalilishaji katika skuli.
Nae Martin Okhako
kutoka FAWE Nairobi alisema wameona kunahaja kubwa ya kuelekeza mradi huo kwa
walimu kwa lengo la kuleta mabadiliko katika ufundishaji wao.
Mkufunzi wa Mafunzo
hayo Neema Kitundu kutoka FAWE Tanzania bara alisema walimu wanadhamana kubwa
ya kuhakikisha wanasimamia wanafunzi wakati wakiwa darasani, hivyo wanawajibu
wa kuendeleza ujuzi zaidi ili kupata mbinu bora za kufundisha.
Kwa upande wa
wanafunzi hao walisema mafunzo hayo yamewafunda baadhi ya matendo ambayo
hawakujua kama ni udhalilishaji, hivyo waliahidi kuyatumia vyema mafunzo
waliopatiwa pale wanapotekeleza majukumu yao ili kuweka mustakabali mwema kwa
wanafunzi na kuchochea maendeleo yao.
Mafunzo hayo ya siku
nne yameandaliwa na FAWE Zanzibar ikiwa ni moja ya utekelezaji wa mradi wa
kukuza ubora wa elimu kwa watoto wa kike unatekelezwa na FAWE Zanzibar.
0 Comments