Ticker

6/recent/ticker-posts

Sheria Ya Habari Zanzibar Kizungumkuti

 



Na Thuwaiba Habibu.


Katika jamii, miongoni mwa watu ambao huwa wanyonge ni mayatima, hasa wale ambao wazee waliiga dunia wakiwa wadogo.

Hali huwa mbaya zaidi pale yatima akijikuta hana pahala pa uhakika pa kupata msaada wa malezi na mahitaji ya kila siku ya maisha.

Sura hii ya kusikitisha unaweza kuifananisha na inayowakuta waandishi wa habari wa Zanzibar.

Kwa zaidi ya miaka 20 waandishi wa habari wa Visiwani wamekuwa wakililia marekebisho ya sheria za habari ili  kufanya kazi kwa usalama kama wenzao wa sekta nyengine.

Kwa bahati mbaya maombi yao yamekuwa yanapigwa dana dana na kila siku kutolewa ahadi za ombi lao kupatiwa suluhisho ili wafanye kazi kwa amani na furaha.

Kilio cha waandishi wa habari wa Zanzibar kinatokana na misukosuko wanayokumbana nayo kila siku wakati wakiwa kazini.

Bughudha hii ni pamoja na kuporwa vifaa vya kazi kama kamera, simu, chombo cha kunasia sauti, kitabu, kalamu na fedha .

Wakati mwengine hii huenda sambamba na kupigwa au kufunguliwa mashitaka yasiokuwa na kiuchwa wala miguu.

Njia pekee ya kutokea mabadiliko na waandishi wa habari kujioona salama na mchango wao kwa taifa unathaminiwa ni kuwa na mzazi atayelinda maisha na maslahi yao.

Huyu mzazi unayeweza kusema atasaidia Kuweka mazingira ni sheria nzuri anaonekana kutojali. Wakati kila siku unasikia sheria mbali mbali zinarekebishwa hizi za habari zinazungushwa kama pia.

Wanaambiwa waandishi wa habari  kila siku ni kesho…kesho…kesho.

Imeshakuwa miaka mingi  sasa wanahabari wanalilia  sheria ambazo ndani yake vipo vifungu vinavyokandamiza uhuru  wao wa kupata  kutoa habari.

Hii inapelekea watu wa Zanzibar kukosa taarifa za ukweli na wanapokuwa na  matatizo kutoweza kuyatoa kwa vile vyombo vya habari vimebanwa.

Vikwazo hivi ni pamoja na kuwepo  sheria kuu mbili zinazosimamia taaluma ya habari kuwa sio rafiki. Nazo ni Sheria ya usajili wa wakala  wa habari za magazeti na vitabu namba 5 ya 1988 iliyofanyiwa marekebisho ya kubana zaidi na sheria  namba 8 ya 1997.

Sheria nyengine ni ya Tume ya utangazaji , namba  7 ya 1997 iliyofanyiwa marekebisho na sharia namba 1 ya 2010.


Kwa bahati mbaya kila sheria inayohusu taaluma ya habari ikirekebishwa basi badala ya kuleta afueni huwa ni kubana zaidi waandishi na vyombo vya habari.

Licha ya marekebisho  yaliofanyiwa sheria hizi  bado vipo vifungu visivyotoa uhuru wa kutoa  taarifa na kujieleza na kutoa nafasi ya kuuficha ukweli wa jambo kwa vile wana habari kupitia baadhi ya vifungu vya sheria wanajikuta hawawezi kuifanya kazi yao ipasavyo.

Haya yanafanyika wakati Tanzania ikiwa imeridhia mikataba mingi ya kikanda na kimataifa yanayosisitiza umuhimu wa uhuru wa habari na wa kujieleza.

Mikataba hii ni pamioja na ule wa kimataifa wa haki za binadadamu wa 1948 ambao umebainisha kuwa  uhuru wa kujieleza.


Mkataba hu unaeleza wazi wazi kuwa kila mtu ana haki ya kujieza, kupokea maoni na kusambaza bila ya vikwazo.


Mkataba mwengine unaeleza haki za kiraia na kisiasa  wa 1966 ambao unaeleza kuwa kama italazimika kuwepo  vikwazo ni mambo mawili tu. Nayo ni kuheshimu faragha ya mtu  na usalama wa taifa.

Kwa mujibu wa takwimu zinazoelezwa mara kwa mara ni yapo matukio manne ambayo ni vielezo vya wazi vya kutowatendea haki waandishi wa habari na vyombo vyao.

Hii ni pamoja na kufungiwa kwa Swahiba fm, kutekwa nyara kwa Salma Said, vikwazo alivyopata Yassir Mkubwa, na changamoto alizopata Ali Salehe.

Hapa unajiuliza kama kweli waandishi hawa walikuwa wamevunja sheria kwa nini mahakama isitumike kufanya uamuzi na badala yake wawepo watu ndio wanaoamua kama vile Zanzibar inazo mahakama zisio rasmi?

Kwa mtazamo wa wana taaluma wengi ipo haja ya kufanya  mapitio  na kuja na mabadiliko. Hapa Zanzibar inafaa kuchota uzoefu uliopatika katika nchi za jirani na kwengineko ili kuwa na sheria zenye haki na zinazokwenda na wakati.

Huwezi kusema unao utawala bora wakati uhuru wa habari unafinywa na ule wa kujieleza unaminywa.

Waandishi wa habri na viongozi wa serikali wamekuwa na msururu wa vikao vya kujaribu kupata muwafaka, lakini vikao vyote hivyo havijaonekana sio kuzaa magunda tu, bali hata kuchomoza maua yake.


Kinachosikika kila kukicha ni serikali ipo katika mchakato wa kufanya marekebisho.

Wakati mabadiliko ya sheria nyingi za nchi huchukua wiki  au miezi kurekebishwa hizi zinazogusa habari zimekuwa na safari ya zaidi ya miaka 20 na mwanga wa kupatikana ufumbuzi haujachomoza.

Mwana habari mkongwe na Zanzbar ambaye amekuwa mstari wa mbele kuonyesha udhaifu uliopo katika sheria za hivi sasa, Shifaa Said Hassan,   ambaye ni afisa mwandamizi wa Baraza  la Habari Tanzania katika ofisi za Zanzibar alisema

wamewaambia viongozi  mbali mbali juu ya umuhimu wa kuwa na sheria mpya ya habari

‘’Kamati tumeonana na tume  ya marekebisho ya sheria,wizara husika  mara kadha na kukutana na waziri  tarehe 22 Septemba 2023. Mnamo tarehe  29 Ramadhani tulikutana tena na tume ya marekebisho ya sheria na kukiri kuopekea mapendekezo ya  mswada mpya wa sheria’, alieleza.

Hata hivyo, wapi safari ya kuelekea kuwa na sheria bora ya habari umefikia ni kizungumkuti

Kwa muhtasari kinachoendelea ni kila kukicha kusikia serikali ipo mbioni kufanya marekebisho. Wapi mbio hizo zimefikia hakuna anayejua.

Kauli za serikali kuwepo mbioni kufanya marekebisho zilisikika kwa mara nyengine mapema mwaka 2023 na kurejewa kila baada ya wiki chache.

Katika maadhimisho ya Siku ya Habari Duniani ya hivi karibuni kauli ilikuwa hio hio…. Tupo mbioni.

Kwa sasa wana habri wanajiona kutofautiana na mayatima na hawaelewi wapi watapata msaada wa kuona Zanzibar inayo sheria rafiki za taaluma ya habari

Mkurugenzi wa Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania .(Tamwa ), Dk. Mzuri Issa, alisema  anatamani kuona tasnia ya habari inaenda mbele na inaleta mvuto zaidi.

Alikumbusha kuwa habari ni kitu muhimu na uhuru wa  kujieleza ni haki ya ambayo kila  mtu  amezaliwa nayo na sio haki kumpokonya.

Alisema Zanzibar imekuwa na historia ndefu ya kuvutia ya shughuli za habari, lakini kwa sasa imerudi nyuma .

Hapo zamani Zanzibar ilikuwa na vyombo vingi vya habari na watu walifurahia utamaduni huo.


Lakini kwa sasa utamaduni huo umepotea na miongoni mwa sababu zilizopelekea kuwepo kwa hali hii ni kutoku wa na sheria rafiki za habari.


Alisitiza umuhimu wa kuwepo  mashirikiano na watunzi wa sera na serikali kufufua sekta hii ili kuwapa nafasi wandishi kuandika vizuri habari na kuelimisha umma juu ya masuala mbali mbali .

Mwandishi mkongwe na mwalimu wa waandishi wa habari hapa nchini na nje,  Salim Said Salim, aliwasihi wanahabari kutokata tamaa na kuendelea kudai haki yao ya kuwa na uhuru wa kukusanya na kusambaza habari kwa usalama.


"Mwaka  jana tulikutana  na kamati  ya baraza la wawakilishi takribani masaa manne  na kujadiliana. Tukio hilo lilitupa matumaini kwamba ndoto yetu ya kupata marekebisho mazuri ya katiba itakuwa ya kweli’’, aliongeza.


Alisema ni muhimu kwa waandishi kuendeleza kilio chao, ijapokuwa hali ya sasa ni afadhali kuliko ya miaka michache iliopita’’, aliongeza.


Mwana habari mkongwe, Hawra Shamte alisema lazima kuwe na msisitizo wa upatikanaji wa sheria mpya za bahari  ili uhuru wa habari na haki ya kujeleza ipatikane na kuchangia maendeleo ya nchi.

Post a Comment

0 Comments