Ticker

6/recent/ticker-posts

Michezo Sio Suala La Jinsi Kila Mmoja Ana Haki Ya Kushiriki – TAMWA -ZNZ.

Baadhi ya Waandishi wa Habari Wakiwa katika mafunzo kwa vitendo kwenye mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo juu ya kuripoti habari zitakazosaidia upatikanaji wa maendeleo ya kimichezo kwa wanawake


Na Najjat Omar, Zanzibar:

Utafiti wa Taasis ya Wanawake kwenye michezo nchini  Marekani (Women’s Sport Foundation) inaonesha kwamba wasichana ambao wana umri wa miaka 14 huacha kuendelea kwa michezo ikiwa tofauti na wavulana kwenye umri huo huo kuendelea kwenye michezo.

Utafiti huo unaonesha kuwa hamasa katika familia inakosekana ndio sababu kubwa ya wasichana kuacha michezo huku karibu wasichana milioni 1.3 hushiriki michezo wakiwa skuli kati ya umri wa miaka 5 hadi 13.

Huku kati hao milioni 1.3 ni asilimia 43 tu ndio huanza michezo wakiwa skuli na kujiona wanamichezo, asilimia 68 wanakuwa na hofu ya kuhukumiwa kuwa kwenye michezo,asilimia 61 wanakuwa na hofu ya kuwa na ujasiri ,huku asilimia 47 wakipata msukumo wa kuendelea na masomo ya skuli na  asilimia 43 wanahisi hawako salama kushiriki kwenye michezo.

Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ambayo ni 17 huku lengo namba 5 linazungumzia “Usawa wa Jinsia” hii ikawa na maana kufanikisha usawa wa jinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana wote.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani ulifanyika June 2023 hapa Zanzibar unaonesha kuwa kuna vikwazo vinavyorudisha nyuma wanawake na wasichana kushiriki kwenye michezo ni kutokana na dhana potofu,uhamasishaji mdogo,mtazamano wa kidini pamoja na ushirikishwaji wa jamii kwenye hili.

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar -TAMWA -Z kimewakutanisha waandishi wa Habari 20 ambao wanafanya kazi katika radio za jamii, magazeti,mitandao pamoja na vyombo vya habari vilivyopo mjini kuwapatia mafunzo ili kuweza kuwawesha waandishi kuandika habari za jinsia kwenye maendeleo ya kimichezo .Akizungumza juu ya mafunzo haya Afisa Mradi wa Masuala ya Jinsia na Michezo -Khairat Haji amesema mafunzo haya ya masuala ya Michezo na jinsia ni mafunzo maalum ambayo yatawezesha waandishi wa habari kuandika na kuripoti habari zinazohusu masuala ya michezo “Waandishi wanaandike na wahamasishe wanawake na wasichana juu ya kushiriki kwenye michezo yote na kusiwe na utofauti wa masuala ya michezo kwa upande wa wanawake kuwekwa nyuma na kutokuzungumziwa”  Amesema Khairat.

Makame Amir Mgeni ni Mwalimu na Mtalaam wa masuala ya michezo wa amekutana pia na waandishi hao wa habari na ambao wapo kwenye mafunzo hayo na kutoa uzoefu wake juu ya kuwa mwalimu kwenye michezo  amesema bado jamii ina mawazo ya kuwa wanawake na wasichana hawawezi kushiriki kwenye michezo kwa sababu ya maumbile “Ni lazima wakati mkiwa mnaandika basi muandike kwa kuonesha faida zaidi zinazopatikana katika michezo zaidi na sio mapungufu yake kwani kutokuonesha faida kunaweza kuendelea kuwarudisha nyuma wasichana kujiunga kwenye michezo”.Amesema Makame wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Waandishi hao ambao wamekaa siku tano katika mafunzo yaliyojikita kwenye masuala ya Michezo na jinsia kwa kuangalia zaidi michezo na maendeleo endelevu,Hawra Shamte ni mwandishi mkongwe ambaye alikuwa  mkufunzi  kwenye mafunzo hayo amesema waandishi wanajukumu la kuandika changamoto zinawakatisha tamaa wasichana kuingia kwenye michezo “Wapo wasichana wengi wenye ndoto za kuwa kama Serena Williams ila ndoto zao zinakatishwa kwa sababu ya dhana na imani za kidini pia “ Ameendelea kusema kuwa ushirikishwaji wa kijinsia hauhusiani na masuala jinsia ila inahusiana na uthubutu na ushirikishwaji.

Donisia Thomas ni mwaandishi wa habari za michezo ambaye ni mmoja wa washiriki katika mafunzo haya amesema bado jamii inaamini masuala ya michezo ni uhuni na elimu zaidi inatakiwa kutolewa “Dhana ya uhuni sio tu kwa wasichana wanaoshiriki bali hata kwa waandishi wa habari wanawake pia wanafikiriwa kuwa ni wahuni kitu ambacho kinarudisha nyuma”Amesema Donisia.

Wadau wengine ambao wapo kwenye mradi huu ni pamoja na Jumuiya ya wanasheria wanawake Zanzibar – ZAFELA,Kituo cha Majadiliano ya Vijana -CYD na Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Zanzibar – TAMWA -Z  mradii huu wa mwaka mmoja umefadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kwa mashirikiano ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.


Post a Comment

0 Comments