Na Ahmed Abdulla, Zanzibar
Katika zama hizi za teknolojia na
habari zinazoenea kwa kasi, uhuru wa kujieleza ni msingi wa demokrasia,
uwajibikaji wa viongozi na maendeleo ya kijamii. Haki hii ni dhamana
inayotambuliwa kimataifa na inahitajika kulindwa na sheria rafiki kwa vyombo
vya habari na wanahabari.
Lakini visiwani Zanzibar, hali ni
tofauti. Kwa zaidi ya miongo mitatu, Sheria
ya Wakala wa Habari, Magazeti na Vijarida Na. 5 ya 1988 bado ndiyo
inasimamia sekta ya habari, huku wadau wakipaza sauti wakitaka mabadiliko
yanayohakikisha uhuru wa kweli wa kujieleza.
Sheria hiyo inahitaji vyombo vya
habari kupata ruhusa kabla ya kuanzishwa na inampa Waziri mamlaka ya
kusimamisha au kupiga marufuku magazeti kwa maslahi ya taifa, mara nyingi bila
utetezi wa mchapishaji.
Wakati Zanzibar ikiwa bado haijapata
sharia inayotoa uhuru wa moja kwa moja kwa vyombo vya habari lakini yapo
mataifa ambayo yana sharia bora za habari.
Miongoni mwa mataifa hayo kwa upande wa Afrika ni
pamoja na Afrika Kusini ambayo
Sheria yao ya habari Promotion of
Access to Information Act (Sheria ya Kukuza Upatikanaji wa Taarifa) ya mwaka 2000 inaruhusu raia kupata
taarifa kwa urahisi kutoka kwa taasisi za umma, ikichochea uwajibikaji wa
serikali.
Nchi ya Ghana
imejipambanuwa kwenye sharia bora ya habari Sheria ya Right to Information Act (Sheria ya Haki ya
Kupata Habari)
ya 2019 imeimarisha haki ya raia na wanahabari kupata habari bila vikwazo.
Afrika Mashariki ipo nchi ya Kenya ambayo Katiba yake ya
mwaka 2010 inatambua uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata taarifa kama
haki za msingi za binadamu.
Lakini
mbali na katiba lakini sheria zake za habari zinatoa uhuru wa moja kwa moja wa
habari ikiwa ni pamoja na Sheria ya Upatikanaji wa Habari ya mwaka
2016.
Kifungu
cha 5(1) kinaeleza kuwa “Kwa mujibu wa kifungu cha 6, shirika la umma litalazimika”
(a)
kuwezesha upatikanaji wa taarifa zinazoshikiliwa na chombo hicho na
taarifa ambazo zinaweza kujumuisha.
Mbali na kuwepo kwa nchi hizo zenye
sharia bora kwa Bara la Afrika lakini pia baadhi ya viongozi mbalimbali duniani
wamenukuliwa wakisema maneno yaliyojaa dhamira ya kutaka uhuru wa habari katika
ulimwengu.
Barack
Obama Rais wa zanani wa Marekani
alinukuliwa akisema kuwa “Vyombo vya
habari huru si tishio kwa serikali nzuri; ni daraja la uwajibikaji.”
Kwa upande
wa Justin Trudeau
Waziri Mkuu wa Canada yeye alinukuliwa akisema “Serikali inapaswa kuogopa kukosa ukosoaji, si kukosolewa.”
Kofi Annan Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa zamani yeye alisema kuwa
“Uhuru wa vyombo vya habari ni msingi
wa amani na maendeleo ya kijamii.”
Nelson
Mandela Rais wa zamani wa Afrika Kusini naye alisema “Sio tu tunahitaji uhuru wa siasa bali pia uhuru wa kusema ukweli.”
Angela
Merkel Kansela wa zamani wa Ujerumani
alisema “Demokrasia haiwezi kustawi
bila vyombo vya habari huru na huru.”
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984,
kupitia Kifungu cha 18, inatambua haki ya kila mtu ya kupata na
kusambaza taarifa bila kuingiliwa.
Pia Zanzibar ni
sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imeridhia mikataba muhimu ya
haki za binadamu ikiwemo Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (ACHPR) na Mapendekezo ya UNESCO kuhusu Upatikanaji wa Habari lakini hata
hivyo, sheria ya 1988 haijaendana na misingi hii.
Salma Said, mwandishi wa habari za maendeleo na mkurugenzi wa jumuiya
ya waandishi wa habari za maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA), alisema kuwa mazingira
ya uandishi wa habari visiwani Zanzibar bado hayatoi uhuru wa kweli kwa
wanahabari.
“Nimeshuhudia
mara kadhaa waandishi wakijikuta mikononi mwa polisi, wakitishwa au hata vyombo
vyao kufungiwa, hasa wanapoandika habari zinazogusa mamlaka au viongozi wa
juu,” alisema Salma.
Aidha aliongezea kuwa hali hiyo
imewafanya baadhi ya waandishi kuishi kwa hofu, na badala ya kuisemea jamii kwa
uhuru, wanajikuta wakifanya kazi kwa kusita au kwa kumfurahisha mtu mmoja.
“Changamoto
hizi zinatokana na vitisho vinavyozidi kushamiri, huku kukiwa hakuna sheria
madhubuti ya kuwalinda wanahabari licha ya uwepo wa mikataba na matamko ya
kimataifa yanayotambua haki zao,”
aliongeza Salma.
Kwa upande
wa Khairat Haji, kutoka Chama Cha Waandishi wa
Habari Wanawake Zanzibar, TAMWA-Zanzibar, alieleza kuwa sheria zilizopo za
habari visiwani Zanzibar zimekuwa kikwazo kwa uhuru wa uandishi, na kuwaweka
waandishi katika mazingira magumu ya utendaji.
“Waandishi wanapaswa kuendelea kupaza sauti juu ya
ucheleweshaji wa mabadiliko ya sheria, na kusukuma mchakato wa marekebisho
ufanyike kwa wakati.” Alieleza
Aidha, alitambua mchango wa vyombo
vya habari vya kijamii katika kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa sheria bora
za habari:
“Redio za
jamii zinafanya kazi kubwa ya kutoa uelewa kuhusu sheria za habari, jambo
linalosaidia hata jamii za vijijini kufahamu haki zao na kushiriki katika
mjadala wa kitaifa.” Aliongeza
Ripoti ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) Zanzibar ya mwaka 2022/2023
inaweka wazi hali ngumu inayowakabili wanahabari katika kutekeleza majukumu yao
visiwani. Ripoti hiyo inaeleza kuwa:
“Ofisi ya
MCT Zanzibar ilirekodi jumla ya matukio 25 ya vitisho na vitendo vya
unyanyasaji dhidi ya waandishi wa habari kwa mwaka wa 2017/2018. Matukio haya
yalihusisha kunyimwa taarifa, unyanyasaji wa kimwili, waandishi kuzuiwa
kuripoti baadhi ya matukio kwa sababu za kisiasa, na kunyimwa kadi za
utambulisho.”
Ingawa ripoti hiyo ilichapishwa
miaka ya nyuma, bado inaonyesha mifumo na changamoto zinazodumu, hasa kutokana
na kutokuwepo kwa sheria rafiki ya habari inayolinda uhuru wa vyombo vya habari
na wanahabari wenyewe.
0 Comments